Maombolezo yaendelea Orlando,Marekani

Maombolezo yaendelea Orlando
Maelezo ya picha, Maombolezo yaendelea Orlando
Iliyochapishwa

Watu wamekusanyika mjini Orlando nchini Marekani katika shughuli za maombolezo kwa waliouawa katika klabu ya usiku mjini humo.

Takriban watu 50 waliuawa kwa risasi, shambulio linaloelezwa kuwa baya katika historia ya Marekani.

Imamu mkuu wa jamii ya waislamu jimboni Florida,Mohammad Musri amewaambia watu waliokusanyika katika eneo hilo kuwakumbuka watu waliouawa, kuwa waislamu wanaungana nao katika kupinga misimamo yenye chuki,mauaji na yenye kuharibu.

Pia kumekuwepo na salamu za rambirambi kutoka Uingereza,Ufaransa na Canada

Katika hatua nyingine ,Rais wa Marekani, Barack Obama amesema hakuna ushahidi kuwa aliyetekeleza mashambulizi kwenye klabu ya usiku mjini Orlando alikuwa sehemu ya mpango mkubwa wa mashambulizi.

Obama ameeliezea shambulio hilo kuwa lilisukumwa na msimamo binafsi wa mshambuliaji huyo na hakuna ushahidi kuwa Omar Mateen alipata maelekezo kutoka nje kutekeleza mauaji.

Mkurugenzi wa shirika la kijasusi FBI,James Comey amesema kuna ishara kuwa Mateen alishawishika kupitia mitandao ya intaneti.Lakini amesema haijulikani Mateen alikuwa akiunga mkono kundi gani la kigaidi.

Naye Mgombea Urais kwa tiketi ya Republican nchini Marekani, Donald Trump amerejea kauli yake akitaka kuwazuia kwa muda waislamu kuingia nchini Marekani.