Heche aishinikiza Kenya kumtafuta mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya
John Heche amesema haamini serikali ya Kenya ilihusika na kutoweka kwa Twaha Mwaipaya, lakini amehoji jinsi mtu anavyoweza kutekwa katika nchi nyingine bila msaada wa wenye mamlaka.
Muhtasari
- Mgonjwa wa kwanza wa Ebola Nigeria apelekwa Uswisi kwa matibabu
- Muuguzi auawa Congo, walioambukizwa Ebola wakikaribia 10,000
- Kuporomoka kwa jengo Eastleigh: DPP aamuru uchunguzi wa kina
- Mtanzania atwaa tuzo ya Jumuiya ya Madola
- Tahadhari ya Ebola: Uganda yaweka masharti mapya ya usafiri
- Heche aitaka Kenya kuhakikisha Twaha Mwaipaya anapatikana salama
- Junior Starlets yafuzu hatua ya 16 bora Kombe la Dunia U17
- Lula ashinda muhula wa nne wa urais Brazil
- Kiongozi wa upinzani Venezuela Maria Corina Machado arejea nchini baada ya miezi kadhaa uhamishoni
- KWS yamuua tembo aliyehusishwa na kifo cha mtu nchini Kenya
- Tetesi za soka Jumatatu: Howe yuko tayari kuzungumza na Man Utd kuhusu nafasi ya ukocha
- Netanyahu: Iran na washirika wake wanapanga kuvuruga uchaguzi Israel
- Kenya yatangaza huenda ikaumaliza ugonjwa wa Ebola ndani ya siku 42
- Mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya 'atekwa nyara ' Kenya - Amnesty yaonya
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid, Phillys Mwatee & Ambia Hirsi
Algeria kuingia Niger kijeshi kwa mara ya kwanza tangu 1973

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Algeria ilichangia Niger helikopta nne za kijeshi. (Picha ya maktaba) Algeria imeidhinisha kupeleka wanajeshi nchini Niger kwa mara ya kwanza tangu ilipotuma vikosi vyake nchini Misri wakati wa vita vya Kiarabu na Israel mwaka 1973.
Hatua hiyo imekuja baada ya ziara ya Waziri wa Ulinzi wa Niger mjini Algiers, huku Niger ikiendelea kutafuta msaada wa kukabiliana na makundi yenye silaha, yakiwemo yale yanayohusishwa na al-Qaeda na Islamic State.
Algeria pia ina maslahi muhimu ya kiuchumi nchini Niger, ikiwemo mradi wa bomba la gesi linalotarajiwa kusafirisha gesi kutoka Nigeria kupitia Niger hadi Algeria. Wanajeshi watakaotumwa wanatarajiwa kusaidia kulinda miundombinu ya nishati kaskazini mwa Niger karibu na mpaka wa Libya.
Uamuzi huo unakuja wakati Algeria na Niger zikijaribu kuimarisha tena uhusiano wao baada ya mzozo wa kidiplomasia mwaka 2025, ulioifanya Niger kumwita balozi wake kutoka Algiers.
Bunge la juu la Algeria lilipitisha pendekezo la kupeleka wanajeshi hao baada ya maseneta 148 kati ya 174 kupiga kura ya kuunga mkono hatua hiyo. Pendekezo hilo baadaye liliidhinishwa na bunge la chini.
Hata hivyo, mamlaka za Algeria hazijatangaza idadi ya wanajeshi watakaotumwa wala muda wa operesheni hiyo.
Iwapo utatekelezwa, utumaji huo utakuwa matumizi ya kwanza ya kifungu cha katiba ya mwaka 2020 kinachoruhusu jeshi la Algeria kushiriki operesheni nje ya mipaka ya nchi.
"Hatupeleki wanajeshi wetu Niger kwa ajili ya vita, bali kulinda miundombinu ya kiuchumi," alisema seneta wa Algeria, Belkacem Boulghiti.
Chris Brown aponea jela, ahukumiwa kifungo cha nje

Chanzo cha picha, PA
Maelezo ya picha, Nyota wa muziki wa R&B, Chris Brown Nyota wa muziki wa R&B, Chris Brown, amehukumiwa kifungo cha miezi minane gerezani, lakini kifungo hicho kimesitishwa na atatumikia kifungo cha nje kwa kipindi cha miezi 12.
Chris Brown alikiri kosa la kushiriki katika vurugu mwezi wa Julai mwaka huu.
Awali, alitarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka mazito zaidi, ambayo aliyakana na ambayo baadaye yaliondolewa.
Mashtaka hayo yalikuwa ni kushambulia, kujaribu kusababisha madhara makubwa ya mwili na kumiliki silaha inayoweza kutumika kutishia au kudhuru wengine.
Mwalimu wake wa sauti, rapa Omololu Akinlolu, mwenye umri wa miaka 40, pia alikiri kosa la kushiriki katika vurugu.
Kosa hilo linahusiana na shambulio dhidi ya mtayarishaji wa muziki Abe Diaw katika klabu ya usiku jijini London, tarehe 19 Februari mwaka wa 2023.
Upande wa utetezi ulimwelezea Chris Brown kama “baba anayejitolea na mwenye upendo kwa watoto wake wanne”, akisema kuwa ni mtu “anayewajibika na anayeshiriki kikamilifu katika maisha yao”.
Aidha, alielezewa kuwa ameishi “maisha mazuri na yanayoheshimu sheria” tangu alipohukumiwa kwa mara ya mwisho mwaka wa 2013.
Chris Brown ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa zaidi katika muziki wa R&B nchini Marekani.Amewahi kushinda tuzo mbili za Grammy, huku akipata uteuzi wake wa kwanza wa tuzo hizo mwaka wa 2007.

Chanzo cha picha, Reuters
Amekuwa na nyimbo kadhaa zilizoingia katika orodha ya nyimbo kumi zilizofanya vizuri zaidi nchini Uingereza, zikiwemo Turn Up the Music, Freaky Friday, With You na Don't Wake Me Up.
Mahakama ilikuwa imempa dhamana, hatua iliyomruhusu kuondoka nchini Uingereza.Katika vikao vya awali vya mahakama, aliamriwa kulipa kiasi cha pauni milioni tano za Uingereza (£5m) kama dhamana ya kifedha.
Masharti mengine ya dhamana hiyo yalimruhusu kufanya ziara ya kimataifa ya muziki, mradi tu angewasilisha pasipoti yake mara tu alipowasili nchini humo.Brown amekuwa katika ziara ya muziki pamoja na Usher.
Hata hivyo, tovuti ya Ticketmaster imeorodhesha baadhi ya maonyesho yao yaliyopangwa kufanyika mwezi Oktoba kuwa yameahirishwa.
Saudi Arabia yafuta safari za ndege Riyadh kufuatia mashambulizi ya Wahouthi

Chanzo cha picha, get
Mashambulizi ya waasi wa Houthi wa Yemen yamesababisha kufutwa kwa karibu asilimia 90 ya safari za ndege zilizokuwa zimepangwa kuondoka Riyadh, kwa mujibu wa takwimu za ufuatiliaji wa safari za ndege.
Takwimu za kampuni ya uchambuzi wa data za anga, Cirium, zinaonyesha kuwa kati ya Oktoba 8 na 25, safari 4,071 kati ya 4,736 zilizokuwa zimepangwa zilifutwa.
Waasi wa Houthi, wanaoungwa mkono na Iran, wameongeza mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya miundombinu muhimu ya Saudi Arabia katika miezi ya karibuni, ikiwemo vituo vya mafuta, bandari na viwanja vya ndege.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid mjini Riyadh, miongoni mwa viwanja vikubwa zaidi nchini Saudi Arabia, umekuwa ukilengwa mara kwa mara. Shambulio la Oktoba 10 lilisababisha vifo vya watu 13.
Jana, mamlaka za Saudi Arabia zilitangaza kufunguliwa tena kwa Uwanja wa Ndege wa Riyadh baada ya kufungwa kwa wiki mbili. Hata hivyo, ripoti zinaonyesha mashambulizi ya Houthi bado yanaendelea, hali iliyosababisha kufutwa kwa safari nyingi za ndege.
Kwa upande wao, waasi wa Houthi wameonya kwamba uwanja huo wa ndege bado ni "lengo la kijeshi" na hauko salama kwa shughuli za kawaida za usafiri wa anga.
Soma zaidi:
Mgonjwa wa kwanza wa Ebola Nigeria apelekwa Uswisi kwa matibabu

Chanzo cha picha, Fabrice COFFRINI / AFP via Getty Images
Waziri wa Afya wa Nigeria, Muhammad Ali Pate, amesema mgonjwa wa kwanza kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola nchini humo amehamishiwa Uswisi kwa ajili ya matibabu.
Pate amesema hali ya mgonjwa huyo imeimarika kwa kiasi kikubwa na kwamba ana fahamu na ana uwezo wa kuwasiliana. Hata hivyo, alionya kuwa matokeo mazuri ya vipimo vya maabara hayaondoi uwezekano wa mgonjwa huyo kuendelea kuwaambukiza wengine.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, waziri huyo alisema matokeo ya vipimo vya maabara yanaonyesha maendeleo mazuri katika afya ya mgonjwa huyo.
Mgonjwa huyo alisafirishwa pamoja na mumewe, ambaye hadi sasa hajaonyesha dalili zozote za maambukizi ya ugonjwa huo.
Waziri huyo aliwapongeza wahudumu wa afya waliomhudumia mgonjwa huyo pamoja na maafisa wa afya ya umma waliosimamia zoezi la uhamisho, akisema lilifanyika kwa kuzingatia taratibu kali za afya ya umma.
Aliongeza kuwa taarifa zaidi zitatolewa baada ya mgonjwa huyo na mumewe kuwasili salama nchini Uswisi.
Wiki iliyopita, Nigeria ilithibitisha kisa chake cha kwanza cha Ebola katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Mgonjwa huyo aligundulika kuwa na aina ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo.
Wakati huohuo, mamlaka za afya nchini humo zinaendelea kuwafuatilia watu waliowasiliana na mgonjwa huyo katika juhudi za kudhibiti na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Muuguzi auawa Congo, walioambukizwa Ebola wakikaribia 10,000

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Muuguzi mmoja ameuawa na mhudumu mwingine wa afya kujeruhiwa vibaya katika shambulio lililotokea kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), huku nchi hiyo ikikabiliwa na mlipuko wa virusi vya Ebola na idadi ya walioambukizwa ikikaribia 10,000.
Kwa mujibu wa Radio Okapi, chombo cha habari kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, shambulio hilo lilitokea siku ya Jumamosi katika mji wa Bafwasende, mkoani Tshopo.
Inadaiwa kuwa vijana wa eneo hilo waliwashambulia wahudumu hao wa afya, wakiwashutumu kwa kuchafua vyanzo vya maji na kusambaza virusi vya Ebola.
BBC imewasiliana na timu inayoratibu juhudi za kukabiliana na Ebola ili kupata maelezo kuhusu shambulio hilo, lakini bado haijapokea majibu.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limelaani shambulio hilo.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema wahudumu wa afya wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa usalama na kwa heshima.
Alisisitiza kuwa wahudumu wa afya wanapaswa kulindwa wakati wote. Aidha WHO ilitoa pole kwa familia na wafanyakazi wenza wa muuguzi aliyeuawa, na kumtakia mhudumu aliyejeruhiwa afueni ya haraka.
Shambulio hilo limetokea wakati mamlaka za afya zikitoa takwimu za hivi karibuni kuhusu mlipuko huo, zikionyesha kwamba maambukizi yanaendelea kuongezeka.Kwa mujibu wa kikosi kazi cha urais wa DRC kinachoshughulikia Ebola, kufikia tarehe 24 Oktoba, nchi hiyo ilikuwa imerekodi visa 9,964 vilivyothibitishwa na vifo 4,841.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa idadi ya jumla ya visa vilivyothibitishwa inakaribia kufikia 10,000 tangu mlipuko huo ulipotangazwa tarehe 15 mwezi wa Mei.
Katika kipindi kilichotajwa kwenye taarifa hiyo, mamlaka za afya ziliripoti visa vipya 88 vilivyothibitishwa, na vifo 38. Kati ya vifo hivyo, 26 vilitokea katika jamii, huku 12 vikitokea katika vituo vya matibabu ya Ebola.
Maambukizi mapya yaliripotiwa Ituri, Kivu Kaskazini na Haut-Uélé.
Ituri ndiyo mkoa ulioathiriwa zaidi, ukiwa na takribani asilimia 72 ya visa vyote vilivyorekodiwa tangu mlipuko huo uanze. Kivu Kaskazini, kwa upande mwingine, inaendelea kuripoti kiwango cha juu cha vifo miongoni mwa walioambukizwa.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, Dkt Wessam Mankoula wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) alisema kuwa wahudumu 300 wa afya walikuwa wameambukizwa Ebola tangu mlipuko huo uanze, huku 48 kati yao wakifariki kutokana na ugonjwa huo.
Mlipuko wa sasa unasababishwa na aina ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo.
Ugonjwa huo umeenea katika maeneo 66 ya afya katika mikoa minane.
Mamlaka zinaendelea na juhudi za kushirikisha jamii katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, kupambana na taarifa potofu na kuzuia maambukizi zaidi.
Maelez zaidi:
Kuporomoka kwa jengo Eastleigh: DPP aamuru uchunguzi wa kina

Chanzo cha picha, EPA
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameagiza uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu kuporomoka kwa jengo katika eneo la Eastleigh, Nairobi, ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na iwapo kulikuwa na ukiukaji wa sheria.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, DPP amesema uchunguzi huo utaangazia nafasi ya wahusika wote waliohusika katika mchakato wa ujenzi, ikiwemo maafisa wa umma, wawekezaji, wakandarasi na wataalamu wa ujenzi.
"Iwapo ushahidi utabaini kuwepo kwa makosa ya jinai, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaohusika bila kujali nafasi au hadhi zao," amesema DPP.
DPP amemwagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kwa hatua zaidi.
Pia ametoa pole kwa waathiriwa wa tukio hilo na kusisitiza umuhimu wa kuzingatiwa kwa viwango vya usalama na sheria za ujenzi ili kuepusha ajali kama hiyo siku zijazo.
Soma zaidi:
Mtanzania atwaa tuzo ya Jumuiya ya Madola

Chanzo cha picha, QECT
Mjasiriamali wa teknolojia kutoka Tanzania, Julius Mbungo, ametambuliwa miongoni mwa viongozi vijana 100 kwenye mataifa ya Jumuiya ya Madola katika tuzo za Queen Elizabeth II Commonwealth Trust (QECT) 100 Young Leaders Awards 2026.
Mbungo, ambaye ni mwanzilishi wa kampuni za Toolboksi na Spana za nchini Tanzania alihudhuria sherehe za tuzo hizo zilizotolewa Oktoba 13, akiwaki mmoja wa vijana wa kitanzania waliohudhuria kati ya wanne waliopewa heshima hiyo kutokana na kuleta mabadiliko katika jamii.
Wengine walioshinda tuzo hizo kutoka Tanzania ni Editha Mshiu, Dkt Noely Mapunda, na Suleiman Salum Suleiman.Katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo kwa Afrika Mashariki, Kenya pia ilikuwa na vijana wanne walioshinda tuzo hizo, Rwanda walipata washindi wawili na Uganda wakapata mshindi mmoja.
Tuzo hizo kwa vijana kati ya umri wa miaka 18 na 35, zilizotolewa na Queen Elizabeth II Commonwealth Trust zikiadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Malkia Elizabeth II na kuendeleza dhamira yake ya kusaidia vijana wanaoboresha maisha ya jamii zao.
Mbungo sambamba na washindi wengine kutoka mataifa mbalimbali pia walialikwa kuhudhuria mapokezi ya Mfalme na Malkia katika Kasri la St James’s jijini London, ambako alikutana na Mfalme Charles III na Malkia Camilla.
Mbungo anasema, kilichompa fursa ya kutambuliwa ni kutokana na jinsi alivyolenga makundi muhimu katika uchumi wa Tanzania ambapo kampuni zake zimekuwa zikisaidia mafundi na wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi.
“Nyuma ya heshima hiyo kuna kazi inayolenga mahitaji ya kawaida lakini muhimu kwa maisha ya mafundi,” anasema MbungoKupitia Kampuni yake ya Toolboksi, Mbungo anatumia teknolojia kuwaunganisha mafundi na kaya pamoja na biashara zinazohitaji huduma za ukarabati, matengenezo na ufungaji vifaa kwenye magari na vyombo vya moto.
Mbungo anasema jukwaa hilo la kiteknolojia linalenga kupanua fursa za kazi, kuendeleza ujuzi na kuwasaidia mafundi kujenga biashara zenye kipato endelevu.
Toolboksi iliyoanzishwa mwaka 2019, yenye mtandao wa mafundi zaidi ya 5,000 nchini Tanzania, inayowaunganisha mafundi wa sekta isiyo rasmi na fursa za kazi, kuanzia matengenezo madogo hadi miradi mikubwa, kwa lengo la kuongeza ajira na kipato.
Ubunifu wake mwingine, ni katika Kampuni yenye huduma inaitwa ‘Spana’ ambalo ni jukwaa la teknolojia linalotumia Akili Unde (AI) kuwasaidia mafundi magari kutambua hitilafu, kufanya matengenezo kwa ufanisi na kukuza biashara zao, huku likiwasaidia wamiliki wa magari kupata huduma bora na kusimamia matengenezo ya magari yao.
Tahadhari ya Ebola: Uganda yaweka masharti mapya ya usafiri

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Waziri wa Afya wa Uganda, Chris Baryomunsi, amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuzuia Ebola kuingia nchini na kudumisha hali ya Uganda kuwa huru dhidi ya ugonjwa huo. Uganda imeamuru karantini ya siku 21 kwa raia wake wanaorejea nchini kutoka DR Congo, kama sehemu ya hatua mpya za kujikinga dhidi ya Ebola.
Hatua hiyo inakuja wakati DRC ikiendelea kukabiliwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa huo, pamoja na kuibuka kwa wasiwasi baada ya watu wawili waliowahi kupita nchini Uganda kubainika baadaye kuwa na Ebola nchini Kenya na Nigeria.
Wizara ya Afya ya Uganda imesema wasafiri waliotembelea DRC hawataruhusiwa kwa sasa kutumia Uganda kama njia ya kupita kwenda nchi nyingine. Vilevile, raia wa Uganda wanaorejea kutoka DRC watalazimika kugharamia na kukamilisha karantini ya siku 21.
Mamlaka za afya pia zimeimarisha uchunguzi wa wasafiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, mipaka ya nchi kavu na vituo maalumu vya ukaguzi vilivyowekwa kwenye baadhi ya barabara.
Waziri wa Afya wa Uganda, Chris Baryomunsi, amesema ni wasafiri wa huduma muhimu pekee kutoka DRC watakaoruhusiwa kuingia nchini, lakini chini ya hatua kali za afya ya umma.
Alisema hatua hizo zinalenga kuzuia Ebola kuingia nchini na kuhakikisha Uganda inaendelea kuwa huru dhidi ya ugonjwa huo.
Wakati huohuo, Wizara ya Afya imesema watu 60 waliokuwa wakifuatiliwa baada ya kuhusishwa na mgonjwa wa Ebola nchini Kenya wameondolewa kwenye uangalizi baada ya kukamilisha kipindi cha ufuatiliaji bila kuonesha dalili za maambukizi.
“Hatua hizi zote zinalenga kuhakikisha Uganda inaendelea kuwa huru dhidi ya Ebola,” amesema Waziri wa Afya, Chris Baryomunsi.
Tangu wagonjwa waiwili wa Ebola kuthibitishwa nchini Kenya na Nigeria mwezi huu, Uganda imeendelea kusisitiza kuwa hakuna kisa chochote cha maambukizi kilichoripotiwa ndani ya mipaka yake.
Uganda ilithibitisha kuwa watu 20 wameabukizwa Ebola na vifo viwili kabla ya kutangazwa kuwa huru dhidi ya ugonjwa huo mwezi Agosti.
Hata hivyo, wasiwasi umeendelea kuibuka baada ya wasafiri wawili waliopitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe siku moja kubainika baadaye kuwa na Ebola nchini Kenya na Nigeria.
Maelezo zaidi:
Heche aitaka Kenya kuhakikisha Twaha Mwaipaya anapatikana salama

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, amesema wamejitahidi usiku kucha kuwasiliana na vyombo husika nchini Kenya ili kupata taarifa kuhusu aliko Twaha Mwaipaya.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Heche amesema haamini kuwa serikali ya Kenya ina sababu ya kumteka Mwaipaya, lakini amehoji jinsi watekaji wanavyoweza kuingia katika nchi nyingine na kumchukua mtu bila msaada wa watu wenye mamlaka.
“Ni vipi mtu anaweza kuingia katika nchi nyingine na kumchukua mtu bila msaada wa watu walioko ndani ya serikali hiyo?” amehoji Heche.
Amemwomba Rais wa Kenya, William Ruto, na serikali yake kusaidia kuhakikisha Mwaipaya anapatikana akiwa hai na salama.
Heche ameonya kuwa tukio hilo, iwapo litathibitishwa, linaweza kulitia doa jina la Kenya kama taifa la kidemokrasia, akisema mtu aliyekimbilia nchini humo kutafuta hifadhi hapaswi kutekwa akiwa ndani ya mipaka yake.
Aidha, amedai kuwa makundi machache nchini Tanzania yamekuwa yakitumia vitendo vya mauaji, utekaji na vitisho kuwanyamazisha wanaokosoa uovu. Amewataka Watanzania kutokubali hali hiyo kuendelea na kusisitiza kuwa wanamtaka Mwaipaya apatikane akiwa salama.
Kwa upande wake, serikali ya Tanzania imekuwa ikikanusha madai ya kuhusika na vitendo visivyo halali dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi au tamko lolote lililotolewa na mamlaka za usalama nchini Kenya kuhusiana na tukio hilo la kutekwa kwa Mwaipaya.
BBC Swahili inafuatilia na serikali ya Kenya kujua msimamo wao.
Junior Starlets yafuzu hatua ya 16 bora Kombe la Dunia U17

Chanzo cha picha, FKF
Timu ya taifa ya wanawake ya Kenya walio chini ya umri wa miaka 17, Junior Starlets, imeandika historia kwa kufuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia U17 nchini Morocco, baada ya kuicharaza Samoa mabao 4-0.
Junior Starlets ilipata ushindi huo katika mechi iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Mohammed VI mjini Rabat, na kufuzu kama mojawapo ya timu nne zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi, zilizopata nafasi ya kusonga mbele.
Kenya ilikuwa katika hatari ya kuondolewa baada ya kupoteza mechi zake mbili za kwanza. Ilianza kampeni kwa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya China, kabla ya kufungwa mabao 6-1 na Marekani.
Hivyo, katika mechi dhidi ya Samoa, Starlets ilihitaji ushindi wa mabao mengi ili kuongeza nafasi yake ya kufuzu.
Mwanakombo Bakari aliipa Kenya bao la kwanza dakika ya tano, kabla ya Brenda Awuor kuongeza la pili dakika ya 44. Kenya ilienda mapumzikoni ikiwa mbele kwa mabao 2-0, lakini bado ilihitaji mabao zaidi ili kuimarisha nafasi yake ya kufuzu.
Kipindi cha pili, Junior Starlets iliendeleza mashambulizi yake. Gaudencia Maloba alifunga bao la tatu dakika ya 61, kabla ya Mwanakombo Bakari kukamilisha mabao manne dakika mbili baadaye na kuuhakikishia ushindi huo muhimu.
Mwanakombo Bakari, anayeichezea akademia ya Spire nchini Marekani, alituzwa mchezaji bora wa mechi kufuatia kiwango chake cha kuvutia.
Katika hatua ya 16 bora, Kenya itakutana na Japan siku ya Alhamisi, tarehe 29, kuanzia saa tatu usiku kwa saa za Afrika Mashariki, katika Uwanja wa Mohammed VI mjini Rabat.

Chanzo cha picha, FKF
Maelezo ya picha, Mwanakombo Bakari, anayeichezea akademia ya Spire nchini Marekani, alituzwa mchezaji bora wa mechi kufuatia kiwango chake cha kuvutia. Mnamo mwaka 2024, nchini Jamhuri ya Dominika, Junior Starlets iliandika historia kwa kuwa timu ya kwanza ya kandanda ya Kenya kufuzu kwa Kombe la Dunia. Ingawa ilishinda mechi moja pekee, ikiilaza Mexico mabao 2-1 baada ya kupoteza mechi zake mbili za awali, timu hiyo haikufanikiwa kuvuka hatua ya makundi.
Kwa hiyo, ushindi wa jana ni hatua muhimu katika maendeleo ya kandanda nchini Kenya. Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya, Hussein Mohamed, amesisitiza umuhimu wa kukuza vipaji vya soka kuanzia ngazi ya chini.
Lula ashinda muhula wa nne wa urais Brazil

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, amechaguliwa kuhudumu kwa muhula wa nne baada ya kumshinda seneta Flávio Bolsonaro katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais nchini humo.
Baada ya asilimia 98.87 ya masanduku ya kura kuhesabiwa, Mahakama ya Uchaguzi ya Brazil (TSE) ilimtangaza Lula kuwa mshindi kwa mujibu wa hesabu za kura zilizokuwa zimepatikana. Lula alipata asilimia 51.79 ya kura, dhidi ya asilimia 48.21 alizopata Bolsonaro.
Tofauti hiyo ya kura ilikuwa kubwa kuliko ushindi wa Lula dhidi ya baba yake Flávio, rais wa zamani Jair Bolsonaro, katika uchaguzi wa mwaka 2022.
Matokeo hayo yalikuwa ya kushangaza, yakiwa mara ya kwanza tangu Brazil irejee katika mfumo wa demokrasia kwa mgombea aliyeshindwa katika duru ya kwanza kugeuza matokeo na hatimaye kushinda urais.
Katika hotuba yake ya kwanza baadaya kutangazwa mshindi Lula amesema “Demokrasia iishi milele,”.
Aidha, ameongezea kuwa, “Muhula huu wangu wa nne utakuwa bora kuliko muhula wowote wa rais katika historia ya nchi hii.”
“Utakuwa muhula ambao nitawasikiliza zaidi wananchi wa Brazil.”
Ushindi huo ulifuatia kampeni kubwa iliyofanywa na wafuasi wa Lula kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na maandamano yaliyovutia mamia ya maelfu ya watu katika miji mikuu ya nchi hiyo, ikiwemo Rio de Janeiro na São Paulo.
Siku ya uchaguzi pia ilishuhudia idadi kubwa ya wapiga kura wakijitokeza. Kiwango cha kutoshiriki uchaguzi kilipungua kwa kiasi kikubwa zaidi kati ya duru ya kwanza na ya pili kuliko katika uchaguzi wowote wa urais nchini humo tangu mwaka 1989.
Hata hivyo, uchaguzi huo haukukosa utata. Kampeni ya Lula ilidai kuwa baadhi ya wapiga kura walizuiwa kushiriki baada ya uhaba wa mabasi kufanya iwe vigumu kwao kufika katika vituo vya kupigia kura katika miji kadhaa, ikiwemo São Paulo na Salvador, kaskazini-mashariki mwa Brazil.
Kampeni ya Flávio Bolsonaro nayo iliomba muda wa kupiga kura uongezwe kutokana na hali mbaya ya hewa kusini mwa Brazil. Hatimaye, Mahakama ya Juu iliongeza muda wa upigaji kura kwa saa mbili.
Jair Bolsonaro kwa sasa yuko kizuizini baada ya kutiwa hatiani mwezi Septemba 2025 kwa kujaribu kufanya mapinduzi ya serikali kufuatia kushindwa na Lula katika uchaguzi wa mwaka 2022.
Kwa ushindi huo, Lula anakuwa rais wa kwanza katika historia ya Brazil kuchaguliwa kuhudumu kwa muhula wa nne. Ataendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2030.
Flávio Bolsonaro alikuwa mgombea ambaye Rais wa Marekani Donald Trump alimpigia upatu kuwa rais wa Brazil.
Soma pia:
Kiongozi wa upinzani Venezuela Maria Corina Machado arejea nchini baada ya miezi kadhaa uhamishoni

Chanzo cha picha, Reuters
Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, Maria Corina Machado, amerejea nchini humo baada ya kukaa nje ya nchi kwa zaidi ya miezi 10, wakati hali ya kisiasa ikiendelea kuwa na mvutano.
“Nimerudi hapa, niko pamoja nanyi,” aliandika Machado kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili.
Edmundo Gonzalez Urrutia, aliyewahi kugombea urais nchini Venezuela na ambaye ni mshirika wa Machado, pia alithibitisha taarifa hizo dakika chache baadaye.
“Nina furaha kuwajulisha kwamba kiongozi wetu, mpendwa wangu Maria Corina, yuko nchini Venezuela,” aliandika.
Aliongeza kuwa hivi karibuni atajiunga na Machado nchini humo ili kuongoza juhudi za kuifikisha nchi hiyo kwenye “uhuru”.
Mmoja wa washauri wa Machado alisema mwezi Septemba kuwa alikuwa amejaribu kurejea Venezuela mara saba katika wiki chache zilizotangulia, lakini alizuiwa kuingia nchini kila mara.
Bado haijafahamika Machado anapanga kufanya nini baada ya kurejea. Hata hivyo, amewahi kusema kuwa atawania tena urais iwapo uchaguzi utafanyika.
Katika taarifa iliyotolewa kwa Margaret Brennan wa CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, msemaji wa Machado alielezea kurejea kwake kuwa “hatua muhimu kuelekea mpito wa kidemokrasia na kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki na unaoweza kuthibitishwa katika siku za usoni”.
Soma Pia:
KWS yamuua tembo aliyehusishwa na kifo cha mtu nchini Kenya

Chanzo cha picha, KWS
Maafisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya (KWS) wamempiga risasi na kumuua tembo anayehusishwa na kifo cha mtu mmoja katika eneo la Kamaindi, wadi ya Tharaka, kaunti ya Kitui.
Tembo huyo aliuawa saa chache baada ya tukio hilo la mauaji, kufuatia malalamiko ya wakazi waliokuwa na wasiwasi kuhusu kuendelea kwake kuzurura katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, tembo huyo alikuwa akizunguka eneo hilo kwa wiki kadhaa na kujificha katika shamba la mkazi mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Mkulima.
Kifo hicho kilisababisha maafisa wa KWS kuingilia kati, na hatimaye kumuua tembo huyo huku hofu kuhusu usalama wa wakazi ikiendelea kuongezeka.
Mzoga wa tembo huyo unatarajiwa kuchomwa moto kama sehemu ya utaratibu wa kuutupa.
Tukio hilo limezua tena wasiwasi kuhusu migogoro kati ya binadamu na wanyamapori katika eneo hilo, ambako kukutana kwa wakazi na tembo kunahatarisha maisha na shughuli zao za kujipatia riziki.
Tetesi za soka Jumatatu: Howe yuko tayari kuzungumza na Man Utd kuhusu nafasi ya ukocha

Chanzo cha picha, Getty Images
Aliyekuwa kocha wa Newcastle United,Eddie Howe, ambaye kwa sasa hana timu ya kufundisha, anavutiwa na uwezekano wa kuzungumza na Manchester United iwapo klabu hiyo ya Old Trafford itaamua kumtimua Michael Carrick, ambaye anakabiliwa na shinikizo kutokana na Man Utd kuandikisha matokeo duni. (Sky Sports)
Manchester United inalenga kumsajili Jarrad Branthwaite, beki wa Everton na timu ya taifa ya England mwenye umri wa miaka 24, katika juhudi za kufanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya ulinzi.(Football Insider)
Sean Dyche, aliyewahi kuzinoa Watford, Burnley, Everton na Nottingham Forest, anatajwa kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi ya kuinoa Crystal Palace iwapo klabu hiyo itamfuta kazi kocha wake Pierre Sage. (Telegraph - subscription required)
Thomas Frank, aliyewahi kuinoa Brentford, Vitor Pereira, aliyewahi kuifundisha Wolverhampton Wanderers, na Robbie Keane, aliyewahi kuinoa Ferencváros, pia wanatajwa kuwa wagombea wa nafasi hiyo. (Talksport)
Kiungo wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Sweden, Lucas Bergvall, mwenye umri wa miaka 20, anafuatiliwa na Napoli na Barcelona. . (Tuttomercato via Teamtalk)
Manchester United haitafuta usajili wa mshambuliaji wake wa akademia, JJ Gabriel, mwenye umri wa miaka 16. Hatua hiyo ina maana kwamba mchezaji huyo hataweza kuondoka klabuni hapo hadi Januari, huku Barcelona na Paris Saint-Germain zikijaribu kufikia makubaliano ya kumsajili. (Football Insider)
Arsenal, Liverpool na Manchester United zinafuatilia maendeleo ya Lennart Karl, kiungo wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 18. (Teamtalk)
Beki wa Brazil, Dodo, anatarajiwa kuondoka Fiorentina mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu. AC Milan, Juventus na Barcelona zinahusishwa na uwezekano wa kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27. (Football Italia)
Brighton na RB Leipzig ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia Adin Licina, kiungo wa Juventus mwenye umri wa miaka 19 anayeichezea Cremonese kwa mkopo. Licina ni mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Ujerumani chini ya umri wa miaka 19. (Gianluca di Marzo)
Soma pia:
Netanyahu: Iran na washirika wake wanapanga kuvuruga uchaguzi Israel

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema Iran na washirika wake huenda wakajaribu kufanya mashambulizi ili kuvuruga uchaguzi nchini Israel, unaotarajiwa kufanyika Jumanne.
Katika video iliyotolewa na ofisi yake Jumapili, Netanyahu amesema Israel ina taarifa za kiintelijensia zinazoashiria uwezekano wa maadui wake kujaribu kuathiri uchaguzi huo kupitia mashambulizi.
Amesema: “Tuna taarifa za kiintelijensia kwamba maadui wetu, yaani Iran na washirika wake, wanaweza kutujaribu kwa kufanya mashambulizi yanayolenga kuvuruga uchaguzi.”
Netanyahu pia ameeleza kuwa jeshi la Israel limejiandaa kukabiliana na hali hiyo, kwa hatua za kujilinda na kushambulia.
Ameonya kuwa iwapo mashambulizi hayo yatatokea, Israel itajibu kwa nguvu zaidi kuliko washambuliaji wanavyoweza kutarajia.
Kauli hizo zinatolewa huku mvutano kati ya Israel na Iran ukiendelea kuongezeka, wakati uchaguzi wa Israel ukiratibiwa kufanyika kesho Jumanne.
Kenya yatangaza huenda ikaumaliza ugonjwa wa Ebola ndani ya siku 42

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Afya nchini Kenya, Aden Duale, amesema huenda Kenya ikatokomeza Ebola ndani ya siku 42, iwapo hakutakuwa na visa vipya vya maambukizi katika kipindi hicho.
“Tumefanikiwa kuudhibiti ugonjwa huo, na nina uhakika kuwa Kenya itatangazwa kuwa huru dhidi ya Ebola tutakapofikisha siku 42. Huu si muda uliowekwa na Kenya, bali ni mwongozo wa kimataifa uliowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).”
Kuhusu vikwazo vya safari, biashara na utalii nchini Kenya, Waziri Duale amesema, “Hakuna vikwazo vya safari, biashara wala utalii nchini Kenya. Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Afya zimejulishwa kupitia WHO. Msimamo wa WHO ni kwamba hakuna nchi inayopaswa kufunga mipaka yake au kuweka vikwazo hivyo''.
AIdha Kenya imeeleza kuwa Balozi wa Uingereza aliyekuwa amezuru kaunti ya Mombasa aliwaambia kuwa Kenya inafanya kazi nzuri sana, na kwamba hakutakuwa na vikwazo vya safari.
Kisa cha kwanza cha Ebola nchini Kenya kiligunduliwa tarehe 3 Oktoba 2026, baada ya mgonjwa kuingia nchini akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Duale amesema serikali inaendelea kuwapima watu wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa na kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Katika kipindi cha saa 48 zilizopita, watu 551 walipimwa virusi vya Ebola na matokeo yao yote yakawa hasi.
Waziri huyo amesema baadhi ya watu waliowekwa karantini wanaweza kuruhusiwa kuondoka iwapo vipimo vyao vitaonyesha kuwa hawajaambukizwa. Watu 21 wanatarajiwa kufanyiwa vipimo zaidi.
Hata hivyo, Kenya imerekodi vifo viwili vilivyohusishwa na mlipuko huo. Waathiriwa hao ni pamoja na mgonjwa wa kwanza, mwenye umri wa miaka 45, aliyeingia nchini akiwa ameambukizwa, na mwanamke mwenye umri wa miaka 65 aliyefariki tarehe 23 Oktoba.
Wizara ya Afya imesema visa vyote vilivyothibitishwa hadi sasa vinahusiana na kundi moja la watu ambao walikuwa na mawasiliano yanayojulikana. Hadi sasa, hakuna ushahidi wa maambukizi yaliyoenea katika jamii kwa ujumla.
Serikali imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, kudumisha usafi wa mikono na kufuata maelekezo ya maafisa wa afya.

Mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya 'atekwa nyara ' Kenya - Amnesty yaonya

Chanzo cha picha, MITANDAONI
Mwanaharakati wa upinzani na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Tanzania, Twaha Mwaipaya, anaripotiwa kutekwa katika eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos, viungani mwa jiji la Nairobi, kwa mujibu wa Amnesty International Kenya.
Shirika hilo limesema Mwaipaya alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake mwendo wa saa nane mchana Jumapili alipodaiwa kuzuiwa na watu waliokuwa katika magari matatu, likiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop.
Amnesty imezitaka mamlaka za Kenya kuchukua hatua za haraka kubaini alipo Mwaipaya na kuhakikisha usalama wake.
Pia limewaomba wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kujua alipo kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Vile vile, haijulikani iwapo tukio hilo linahusiana na shughuli za kisiasa za Mwaipaya au kama kulikuwa na sababu nyingine.
Kwa mujibu wa mwanaharakati mashuhuri wa Tanzania, Maria Sarungi Tsehai, akaunti za mitandao za Mwaipaya zimesimamishwa ili kulinda usalama wa taarifa zake.
Mwaipaya ni kiongozi wa vijana katika chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Amekuwa akitetea mageuzi ya katiba, uwajibikaji na ulinzi wa haki za binadamu.
Pia amekuwa akiikosoa serikali ya Tanzania kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Taarifa zinaonyesha kuwa amewahi kukabiliwa na changamoto za kisheria na kisiasa nchini Tanzania. Mwaka 2022, CHADEMA ilitafuta msaada wa mahakama kufuatia wasiwasi kuhusu kuzuiliwa kwake na mahali alipokuwa baada ya kukamatwa.
Kutoweka kwake kunakodaiwa kumezua wasiwasi miongoni mwa mashirika ya haki za binadamu na wanaharakati wa kikanda kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali wanaofanya shughuli zao katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.
Mashirika ya haki za binadamu, yakiwemo Amnesty International Kenya na Defenders Coalition, yametaka hatua za haraka zichukuliwe kumtafuta.
Kisa hicho pia kimeibua upya wasiwasi kuhusu kile ambacho mashirika hayo yanakitaja kuwa ukandamizaji unaovuka mipaka ya nchi dhidi ya wapinzani wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu.
Kwa upande wake, serikali ya Tanzania imekuwa ikikanusha madai ya kuhusika na vitendo visivyo halali dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi au tamko lolote lililotolewa na mamlaka za usalama nchini Kenya kuhusiana na tukio hilo la kutekwa kwa Mwaipaya.
BBC Swahili inafuatilia na serikali ya Kenya kujua msimamo wao.
Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 26/10/2026.



















