Maandamano Kenya kuendelea Jumatano ijayo - Azimio

Muungano wa Azimio umetangaza kuwa utarejelea maandamano ya kupinga gharama kubwa ya maisha Jumatano ijayo.

Moja kwa moja

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu, mpaka kesho majaaliwa

  2. Maandamano Kenya kuendelea Jumatano ijayo - Azimio

    Waandamanaji

    Muungano wa Azimio umetangaza kuwa utarejelea maandamano ya kupinga gharama kubwa ya maisha Jumatano ijayo.

    Wakati wa kikao na wanahabari kilichofanyika katika Kituo cha Amri cha SKM Jumamosi, viongozi wa Azimio walisema maandamano hayo yatakuwa ya amani.

    Kiongozi wa Chama cha Usawa Kwa Wote, Mwangi wa Iria, ambaye alikuwepo wakati wa kikao na wanahabari, alisema upinzani hauko tayari kushirikisha serikali ya Kenya Kwanza, na kuongeza kuwa ukatili umetekelezwa kwa baadhi ya raia.

    "Maandamano yetu ya amani yataendelea Jumatano ijayo na tutawajulisha OCS wote nchini," alisema. Wa Iria amekemea mashambulizi ya polisi dhidi ya raia, akiongeza kuwa yalilengwa katika maeneo fulani.

    Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka pia alizungumzia suala la wajumbe wa mkutano kwa waandishi wa habari, akisema, "Wawakilishi na mabalozi wa Marekani wa Uingereza, Denmark na Umoja wa Mataifa walikuja kwenye makazi yangu lakini tulikubaliana kutozungumza na vyombo vya habari." Aliendelea, "Walikuwa na wasiwasi sana kwamba maandamano ya amani yaligeuka kuwa vurugu."

    Kalonzo alisema kiongozi wa Azimio Raila Odinga, Martha Karua wa Narc-Kenya na naibu kiongozi wa chama cha ODM Wycliff Oparanya waliomba radhi kwa kuwa hawakuweza kuhudhuria kikao na wanahabari. Kalonzo alidai kuachiliwa mara moja kwa viongozi na wafuasi wote wa Azimio ambao bado wanazuiliwa.

  3. Malaysia yasitisha tamasha la muziki baada ya wanaume wawili wa bendi ya Uingereza kubusu jukwaani

    w
    Maelezo ya picha, Kundi la muziki la 1975

    Serikali ya Malaysia imesitisha tamasha la muziki katika mji mkuu Kuala Lumpur siku ya Jumamosi, siku moja baada ya mwimbaji wa bendi ya muziki ya pop ya Uingereza The 1975 kumbusu mwanamuziki mwenzake wa kiume jukwaani na kukosoa sheria za nchi hiyo dhidi ya kundi la wapenzi wa jinsia moja (LGBT).

    "Hakutakuwa na maelewano dhidi ya chama chochote kinachopinga, kudharau na kukiuka sheria za Malaysia," Waziri wa Mawasiliano Fahmi Fadzil alisema katika chapisho la Twitter.

    Kundi la The 1975 pia wamepigwa marufuku kutumbuiza nchini Malaysia, ilisema kamati ya serikali ambayo inasimamia filamu na maonyesho ya wageni.

    Mpenzi ya jinsia moja ni uhalifu katika nchi ya Malaysia yenye Waislamu wengi.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya juu ya kuongezeka kwa kutovumilia dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na wale waliobadili jinsia.

    Katika video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Ijumaa jioni, Healy alionekana akimbusu mpiga besi Ross MacDonald baada ya kukosoa msimamo wa Malaysia dhidi ya LGBT katika hotuba iliyojaa lugha chafu kwa hadhira ya tamasha.

  4. Algeria yatuma maombi ya kujiunga na BRICS

    w

    Algeria imetuma maombi ya kujiunga na kundi la BRICS na kuwasilisha ombi la kuwa mwanachama mwenye hisa wa Benki ya BRICS yenye kiasi cha dola bilioni 1.5, Ennahar TV ilimnukuu Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune akisema.

    Imeongeza kuwa Tebboune alisema mwishoni mwa ziara yake nchini China kwamba Algeria imetaka kujiunga na BRICS ili kufungua fursa mpya za kiuchumi.

    Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini ina utajiri mkubwa wa rasilimali za mafuta na gesi na inataka kubadilisha uchumi wake na kuimarisha ushirikiano wake na nchi kama vile China.

    Argentina, Iran, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Cuba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Comoro, Gabon, na Kazakhstan ni miongoni mwa nchi zilizoonyesha nia.

    China itawekeza dola bilioni 36 nchini Algeria katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, teknolojia mpya, uchumi wa maarifa, usafiri na kilimo, vyombo vya habari vya ndani vilimnukuu Tebboune akisema wiki hii.

  5. Daraja la Crimea lafungwa baada ya bohari ya mafuta kushambuliwa - Urusi

    Daraja la Crimea

    Shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye ghala la silaha huko Crimea limesababisha raia kuhamishwa na kutatiza usafiri, mamlaka ya Urusi imesema.

    Sergei Aksyonov, gavana wa Crimea aliyewekwa na Urusi, alisema Ukraine ndiyo iliyohusika na shambulio hilo, bila kutoa ushahidi.

    Bw Aksyonov alisema wakazi wa eneo hilo wanaoishi umbali wa kilomita tano baada ya mlipuko huo walikuwa wakiondolewa.

    Huduma za reli katika daraja la Kerch pia zimeripotiwa kusitishwa.

    Mapema siku ya Jumamosi, viongozi wa Urusi walisimamisha safari kwenye daraja, lakini kwa haraka wakafungua tena kwa ajili ya magari kupita.

    Bw.Aksyonov alisema miundombinu katika wilaya ya Krasnogvardeysky katika Crimea ilikuwa ikilengwa.

    "Kulingana na data ya awali, hakukuwa na uharibifu au majeruhi," Bw Aksyonov aliandika kwenye chapisho la Telegram.

    BBC haijaweza kuthibitisha kwa uhuru shambulio hilo. Wilaya ambayo shambulio hilo liliripotiwa ni zaidi ya kilomita 160 (maili 100) kutoka kwenye daraja la Kerch.

  6. Hofu ya maisha ya mwanafunzi wa Mauritania aliyekamatwa kwa kukufuru

    Kumtukana Mtume Muhammad ni adhabu ya kifo

    Mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mauritania amekamatwa kwa kuandika karatasi ya mtihani akimtusi Mtume Muhammad katika mitihani ya mwezi uliopita.

    Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa mamlaka za kidini zilidai hukumu ya kifo ikiwa msichana huyo ambaye hajatajwa jina lake atapatikana na hatia ya kukufuru.

    Mauritania imeimarisha sheria za kukufuru, zinazoelekeza adhabu ya kifo kwa Waislamu ambao "wanamdhihaki au kumtukana Mungu au Mtume, hata wakitubu".

    Hapo awali watu waliweza kuepuka hukumu ya kifo ikiwa walionesha majuto. Chombo cha habari cha Pan-Arab al-Quds al-Araby kiliripoti Jumatano kwamba mwanafunzi huyo anatoka katika mji wa kaskazini-magharibi wa Atar na anatoka katika kabila la Haratin, ambao ni vizazi vya watumwa wenye asili ya kusini mwa jangwa la Sahara.

  7. Mzozo wa Sudan: Madaktari wachapwa viboko baada ya msafara kushambuliwa - MSF

    Madaktari wa MSF wanatibu majeruhi wa vita kote Sudan - na mpakani mwa Chad ambako wengi kutoka Darfur wanakimbia

    Madaktari katika mji mkuu wa Sudan wamepigwa na kuchapwa viboko na watu wenye silaha ambao walishambulia msafara wao, shirika la madaktari wasio na mipaka, Médecins Sans Frontières (MSF) linasema.

    Timu ya madaktari ilikuwa ikipeleka vifaa katika Hospitali ya Uturuki kusini mwa Khartoum iliposhambuliwa siku ya Alhamisi na gari lao moja kuibwa.

    Tangu vita vilipozuka katikati ya mwezi wa Aprili, ni mojawapo ya hospitali mbili ambazo bado zinafanya kazi kusini mwa jiji Wote wanaungwa mkono na MSF, ambayo inasema msaada wake kwao sasa uko hatarini.

    Mapambano makali ya madaraka katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kati ya jeshi na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) yameharibu vituo vya matibabu jijini.

    'Tishio la kifo'

    Wakati zaidi ya watu milioni tatu nchini kote wamekimbia makazi yao tangu Aprili, mamilioni ya wengine bado wamekwama Khartoum, wakihangaika kupata dawa na usaidizi wa kimatibabu.

    MSF ni mojawapo ya vikundi vichache vya misaada vya kimataifa ambavyo bado vinasaidia hospitali huko Khartoum na mji wake pacha wa Omdurman, kusaidia kuweka mfumo wa afya ambao umekuwa katika matatizo kwa miongo kadhaa.

    Inasema imewatibu zaidi ya wagonjwa 1,600 katika hospitali hizi tangu mzozo huo uanze.

    Lakini shirika la usaidizi lilionya kwamba matukio haya yanaweza kukomesha huduma za msaada kwa sababu ya kuzorota kwa kiasi kikubwa kwa usalama na matukio kadhaa ambayo wafanyakazi wake walikuwa wakilengwa.

    Unaweza kusoma;

  8. Museveni, Muhoozi wakabiliwa na madai mapya ICC- Monitor

    Museveni

    Katikati ya mwezi huu, Bw Bruce Afran, wakili anayeishi Princeton, New Jersey, Marekani aliwasilisha ombi jipya katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) akiiomba mahakama hiyo ichunguze madai kwamba maafisa wa Uganda, akiwemo Kamanda Mkuu wa Jeshi la Uganda (UPDF) na Rais wa Uganda, Jenerali Museveni, pamoja na mtoto wake, Jenerali Muhoozi Kaineruga kuwatesa wapinzani wao katika maeneo mengine ya siri.

    Jumla ya maafisa 26 wametajwa katika ombi hilo ambalo liliwasilishwa wiki moja au zaidi ICC, The Hague, Uholanzi. Kando yake kuna taarifa za kiapo zilizoripotiwa kurekodiwa cha zaidi ya watu 200, ambao wote wanadai kuwa waathiriwa wa uhalifu unaodaiwa.

    Bw Afran aliiambia Monitor kwa njia ya simu kutoka Marekani kwamba ikiwa ICC itakubali ombi hilo, maafisa wengine wa polisi na wanajeshi wa Uganda wanaweza pia kujikuta wakifikishwa mahakamani kwa makosa hayo hayo.

    Jana, Mwanasheria Mkuu Kiryowa Kiwanuka aliiambia Monitor kwa kwamba ingawa serikali haijakabidhiwa rasmi nakala ya ombi hilo, uamuzi wa kuwasilisha katika ICC huenda haukuwa wa lazima.

    "ICC kwa asili yake ni mahakama ya mwisho na inakamilisha tu mfumo wa haki wa nchi iliyotia saini ambapo hawajatoa au hawawezi kutoa Haki," alisema.

    Bw Kiwanuka alisema "hajaona ombi hilo na sijui kilichomo kwenye ombi hilo, lakini kutokana na kile ninachokiona kwenye mitandao ya kijamii ... kuna mwanamke wakili wa Marekani ambaye anashinikiza ICC kufanya uchunguzi kuhusu ghasia za uchaguzi wa 2021 lakini hii ni siasa kwa sababu hii imekuwa kwa miaka mitatu iliyopita."

    "Tayari uchunguzi umefanywa nchini Uganda, kupelekwa mahakamani, watu binafsi walishtakiwa na hata kuhukumiwa," alisema.

  9. Messi afunga bao la dakika za mwisho kwenye mechi yake ya kwanza Inter Miami

    w

    Nyota wa Argentina, Lionel Messi alifunga kwa mkwaju wa faulo dakika za lala salama kwenye mechi yake ya kwanza ya Inter Miami na kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Cruz Azul ya Mexico.

    Messi, 36, alifunga bao hilo katika dakika ya nne ya muda ulioongezwa huku timu yake ya Ligi Kuu ya Soka ikishinda mechi ya Kombe la Ligi.

    Umati huo wa watu watu zaidi ya 20,000 ulijumuisha watu mashuhuri kama vile LeBron James wa mpira wa vikapu, nguli wa tenisi Serena Williams na nyota wa televisheni wa Marekani Kim Kardashian.

    "Tulitaka kuanza hivi kwa kuwapa ushindi watu hawa," alisema Messi.

    Nahodha wa zamani wa Uingereza David Beckham, ambaye ni mmiliki mwenza wa Inter Miami, alitazama mechi ya kwanza ya Messi kutoka juu ya karibu na ukumbi wa kubadili nguo .

    "Kusema kweli, mara tu nilipoona mpira wa adhabu ukitolewa nilidhani hii ndiyo njia ambayo inakusudiwa kumalizika,"

    alisema mchezaji huyo mwenye miaka 48. "Hasa unapokuwa na wachezaji kama Leo na Sergio uwanjani, ndivyo wanavyozalisha.

    w

    Mshindi huyo mwenye tuzo ya Ballon d'Or mara saba alifanya mazoezi na wachezaji wenzake kwa mara ya kwanza Jumanne baada ya kuhamia MLS baada ya kumalizika kwa mkataba wake huko Paris St-Germain.

    Messi alifunga mabao 32 katika michezo 75 katika kipindi cha miaka miwili akiwa na mabingwa hao wa Ufaransa baada ya kuondoka Barcelona, na akakataa ofa nono kutoka nchi nyingine kwenda kucheza Marekani.

  10. Serikali ya Afrika Kusini yaomba rasmi hati ya kukamatwa kwa Putin

    Putin

    Serikali ya Afrika Kusini imetuma maombi rasmi kwa mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin iwapo atawasili nchini humo.

    Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini, Democratic Alliance, kinasema kuwa haya ni makubaliano ya matakwa yake: chama hicho hapo awali kiliwasilisha ombi kwa mahakama kulazimisha serikali kutekeleza agizo la kukamatwa kwa Putin lililotolewa mwezi Machi na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huko The Hague.

    Afrika Kusini inawajibika rasmi kufuata matakwa ya ICC, na Putin alialikwa kwenye mkutano wa BRICS utakaofanyika Agosti mjini Johannesburg, lakini uongozi wa nchi hiyo haukuficha ukweli kwamba haikuwa na nia ya kumkamata rais wa Urusi.

    Hata hivyo, serikali ya Afrika Kusini haikupata njia yoyote ya kisheria ya kutotekeleza kibali hicho. Viongozi wa Afrika Kusini wamesema kwa uwazi katika siku za hivi karibuni kwamba walimwomba Putin asiende, na siku ya Jumatano aliamua kutokwenda, ingawa si lazima kutokana na hofu ya kukamatwa.

  11. Habari, karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja