Roy Hodgson asikitishwa na kauli yake
Meneja wa Liverpool Roy Hodgson, amewaomba msamaha mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kauli yake baada ya timu hiyo kufungwa na Wolves nyumbani na akaahidi hataondoka.

Kufungwa mara ya nane siku ya Jumatano kwa Liverpool msimu huu na timu ambayo inachungulia lindi la kushuka daraja, kulisababisha timu hiyo kuzomewa, hali iliyomfanya Hodgson kutoa wito wa kuungwa mkono zaidi.
"Nimesikitishwa na kwa kweli nasikitika kama matamshi yangu yamewakera mashabiki kwa namna yoyote ile," Alisikika akisema Hodgson siku ya Ijumaa.
"Jambo la mwisho katika mawazo yangu ni kuondoka katika klabu kama mambo yanakuwa namna hii," aliongeza Hodgson.
Kuelekea kupoteza mchezo dhidi ya Wolves, ambayo haikuwahi kushinda mchezo wa nje msimu huu, mashabiki walisikika wakiimba kwa mzaha "Hodgson kwa England" huku wakihanikiza kuimba jina la meneja wa zamani Kenny Dalglish.
Baada ya mchezo huo, Hodgson alionekana kupendekeza nguvu hizo za mashabiki zielekezwe kuipa moyo timu.
Mmiliki wa klabu ya Liverpool John Henry, sasa anakabiliwa na chagizo kubwa. Jee anayatilia maanani maneno ya mashabiki wanaomtaka kumtimua meneja au ataendelea na mikakati yake ya muda mrefu na kusubiri hadi msimu mpya wa joto ndipo afanye mabadiliko?



























