Chombo kinachotarajiwa kugongana na mwezi chatambuliwa

Wanaastronomia wanasema kwamba sehemu ya roketi iliotarajiwa kugongana na mwezi , mnamo mwezi Machi haikutoka kwa kampuni ya uchunguzi wa anga ya Elon Musk kama ilivyodhaniwa.

Moja kwa moja

  1. Mpaka hapa tumefika mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja ya kurasa wetu wa BBC Swahili, Shukrani!

  2. Hatma ya Mbowe na wenzake kujulikana Ijumaa

    th

    Mwenyekiti wa chama cha Chadema, nchini Tanzania Freeman Mbowe na wenzake watatu watajua iwapo wana kesi ya kujibu au la katika kesi ya ugaidi inayowakabili Ijumaa Februari 18, 2022 wakati Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi itakapotoa uamuzi wake .

    Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo amesema hayo leo Jumanne Februari 15, 2022 baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahaka kuwa wamefunga kesi hiyo kwa shahidi wa 13 kuhitimisha ushahidi wake.

    Shahidi huyo wa 13 wa upande wa mashtaka ambaye ni Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila amemaliza kutoa ushahidi baada ya kuhojiwa maswali ya dodoso na upande wa utetezi.

    Baada ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, Wakili wa Serikali Robert Kidando aliiambia Mahakama kuwa wamefunga ushahidi na kuiomba mahakama ione kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.

    “Baada ya ushahidi wa shahidi huyu wa kumi na tatu tunaialika Mahakama yako chini ya kifungu 41 (1) cha sheria ya Uhujumu Uchumi ione washtakiwa wote wanne wana kesi ya kujibu hivyo hatua nyingine kwaajili ya kujitetea ifuate kwa upande wetu tunafunga kesi hii” amesema Wakili Kidando

    Hata hivyo, baada ya kutoa ombe hilo, upande wa utetezi kupitia Wakili Peter Kibatala umeomba kupewa nafasi ya kufanya mawasiliano ya mdomo pamoja na kupewa mwenendoi wa kesi.

  3. Urusi haitaki vita asema Putin

    th

    Rais Vladmir Putin amesema nchi yake haitaki vita .Ameulizwa ikiwa anaweza kufutilia mbali uwezekano wa vita barani Ulaya na

    Akarejelea maoni ya awali ya Kansela wa Ujerumani Scholz kwamba kizazi chake hakiwezi kufikiria vita barani Ulaya - lakini anasema kuwa bara hilo limeshuhudia vita huko Yugoslavia katika miaka ya 1990, ambayo anadai ilianzishwa na Nato.

    Putin anasema Urusi haitaki vita na hivyo ametoa mapendekezo ya kuanza mchakato wa mazungumzo - lakini anasema hakujawa na majibu ya kujenga kwa mapendekezo ya Urusi.

    Hata hivyo, anaongeza kuwa bado kuna masuala yaliyotolewa na Nato na Marekani ambayo yanaweza kujadiliwa.

    Rais Putin ameishutumu Ukraine kwa kufanya vitendo vya mauaji ya halaiki dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na waasi wanaoungwa mkono na Moscow katika eneo la Donbas mashariki.

    "Kwa maoni yetu kinachotokea sasa Donbas ni mauaji ya halaiki," ameuambia mkutano wa waandishi wa habari.

    Rais Putin anasema mahitaji ya kimsingi hayajafikiwa na Nato na kwamba ina wajibu wa kutoimarisha usalama wake kwa gharama ya nchi nyingine.

    Hata hivyo, anasema yuko tayari kuzungumzia masuala ya usalama na makombora ya Ulaya.

  4. Aliyembaka ajuza mwenye umri wa miaka 87 amekamatwa

    m

    Mwanaume mwenye umri wa miaka 30 amekamatwa kwa kosa la kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 87 huko Delhi, mji mkuu wa India.

    Polisi walisema mwanaume huyo alikuwa mfanyakazi wa kuzoa taka aliyekuwa akiishi karibu na nyumba ya mwanamke huyo eneo la Tilak Nagar.

    Polisi waliongeza kuwa mwanamke huyo aliyelazwa hospitalini kwa uzee na ugonjwa, alikuwa peke yake nyumbani Jumapili jioni alipovamiwa na kuibiwa.

    Ndugu wa mwanamke huyo wanasema ni kosa la polisi, ambalo lilisababisha malalamiko ya wizi zaidi ya ubakaji - lakini polisi wanasema vinginevyo.

    Polisi wanasema familia ya mwanamke huyo iliripoti tu wizi siku ya Jumapili - baadaye kesi ya ubakaji siku ya Jumatatu.

    Mmoja wa ndugu wa mwanamke huyo aliliambia gazeti la Indian Express kwamba polisi walimwambia mwanamke huyo na binti yake wasifuatilie malalamiko ya ubakaji kwa sababu yatawaweka katika mazingira magumu zaidi." mtu huyo alisema.

    Mwanamke huyo alikuwa akikaa nyumbani na binti yake, ambaye hakuwa nyumbani wakati wa tukio.

    Aliporudi, alimkuta mama yake akiwa amejeruhiwa.

    Tume ya Kitaifa ya Wanawake ilisema Jumatatu iliyopita kwamba iliandika barua kwa polisi wa Delhi kuomba hatua zichukuliwe dhidi ya wale wanaoshutumiwa kwa kutochukua hatua za haraka.

    Mnamo 2020, ubakaji wa mwanamke mwenye umri wa miaka 86 huko Delhi- ulishtua watu wa nchi hiyo. Ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia umekuwa ukiangaliwa nchini India tangu mwaka wa 2012 walipobaka na kuuawa na genge la msichana kwenye basi huko Delhi.

    Ubakaji na unyanyasaji umekuwa ukiongezeka nchini India tangu 2012, wakati msichana mdogo alibakwa na kuuawa kwenye basi huko Delhi.

  5. Walimu wa Kenya kupata hadi miezi minne ya likizo ya wazazi

    th

    Walimu wa Kenya sasa watakuwa na haki ya hadi miezi minne ya likizo ya wazazi yenye malipo kufuatia makubaliano na mwajiri wao .

    Walimu wa kike watapata likizo ya siku 120 ya uzazi huku wenzao wa kiume wakistahiki wiki tatu za likizo ya uzazi.

    Hili ni ongezeko kutoka miezi mitatu na siku 14 ambazo wafanyikazi wa kike na wa kiume wa Kenya wanastahili kupewa mtawalia.

    Wazazi wanaoasili mtoto watapewa likizo ya siku 45 chini ya makubaliano hayo.

    Walimu wanajumuisha idadi kubwa ya wafanyikazi wa umma nchini Kenya, na zaidi ya 300,000 kati yao wameajiriwa na Tume ya Kuwaajiri Walimu(TSC)

    Walimu hao watahitajika kuwasilisha maombi yao ya likizo mtandaoni na mapema ili kuruhusu kupanga jinsi nafasi hizo zitakavyojazwa.

  6. Polisi nchini Uganda wawakamata washukiwa saba wa ugaidi

    th

    Polisi wa Uganda wamewatia mbaroni watu saba kwa madai kuwa makundi mawili ya kigaidi yenye uhusiano na uvamizi katika wilaya ya kati ya Lukaya na Butambala.

    Msemaji wa polisi Fred Enanga amesema operesheni za kijasusi zimeonyesha kuwa washukiwa hao walikuwa wakijiandaa kwa mashambulizi na imam mtoro Suleman Nsubuga.

    Bw Nsubuga alitoroka uvamizi katika maficho yake katika Wilaya ya Wakiso ya kati mwaka jana.

    Bw Enanga alisema polisi wanafanya kazi ya kuvunja seli zozote za kujipanga upya kufuatia msako mkali baada ya mashambulizi ya wanamgambo Oktoba na Novemba 2021.

    "Hizi ni seli zinazofanya kazi ambazo zinajiendesha, zinazotembea .Hata hivyo, tunataka kuwahakikishia wananchi tutahakikisha tunaziondoa na kuzuia kuundwa kwa seli mpya," alisema.

    Serikali ya Uganda mwaka jana ililaumu kundi linalohusishwa na Islamic State-Allied Democratic Forces (ADF) kwa mfululizo wa mashambulizi katika mji mkuu, Kampala, ambayo yalisababisha vifo vya watu wengi na makumi ya wengine kujeruhiwa.

    Mashambulizi hayo yalipelekea operesheni ya pamoja na vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo dhidi ya waasi hao ambayo ilianza kwa mashambulizi ya anga tarehe 30 Novemba.

    Awamu ya pili ya operesheni hiyo kwa sasa inaendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati hakuna shambulio lililoripotiwa nchini Uganda katika siku za hivi karibuni.

  7. Kylian Mbappe: Je mshambuliaji huyo wa PSG anaelekea kujiunga na Real Madrid kipindi hiki cha joto?

    th

    Wakati Kylian Mbappe akijiandaa na Paris St-Germain Jumanne dhidi ya Real Madrid atakabiliana na klabu ambayo huenda atajiunga nayo mkataba wake utakapokamilika msimu huu wa joto.

    Ingawa hakuna kilichothibitishwa, itakuwa mshtuko mkubwa ikiwa mshambuliaji huyo wa Ufaransa hataishia kwenye shati jeupe ambalo amekuwa na ndoto ya kuvaa tangu akiwa mtoto.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 hatasema lolote kwa sasa - angalau hadi mechi ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa ya PSG na viongozi wa ligi ya Uhispania itakapokamilika.

    Kufikia wakati huo, atakuwa na matumaini ya kuwa amewapa Real mtazamo wa moja kwa moja wa kile ambacho watakuwa wakipata.

    Mbappe, mvulana kutoka Bondy katika viunga vya maili saba kutoka katikati mwa jiji la Paris, alitaka kuchezea PSG, lakini pia ni kweli kwamba labda alikuwa akienda Madrid, ingawa imechukua muda kufikia hatua hii. .

    Alitakiwa na vilabu vikubwa vya Uropa mnamo 2017 baada ya kutamba akiwa na Monaco. Alichagua PSG - mwanzoni alijiunga kwa mkopo katika mkataba ambao hatimaye ungegharimu mabingwa hao wa Ufaransa £165.7m - kwa sababu ilikuwa klabu ya jiji lake, ambayo iliungwa mkono na marafiki zake wengi, klabu muhimu zaidi nchini Ufaransa wakati huo.

    Lakini haingekuwa kikomo kwa taaluma yake. Mbappe alivutiwa na Cristiano Ronaldo na alikua akitazama mfano wake aking’aa wakati akiwa na Real. Inasaidia kwamba Mbappe ni mchezaji adimu ambaye, kama Mreno huyo, anaweza kukabiliana na shinikizo kubwa linalotokana na kuwa jina la nyota kwa moja ya klabu vikubwa duniani.

    Akiwa na umri wa miaka 19, akiwa amefunga tu katika fainali wakati Ufaransa ikishinda Kombe la Dunia la 2018, Mbappe alifanya mahojiano ambapo mawazo yake yalidhihirika. "Huu ni mwanzo tu," alisema. "Niko hapa kuweka historia."

    Iwapo ataendelea na kiwango chake cha sasa ni vigumu kuona jinsi ambavyo hataweza kuleta matokeo makubwa kama mchezaji mkuu Bernabeu.

  8. Waandamanaji wawili wameuawa kwa kupigwa risasi nchini Sudan

    Th

    Waandamanaji wawili wa Sudan waliuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya usalama siku ya Jumatatu, muungano wa madaktari nchini Sudan unasema.

    Hii inafikisha idadi ya watu waliouawa tangu mapinduzi ya Oktoba hadi takribani 80.

    Maandamano ya hivi punde ya kuunga mkono demokrasia siku ya Jumatatu yalifanyika katika miji kadhaa kote nchini kukataa utawala wa kijeshi na kutaka kuachiliwa kwa wanasiasa waliokamatwa hivi karibuni.

    Tangu wiki iliyopita wanasiasa watatu ambao waliwahi kuwa katika baraza kuu tawala wamezuiliwa.

    Wote walikuwa sehemu ya kikosi kazi kilichoteuliwa kuvunja mitandao ya kiuchumi na kisiasa iliyoanzishwa wakati wa utawala wa rais wa zamani Omar al-Bashir wa takriban miongo mitatu.

  9. Mvutano wa Ukraine na Urusi: Urusi yawaondoa baadhi ya wanajeshi kutoka mpakani

    Urusi yaondoa baadhi ya majeshi yake
    Maelezo ya picha, Urusi yaondoa baadhi ya majeshi yake

    Urusi inasema inawaondoa baadhi ya wanajeshi wake kutoka karibu na Ukraine baada ya kuwa kujikusanya kwao kumesababisha hofu ya uvamizi.

    Wizara ya ulinzi ilisema kuwa mazoezi makubwa yanaendelea lakini baadhi ya wanajeshi walikuwa wanarejea katika kambi zao.

    Haijasema ni wanajeshi wangapi wanaondoka na bado haijabainika iwapo hilo litapunguza wasiwasi uliopo.

    Zaidi ya wanajeshi 100,000 wa Urusi wamekusanyika katika mpaka wa Ukraine.

    Urusi imekuwa ikikana kwamba inapanga kufanya shambulizi.

    Taarifa ya wizara ya ulinzi, iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari vya Urusi, ilisema kuwa inawaondoa baadhi ya wanajeshi wanaofanya mazoezi katika wilaya za kijeshi zinazopakana na Ukraine.

    "Mazoezi kadhaa ya mafunzo ya mapigano, ikiwa ni pamoja na mazoezi, yamefanywa kama ilivyopangwa," msemaji wa Wizara ya Ulinzi Igor Konashenkov alisema.

    Mazoezi mengine yanaendelea, kama vile kuchimba visima vya pamoja vya Russia-Belarus, ambayo yamepangiwa kumalizika tarehe 20 Februari.

    Soma:

  10. Christian Eriksen: Kiungo wa kati wa Brentford arejea uwanjani katika mechi ya kirafiki

    Christian Eriksen
    Maelezo ya picha, Christian Eriksen anasema ni muujiza kwamba amerejea kucheza soka katika klabu ya Brentford

    Christian Eriksen alicheza kwa saa moja katika mechi ya kirafiki dhidi ya Southend United XI siku ya Jumatatu, mechi yake ya kwanza tangu apatwe na mshtuko wa moyo.

    Kiungo wa kati wa zamani wa Spurs Eriksen alitengeneza bao katika ushindi wa 3-2 wa Brentford.

    Mchezaji huyo wa kimataifa wa Denmark, ambaye leo alitimiza umri wa miaka 30, alijiunga na Brentford mwezi uliopita baada ya kutolewa na Inter Milan.

    Wiki iliyopita, Eriksen aliiambia BBC Sport anahisi kama muujiza kuweza kurejea katika taaluma yake baada ya kuzimia alipokuwa akicheza Euro 2020 majira ya joto yaliyopita.

    Eriksen anajiimarisha katika mechi zinazokuja jambo linalochukuliwa na meneja wa Brentford Thomas Frank kama sehemu muhimu ya kufanikisha hilo.

    Alicheza mechi ya ushindani mara ya mwisho tarehe 12 Juni 2021 kwenye Euro 2020 akiwa na Denmark, alipoanguka uwanjani na kupokea CPR kabla ya kupelekwa hospitalini.

    Dane baadaye iliwekwa kifaa cha kumsaidia moyo kinachoweza kupandikizwa.

    Mkataba wa Eriksen wa Inter ulifutwa kwa maelewano ya pande zote mwezi Desemba kwa sababu wachezaji walio na tatizo hilo hawawezi kushiriki Ligi ya Serie A.

    Hata hivyo, Ligi ya Premia haina kanuni sawa na hiyo.

  11. Waziri wa elimu Kenya: Wanafunzi wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wasijiunge na shule za bweni

    Wanafunzi
    Maelezo ya picha, Wanafunzi

    Waziri wa Elimu Prof. George Magoha kwa mara nyingine amesisitiza kwamba wanafunzi ambao ni wapenzi wa jinsia moja wanapaswa kwenda shule na kurejea nyumbani badala ya kujiunga na shule za mabweni.

    Akizungumza baada ya kuzuru darasa la wanafunzi wa ngazi ya kwanza wa shule ya upili linalojengwa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Arya jijini Nairobi, Magoha alisema wanafunzi hao hawafai kuwa katika shule za mabweni.

    CS Magoha aliteta kuwa wanafunzi wakiwa wasomi wa kutwa yaani kwenda na kurejea nyumbani kutawaweka karibu na wazazi wao ambapo mwongozo na uwajibikaji utapewa kipaumbele.

    "Nilisema ikiwa wewe ni mpenzi wa jinsia moja katika shule ya bweni na unaruka ruka kutoka kitanda cha mwanafunzi mwingine kwenda kwa mwingine haki yako itaishia hapo," alisema Magoha akidai kwamba hakueleweka hapo awali.

    "Unaweza kuwa mpenzi wa jinsia moja mzuri ambaye hausumbui mtu yeyote unayeenda kufanya mambo yako ukiwa nje ya shule," aliongeza.

    Profesa Magoha aliongeza kuwa yeye hapingi mapenzi ya jinsia moja lakini hatakubali wahusika wa aina hiyo katika taasisi za masomo.

    Matamshi ya Bw Magoha juu ya suala hili yameibuka tena kufuatia kuibuka kwa madai ya kulawitiwa kwa mtoto mmoja wa shule ya upili.

    Polisi wanachunguza madai hayo ambapo inasemekana ripoti ya madaktari inaonyesha haki za mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 15, wa kidato cha kwanza zilikiukwa.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani kitendo hicho na kutoa wito kwa polisi yakimtaka mkuu wa mashataka ya umma kuanzisha uchunguzi dhidi ya waliohusika na kitendo hicho na kuchukua hatua.

    Brenda Majune, Wakili wa Mahakama Kuu nchini Kenya na Shirika liliso la kiserikali lenye kuangazia ‘Dunia isiyokuwa na Mateso, Ghasia wala Ubaguzi’ amesema:

    ‘Tunatoa wito kwa tume ya waalimu na washika dau wengine kukemea vikali kitendo hiki waziwazi na kuondoa wasimamizi walioshindwa kutekeleza wajibu wao.‘

    Wengine wakitaka wizara ya elimu kuchukua hatua na kuhakikisha haki inatendeka.

  12. Kesi ya wakili wa Kenya kuanza katika mahakama ya ICC

    Paul Gicheru
    Maelezo ya picha, Paul Gicheru

    Kesi ya wakili wa Kenya anayetuhumiwa kuwahonga mashahidi wa upande wa mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) inaanza Jumanne huko The Hague.

    Paul Gicheru anakabiliwa na mashtaka ya kuzuia kutendeka kwa haki kwa kuwashawishi mashahidi kwa ufisadi kuhusu kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008 nchini Kenya.

    Alijisalimisha mwenyewe kwa mahakama mnamo mwezi Novemba 2020.

    Miaka mitano baada ya mahakama ya ICC kutoa hati ya kukamatwa kwake, wakili Mkenya Paul Gicheru kesi yake inaanza kusikilizwa huko The Hague, akituhumiwa kuhujumu kesi ya mahakama inayohusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007.

    Waendesha mashtaka wanadai kuwa alishawishi mashahidi kwa rushwa na kudhoofisha kesi hiyo. ambayo ilimkabili Naibu Rais wa sasa William Ruto.

    Waendesha mashtaka wanadai kuwa alishawishi mashahidi kwa ufisadi na kuhujumu kesi iliyokuwa ikimkabili Naibu Rais wa sasa William Ruto.

    Ruto alikabiliwa na mashtaka ya mauaji, uhamisho na mateso wakati wa ghasia zilizofuatia uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo takriban watu 1,200 waliuawa.

    Hata hivyo, Bw Ruto amekuwa akikana mashtaka kila mara.

    Mahakama ya ICC ilitupilia mbali kesi dhidi ya Ruto ikitaja ukosefu wa ushahidi lakini ikakataa kumwachilia huru.

    Majaji walisema kumekuwa na uingiliaji kati wa mashahidi na uingiliaji wa kisiasa katika kesi hiyo.

    Rais Uhuru Kenyatta amekuwa rais wa kwanza wa nchi kufika katika mahakama ya ICC huko The Hague mwaka wa 2014, lakini mashtaka dhidi yake na wengine watatu yalitupiliwa mbali baadaye mwaka huo huo.

  13. Ethiopia: Kijana aliyepigwa picha akipika jangwani apata msaada

    Boru Konso
    Maelezo ya picha, Kijana aliyepigwa picha akipika jangwani

    Mwandishi wa habari wa Ethiopia aliyepiga picha ya mvulana akipika jangwani peke yake ilyosambaa kwenye mitandao ya kijamii amezungumza na BBC kisa cha picha hiyo yenye ujumbe mzito.

    Picha ya Boru Konso imezua hisia nyingi mtandaoni na kupata watu waliojitolea kumchangia pesa na vitu vingine mvulana huyo.

    Mwanahabari huyo alikuwa akiendesha pikipiki yake katika wilaya ya mashambani ya Mio ambako alikuwa ameenda kuandika habari alipomwona mvulana huyo jioni sana.

    "Mvulana huyo mdogo ambaye pengine umri wake ni chini ya miaka 10, alikuwa amewasha moto na anapika chakula. Nilishtuka nilipomwona mtoto huyu akipika jangwani akiwa peke yake. Huwezi kuona nyumba katika eneo hilo kwa karibu kilomita 10. Niliegesha pikipiki yangu na kumpiga picha," Boru anasema.

    Mvulana huyo alimwambia mwandishi wa habari kwamba familia yake inaishi katika wilaya tofauti na alikuwa akizunguka na wanyama wao kutafuta maji na malisho.

    Ethiopia kwa sasa inakabiliwa na ukame unaowalazimu wafugaji kuzunguka kutafuta malisho.

    Boru alishiriki picha ya mvulana huyo kwenye mitandao ya kijamii na watu wakaanza kuwasiliana ili kutoa msaada.

    Miongoni mwa waliomtembelea kijana huyo ni mfanyabiashara Muna Bakare ambaye alitoa msaada wa vyakula na vitu vingine kwa kijana huyo, familia yake na majirani.

    "Niliiona kwenye mitandao ya kijamii picha ya mtoto huyu mdogo ikagusa moyo wangu, sikupata usingizi kabisa, nilihisi kama ni mwanangu, nikaanza kumtafuta," Muna alisema.

    Muna ameahidi kumlipia mtoto huyo ada ya shule hadi atakapomaliza chuo.

    Boru Konso
    Maelezo ya picha, Boru Konso
  14. Mlinzi wa Manchester City Joao Cancelo azungumza kuhusu uvamizi wa mwaka jana

    mchezaji

    Mlinzi wa Manchester City Joao Cancelo amezungumzia tukio la "kutisha" la kuvamiwa na wezi alilolielezea "lilitishia familia yangu" na kumjeruhi.

    Cancelo, mwenye umri wa miaka 27, alijeruhiwa usoni baada ya kujaribu kupambana na kundi la wezihao wanne waliovamia nyumbani kwake mwezi Disemba mwaka uliopita

    "Familia yangu haistahili kupitia ilichokipitia," alisema nyota huyo wa kimataifa wa Ureno, akizungumza na vyombo va habari kwa mara ya kwanza kuhusu tukio hilo.

    "Ni maisha, inatokea kwenye maisha. Napaswa kusonga mbele."

    Cancelo aliweza kucheza katika mcheo ambao City walishinda 2-1 dhidi ya Arsenal mnamo 1 Januari - siku mbili baada ya tukio hilo. Alipimwa na jopo la matabibu na kuonekana anaweza kucheza mchezo huo.

    Aliweka kwenye mtandaoni wa Instagram picha kuonyesha majeraha yake saa chache tu baada ya tukio hilo la kutisha.

    "Kwa bahati mbaya leo nilivamiwa na watu wanne ambao waliniumiza na kujaribu kuumiza familia yangu," aliandika.

    "Unapoonyesha upinzani, ndivyo inavyotokea. Walifanikiwa kuchukua vito vyangu vyote na kuniacha na uso wangu na hali hii."

    cancello/ instagram

    Licha ya shambulio hilo, Cancelo amekuwa akionyesha kiwango bora kwenye timu yake ya Man City ambapo amekuwa akicheza zaidi upande wa kulia au kushoto wa ulinzi.

    Mapema mwezi huu alisaini mkataba mpya wa miaka mitano na vinara hao wa Ligi Kuu ya England, kusalia Etihad hadi mwaka 2027.

  15. Chombo kinachotarajiwa kugongana na mwezi chatambuliwa mmiliki wake

    chombo

    Wanaastronomia wanasema kwamba sehemu ya roketi iliotarajiwa kugongana na mwezi , mnamo mwezi Machi haikutoka kwa kampuni ya uchunguzi wa anga ya Elon Musk kama ilivyodhaniwa.

    Badala yake wanaamini ni roketi ya China iliorushwa angani 2014. Athari za kugongana huko hazitakuwa kubwa , wanasayansi wamesema.

    Wanaanstonomia mara ya kwanza walitambua mashine ndogoiliokuwa ikielekea kugongana na Mwezi tarehe nne mwezi Machi mnamo mwezi Januari.

    Machine iliorushwa angani na ambayo imekataa kurudi duniani baada ya kukamilisha ujumbe wake huitwa Space Junk.

    Mchanganuzi wa data Bill Gray alitambua kifaa hichokuwa falcon 9 Booster kilichorushwa angani na bilionea Elon Musk katika mpango wake wa Spaxe X.

    Lengo la Bwana Musk ni kutaka binadamu kwenda kuishi katika sayari nyingine.

    Lakini sasa Bwana Gray anasema kwamba alifanya makosa na badala yake ana imani ni roketi iliorushwa angani mwezi Oktoba 2014 ukiwa ni ujumbe wa China wa Change 5-T1 uliorusha chombo angani.

  16. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu mubashara ya leo Jumanne tarehe 15.02.2022