Nani kutocheza soka hadi mwezi wa Aprili

Iliyochapishwa

Winga wa Manchester United, Nani hatacheza soka kwa wiki tatu zijazo kutokana na kuumia mguu.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno, alilazimika kutoka nje ya uwanja, Manchester United ilipolazwa 3-1 na Liverpool siku ya Jumapili baada ya kupata jeraha kubwa mguuni alipokabiliwa na mlinzi wa Liverpool Jamie Carragher.

Kwa mujibu wa meneja wa Manchester United:"Ni vigumu kueleza hasa atakuwa tayari kurejea uwanjani, lakini hataweza kucheza mechi dhidi ya Bolton siku ya Jumamosi ijayo."

Ni wazi hatacheza katika robo fainali ya Kombe la FA siku ya Jumamosi dhidi ya Arsenal, na pia mechi ya Jumanne dhidi ya Marseille.

"Kidonda kimeshonwa, hiyo ndio habari njema. Kilichokuwa kikitupa wasiwasi ni kupata maambukizi," aliongeza Ferguson.

"Uvimbe umepungua, nayo pia habari njema - lakini kukufahamisha tarehe kamili lini atarejea kucheza soka, ni vigumu sana.

Nani mwenye umri wa miaka 24, aliyejiunga na Manchester United mwezi wa Juni 2007 akitokea klabu ya Sporting Lisbon, aliaumia muda mfipi kabla ya mapumziko katika mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Liverpool tarehe 6 mwezi wa Machi, wakati rafu zilipoanza kuibuka baina ya wachezaji wa timu hizo mbili.

Wachunguzi wengi wa soka wanahisi Carragher angepaswa kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja, kuliko kuoneshwa kadi ya njano kutoka kwa mwamuzi Phil Dowd. Carragher baada ya mechi mara moja alimuomba radhi Nani.

Mwezi wa Novemba Nani aliumia nyonga na pia hakucheza fainali za Kombe la Dunia kuiwakilisha Ureno baada ya kuumia mfupa wa shingo muda mfupi kabla ya kuanza kwa fainali hizo nchini Afrika Kusini mwaka 2010.

Huku Manchester United ikiwa inakabiliwa na mechi muhimu, kukosekana kwa Nani ni pigo kubwa, huku wachezaji 10 wa kikosi cha kwanza huenda wasicheze katika mchezo na Gunners siku ya Jumamosi katika uwanja wa Old Trafford.