Mgogoro Msumbiji: WFP yasema raia walazimika kutorokea Tanzania

Chanzo cha picha, AFP
Kaskazini mwa Msumbiji, mapigano yanaendelea na kuongezeka hali ambayo imelazimisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao.
Sasa hivi idadi kubwa ya raia hao wanakimbilia nchi jirani ya Tanzania kulingana na mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani eneo la Kusini mwa Afrika alipozungumza na BBC.
Makadirio kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa na wadau wengine ni kwamba idadi ya kundi hilo la wakimbizi ni karibu watu 1000.
Aidha kulingana na Shirika la Chakula Duniani, sasa hivi serikali ya Tanzania ndio inayosimamia mahitaji ya kundi la wakimbizi walioingia nchini humo kutoka Msumbiji hivi majuzi.
Pia kuna taarifa kwamba unyanyasaji wa haki za binadamu katika eneo la Cabo Delgado umekuwa ukiongezeka huku mapigano kati ya wanamgambo wa Kiislamu na vikosi vya serikali yakiendelea.
Mpaka kati ya Msumbiji na Tanzania ni mto Ruvuma, na eneo la pwani ya bahari. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Msumbiji imeshuhudiwa idadi kubwa ya watu wakilazimika kutoroka makazi yao hasa katika mkoa wa Cabo Delgado huku wengine wakielekea eneo la kusini la Nampula, amesema mkurugenzi wa WFP.
Kulingana na Lola Castro mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani eneo la Kusini mwa Afrika, wiki kadhaa zilizopita Shirika hilo lilipata taarifa kwamba kulikuwa na kundi la watu lililovuka mpaka kutoka mto Ruvuma na kuingia eneo la Mtwara nchini Tanzania.
Inasemekana kwamba baadhi ya watu walitumia boti huku wengine wakiogolea katika mto Ruvuma kuingia nchini Tanzania.
''Usafiri ulizoeleka katika mto Ruvuma ni mtumbwi pia wanavuka kwa kutumia boti hadi visiwani eneo la delta la Msumbiji na Tanzania,'' amesema Lola Castro.

Hatahivyo, tatizo ni kwamba wakimbizi katika eneo la Cabo Delgado na Nampula ambapo kulikuwa na watu karibu elfu 310, idadi hiyo imeongezeka pakubwa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
''Hii imesababishwa na ukosefu wa usalama na mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea. Raia wanatoroka makwao na kuacha kila kitu nyuma, na kinachotatiza zaidi ni kwamba wamekuwa wakiondoka tangu mwezi uliopita, kilele cha msimu wa mavuno
''Na kundi hilo halina chakula wakati ambapo shirika la chakula duniani limekuwa likiwapa chakula kwa karibu mwaka mmoja sasa hadi watakapoweza kurejea kwenye makazi yao na kurejelea shughuli za kilimo,'' amesema Lola Castro.
Shirika la Chakula Duniani limasema raia wa kaskazini mwa Msumbiji wamekuwa wakishuhudia ukosefu wa usalama na mapigano yamekuwa yakiendelea kwa karibu miaka mitatu, raia wameuawa, wametoroka makazi yao na sasa hivi wanakimbilia Tanzania na kuna uwezekano hali ikaendelea kuwa mbaya zaidi pengine wafanikiwe kurejea nyumbani, lakini tayari hali inatarajiwa kuwa mbaya kwa mwaka mmoja kwasababu msimu mwingine wa mavuno unatarajiwa kuwa miezi ya Machi, Aprili na Mei mwaka ujao.

Chanzo cha picha, AFP
Chanzo cha kukua kwa uasi wa kundi la kiislamu
Vita iliyoanza Oktoba 05, mwaka 2017 wakati kundi la waasi walipoteka miji na bandari ya Mocimboa da Praia kwa muda wa siku mbili.
Mji huo ulikuwa kilomita 60 kama maili 32 kusini kutoka katika mji wenye eneo kubwa la maendeleo ya gesi huko Palma na bandari ni muhimu kwa ajili ya mradi wa gesi kwa ajili ya kuisambaza.
Uasi huo uligunduliwa na wakazi wa eneo hilo.
Tangu wakati huo, vita iliongezeka na watu wapatao 1,500 waliuawa na wengine wapatao 250,000 walikimbia makazi yao.
Mji wa Cabo Delgado una waislamu wengi na kuna muhubiri mpya, wote wakiwa ni kutoka Afrika Mashariki na Msumbiji walipata mafunzo kutoka ughaibuni, walianzisha misikiti na kudai kuwa maimamu wa mji huo walikuwa washirika wa Frelimo na walishiriki kuwanyang'anya utajiri wao.
Baadhi ya misikiti hii mipya inatoa fedha kwa ajili ya kusaidia wananchi kuanzisha biashara na kutoa mianya ya ajira - na waislamu walidai kuwa jamii ya waisalmu itakuwa vizuri chini ya uongozi wa Sharia.
Je wapiganaji hao ni kundi lipi?
Kundi hilo linalojulikana nchini humo kuwa al-shabab, ama vijana lina ajenda za Kiislamu , lakini pia linajenga malalamishi kuhusu ukosefu wa ajira, uchaguzi unaokumbwa na udanganyifu, ufisadi na ghasia.
Wapiganaji hao walio watiifu kwa kuundi la Islamic State wamezindua mashambulizi kadhaa katika vijiji na miji katika eneo hilo katika kipindi cha miaka mitatu, kuwaua zaidi ya watu 1500 mbali na kuwawacha 250,000 bila makao, kulingana na Reuters.
Hatahivuo, operesheni za jeshi katika eneo hilo kukabiliana na wapiganaji hao ,ambao waliliteka eneo la kimkakati lenye bandari ya Mocimboa da Pria mwezi Agosti limehusishwa na unyanyasaji wa kibinadamu.
Wiki zilizopita, Shirika la Amnesty International lilisema kwamba limetathmini na kuthibitisha kanda za video zikionesha watu kuchinjwa, mateso na ukatili mwengine unaofanyiwa wafungwa mbali na kukatwakatwa kwa wapiganaji wanaodaiwa kuwa wa upinzani mbali na mauaji ya kiholela.
Lakini serikali imekana madai ikisema kwamba wapiganaji hao hujulikana kwa kujifanya wanajeshi wa serikali.

Mkoa wa Cabo Delgado, unamiliki mradi mkubwa wa gesi barani Afrika.
Kampuni ya Exxon Mobile ni mwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa mardi wa gesi asilia wenye thamani ya $60bn katika pwani ya mkoa huo.
Kanda ya Video inyaoonesha mauaji ya watuu wasiokuwa na hatia
Hivi maajuzi, kanda ya video imekuwa ikisambaa kwenye mitandai ya kijamii inayoonesha wanaume wanne, mwanamke mmoja mwenye uoga wakiuawa na wale wanaodaiwa kuwa watu waliovalia magwanda ya kijeshi.
Wizara ya ulinzi ilishutumu kanda hiyo kama inayotisha huku ikiapa kujua chanzo chake.
Makundi ya haki za kibinadamu pia yameshutumu mauaji hayo.
Jeshi lake limeshutumiwa kwa unyanyasaji wa haki za binadamu huku likijaribu kuliangamiza kundi hilo la wapiganaji.
Hata hivyo serikali imekana madai hayo.
Pia unaweza kutazama:
































