Abiria wa meli ya kifahari ya kitalii wamekwama nchini Kambodia kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta

Chanzo cha picha, Villa Vie Residences
Abiria wa meli ya kifahari iliyokuwa ikizunguka dunia wamekwama nchini Cambodia baada ya kampuni inayoendesha meli hiyo kusitisha safari kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta.
Kampuni ya Marekani inayomiliki meli ya Villa Vie Odyssey imesema inashirikiana na abiria kupanga namna ya kushuka melini na kupata makazi ya muda.
Haijafahamika idadi kamili ya abiria waliokuwa melini, lakini meli hiyo yenye urefu wa karibu mita 200 ina uwezo wa kubeba hadi abiria 650. Ilianza safari yake kutoka Belfast, Ireland Kaskazini, mwezi Oktoba 2024, ikiwa na mpango wa kuzunguka dunia.
Bei ya mafuta imepanda kwa kiasi kikubwa tangu kuanza kwa vita vya Iran mapema mwaka huu. Kampuni hiyo imesema gharama ya mafuta kwa kila chumba cha abiria kwa mwezi katika baadhi ya maeneo ya Asia imeongezeka kutoka dola 1,800 hadi dola 8,000.
Kampuni hiyo imesema ilichukua hatua za kupunguza matumizi ya mafuta, zikiwemo kupunguza kasi ya meli na kuongeza muda wa kusimama bandarini. Hata hivyo, hatua hizo hazikutosha kukabiliana na ongezeko kubwa la gharama.
Kampuni hiyo imesema haiwezekani kuwabebesha abiria gharama zote za ongezeko hilo.
Imeongeza kuwa itatumia siku 60 zijazo kurekebisha shughuli zake na kutafuta mtaji zaidi, ingawa hakuna uhakika wa matokeo ya mchakato huo.
Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, safari hiyo ilipangwa kudumu miaka mitatu na nusu na kutembelea karibu nchi 150.
Meli hiyo ilikuwa imezunguka dunia kwa zaidi ya siku 750 ilipotangaza kusitisha safari yake Jumanne, na kuwaacha abiria nchini Cambodia.
Shirika la habari la Bloomberg, likimnukuu mwanzilishi wa kampuni hiyo, limeripoti kuwa takribani abiria 200 walikuwa melini walipoambiwa washuke nchini Cambodia.
Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, meli ya Villa Vie Odyssey ina baa na mikahawa kadhaa, eneo la kuogelea na uwanja wa mchezo wa pickleball.























