Kwanini Haaland anaweza kuipaisha Manchester City?

Halaand
Iliyochapishwa

Kocha wa kwanza wa Erling Haaland anakumbuka aliposhangazwa na uwezo wa mchezaji wake huyo wa zamani aliyekuwa na ufahamu mpana wa soka.

Mshambuliaji huyo alikuwa akiifungia Red Bull Salzburg mabao huko Austria lakini jina lake lilipaa zaidi kwenye hatua za michuano ya Ulaya kwa kufunga mabao matatu (hat-trick) katika kipindi cha kwanza kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Genk, Septemba 2019.

"Whoosh!" anasema Alf Ingve Berntsen, kocha aliyemuonesha njia Haaland na kumpa nafasi ya kucheza kwenye ligi ya kiwango cha juu kupitia timu ya Bryne ya daraja la pili huko Norway akiwa na umri wa miaka 15 tu.

"Huu ulikuwa mwanzo wa kuwa mchezaji ambaye kila mtu anamfahamu. Hata mimi, kocha wake wa zamani toka siku za awali, niliona hili ni jambo tofauti."

Haaland akafunga katika mechi zake tano za kwanza za kundi la Ligi ya Mabingwa, akiwa kijana wa kwanza kufanya hivyo, na aliondoka kwenda Borussia Dortmund kwenye dirisha la uhamisho la Januari akiwa amefunga mabao 28 katika michezo 22 ya ligi msimu huo.

"Nimemwona Erling akifunga mabao kwa miaka mingi," Berntsen aliambia BBC Sport. "Lakini sio kawaida unapokua mkubwa unaendelea kufunga. Kiwangpo chake hupaa kila uchwao."

Sasa amesajiliwa na timu kubwa ya Manchester City. akiwa na umri mdogo wa miaka 21 na ndoto kubwa zaidi. Ni wakati mzuri sana kwa mchezaji anayezingatiwa kuwa mmoja wapo wa vipaji vya ushambuliaji vya kufurahisha zaidi duniani.

Halaand
Maelezo ya picha, Halaand alianza kucheza soka la kulipwa akiwa na miaka 15 huko Bryne Norway

Haaland, ambaye mama yake Gry Marita Braut alikuwa mwanariadha, alikuwa sehemu ya kikundi chenye vipaji huko Bryne, na wachezaji wanne kati ya 40 waliofunzwa na Berntsen wakienda kuichezea timu ya taifa katika viwango mbalimbali.

"Alikuwa na mapenzi ya soka lakini watoto wengi wako hivyo," anasema Berntsen. "Alikuwa na kile ambacho nchini Uingereza kinaitwa 'kipaji cha kipekee' . Alikuwa na kitu maalum na alipokuwa uwanjani alikuwa akizingatia kabisa soka.

"Alijifunza tangu akiwa mdogo jinsi ya kuwa mwanasoka, jinsi ya kuishi katika chumba cha kubadilishia nguo, jinsi ilivyo muhimu kujiburudisha lakini kufanya mazoezi mengi.

"Alikuwa na maumbile kamili na familia yake pia ilikuwa nzuri sana kumruhusu kufikiria kwa njia ya mpira wa miguu.

"Tulianza kuongea mapema sana, tangu alipokuwa na umri wa miaka 12, kwamba yeye ni mtu maalum kwa sababu kwa mbinu, kiufundi na kiakili haogopi kamwe, ana uchungu mkubwa na tulijua kwamba katika miaka michache, angekuwa mchezaji mkubwa.

"Alicheza dhidi ya watu wakubwa, wenye nguvu. Aliimarika zaidi na hilo ni muhimu sana. Unapaswa kuwa na mapambano kidogo ili kuwa mzuri - ikiwa kila kitu kinakwenda vizuri sana, ni rahisi sana."

Halaand

Kwanini Haaland anaweza kuipaisha Man City?

Berntsen anasema vilabu vikubwa duniani vilichelewa kuona uwezo wa Haaland alipokuwa Salzburg, ingawa Dortmund imeonekana kuwa mahali pazuri kukuza kipaji chake.

"Nilisema alipokuwa Salzburg kwamba klabu kubwa sita au saba duniani zisipomnunua watakuwa wanafanya makosa makubwa," anasema. "Sidhani kama walijua jinsi alivyokuwa mzuri. Alishangaza kila mtu, lakini tulipoona alikuwa akifunga mabao mengi huko Salzburg, tulisema hakuna wa kumzuia."

Sasa Fjortoft inaamini kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Norway ni miongoni mwa wachezaji wachache wanaoweza kuipeleka Manchester City katika kiwango kingine.

"Pep Guardiola hakuwahi kupenda kucheza na namba tisa," anasema Fjortoft. "Lakini nadhani umeona ukiwa Manchester City katika misimu michache iliyopita kwamba kufanya vizuri zaidi, unahitaji namba tisa.

"Pia ataona wachezaji anaoweza kucheza nao. Akiwa na Bernardo Silva, Kevin de Bruyne, Raheem Sterling na aina hii ya wachezaji, ni jambo la kupendeza kwa mshambuliaji kupata huduma za kumpaisha na kupaisha timu."

Halaand
Maelezo ya picha, Halaand ameifungia timu ya taifa ya Norway mabao 20 katika michezo 21 aliyocheza

Nyota mkubwa na mtu wa watu

Licha ya wasifu wake mkubwa, Haaland bado anaweza kupata wakati wa utulivu anaporudi Bryne anaonekana ni "mtu wa watu".

"Anapokuwa na marafiki zake, yeye ni mtu wa watu," anasema Berntsen. "Lakini inazidi kuwa ngumu kwake kwa sababu hatujawahi kuwa na nyota wa michezo maarufu kama Erling na ana miaka 21 tu, kwa hivyo maisha ya kawaida ni kitu ambacho hawezi kufanya tena.

"Tulikuwa na Solskjaer mwishoni mwa miaka ya 90 lakini alikuwa mchezaji mkubwa kabla ya mitandao ya kijamii. Sasa shinikizo na hamu ya Erling ni kubwa.

"Kwa sababu anatoka mji huu, ilikuwa na maana kubwa kwake kuwa na mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha kwanza na bado ni mfuasi wa timu. Anapokuwa na mapumziko ya wiki kadhaa, bado anarudi nyumbani na kukutana na marafiki na familia yake.

"Hapa Bryne, mji wetu mdogo, atakuwa na aina fulani ya amani, lakini si katika maeneo mengine - atatambuliwa milele. Ikiwa atakuja nyumbani na kufanya mazungumzo au kupumzika na marafiki zake, ni kijana wetu.

"Bila shaka ninajivunia; sote tunajivunia. Ninajivunia kundi hili lote kwa sababu limekuwa kundi la watu wazuri na wenye heshima. Hilo ndilo lililo muhimu zaidi", Anaseme Berntsen.