Tunisia yaanza kuomboleza

Tunisia imeanza kuomboleza kwa siku tatu kuwakumbuka waliofariki dunia kwenye ghasia zilizosababisha kukimbia kwa Rais Zine al-Abidine Ben Ali.
Takriban watu 78 waliuawa tangu maandamano yalipoanza mwezi Januari.
Serikali mpya ya mpito imekabiliwa na mfululizo wa maandamano kupinga chama cha Bw Ben Ali, RCD, kubaki madarakani.
Imethibitisha kuwa itatambua vyama vya upinzani vilivyokuwa vimepigwa marufuku na kutoa msamaha kwa wafungwa wa kisiasa.
Tangazo hilo limetolewa wakati serikali ilipoitisha mkutano wake wa mwanzo wa baraza la mawaziri.
Mapema wiki hii mawaziri walisema wafungwa wote wa kisiasa waliachiwa huru.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International lilifurahishwa na hatua hiyo, lakini likasema limepokea taarifa kuwa idadi kubwa ya wafungwa wa kisiasa wenye uhusiano na chama cha kiislamu kilichopigwa marufuku cha Ennahda bado wametiwa kizuizini.
Serikali mpya ya Tunisia imeahidi kufanya uchaguzi wa huru na wa haki katika kipindi cha miezi sita lakini bado haijatolewa tarehe.
Katiba inasema lazima uchaguzi ufanyike katika kipindi cha miezi sita.
Kulikuwa na maandamano mjini Tunis siku ya Alhamis karibu na ofisi za chama cha Ben Ali RCD, pamoja na miji ya Gafsa na Kef.































