Sadio Mane: Nyota wa Senegal anayetarajiwa kufanikiwa Bayern Munich

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshindi wa Ligi Kuu, Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia la Vilabu akiwa na Liverpool, Sadio Mane sasa anaanza ukurasa mpya wa maisha yake huko Bayern Munich.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alijiunga na wababe hao wa Ujerumani kwa ada ya £35m baada ya miaka sita Anfield, ambapo alifunga mabao 120 katika michezo 269.
Mane, ambaye alikuwa muhimu kwa ushindi wa Senegal wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi Februari, alifunga bao lake la kwanza la ushindani akiwa na Bayern huku klabu hiyo ya Bavaria ikishinda Kombe la Super Cup la Ujerumani Jumamosi iliyopita.
Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Efan Ekoku anatoa pongezi kwa Mane kwa kuzoea Bundesliga na kuwa kivutio kwa mabingwa hao mara sita wa bara la Ulaya.
"Nadhani kama mchezaji wa kiwango cha juu na cha kimataifa, atafanikiwa Bayern kwa hakika," Ekoku aliiambia BBC Sport Africa.
"Amefanya chaguo zuri. Ikiwa utaondoka katika klabu kubwa kama Liverpool na kama bado uko kwenye kiwango kizuri, basi unapaswa kuchagua kwa busara.
"Mane amefanikiwa na sasa amekwenda kwenye klabu yenye historia kama Liverpool, katika kipindi cha miaka 40 hadi 50 iliyopita, huko Bayern. Uwezekano wa yeye kufanikiwa katika ligi ya Bundesliga akiwa na Bayern ni mkubwa vile vile, tena zaidi."
Baada ya kucheza Metz, Red Bull Salzburg na Southampton, Mane alihamia Liverpool mwaka 2016 na kufanikiwa kufunga mabao 90 ya Ligi Kuu ya England akiwa na Reds, akimaliza msimu wake wa mwisho akiwa na mabao 23 katika michuano yote.
Je, Mane atahitaji muda zaidi akiwa na Bayern?

Akichukua nafasi ya gwiji wa Bayern Robert Lewandowski

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Msimu wa 2021-22 ulikuwa wa mafanikio kwa Mane, ambaye alishinda Kombe la Mataifa na Senegal kabla ya kusaidia Liverpool kushinda Kombe la Ligi na Kombe la FA na kumaliza washindi wa pili katika Ligi ya Premia na Ligi ya Mabingwa.
Atachukua nafasi ya Robert Lewandowski katika klabu ya Bayern, huku mchezaji huyo wa kimataifa wa Poland akihamia kwa wababe wa Uhispania Barcelona.
Lakini Zakuani anaamini kuwa kuwasili kwa mchezaji bora wa mwaka kwa wanaume wa Kiafrika ni mchezaji tofauti kabisa na Lewandowski mwenye umri wa miaka 33, ambaye alifunga mabao 344 katika michezo 374 akiwa Allianz Arena.
"Sidhani kama inaweza kulinganishwa na Mane kucheza zaidi akitokea pembeni, lakini rekodi yake ya mabao ilikuwa nzuri hivi karibuni akiwa na Liverpool.
"Tukielekea Bundesliga, pengine watamtarajia kuhusika na wingi wa mabao kwa sababu ya ada ya uhamisho, kwa sababu vilabu vingi vya Ujerumani huwa havina tabia ya kulipa aina hiyo ya fedha."
Ekoku, mchezaji wa kwanza kufunga zaidi ya mabao matatu kwenye mchezo wa Ligi Kuu na pia Mwafrika wa kwanza kufunga hat-trick katika kitengo hicho, alisema.
"Sidhani kama ni kubadilishana moja kwa moja. Sidhani kama kuna wachezaji wengi kama Lewandowski katika soka la dunia," alisema.
"Lakini nadhani (kocha wa Bayern) Julian Nagelsmann anatafuta aina tofauti ya mashambulizi ya Bayern. Sote tuliona alichokifanya akiwa RB Leipzig. Na hivyo pengine ni kujenga washambuliaji wadogo na kuwa na wachezaji kama Mane, na Serge Gnabry. na Leroy Sane, ambao wanaweza kubadilishana.
"Nadhani hivyo ndivyo Bayern watakavyocheza siku za mbeleni. Ikiwa unataka kupata aina ya mchezaji kama Lewandowski hivi sasa, hakuna anayeweza kusema ni nani haswa anaweza kuwa kama yeye.
"Wanatazamia siku za usoni na Mane ni mdogo kwa miaka michache kuliko Lewandowski kwa hivyo kutakuwa na utofauti, lakini mtindo wa Mane, unafaa kabisa."

































