Vita vitadumu kwa miaka-jitayarisheni kuipa Ukraine silaha zaidi-Mkuu wa Nato

Katibu Mkuu Jens Stoltenberg amesema gharama za vita ni kubwa, lakini bei ya kuiruhusu Moscow kufikia malengo yake ya kijeshi ni kubwa zaidi

Moja kwa moja

  1. Serikali ya Congo yawataka raia kujiepusha na matamshi ya chuki na unyanyapaa

    Jeshi

    Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewataka watu kuepuka matamshi ya chuki na unyanyapaa. Katika siku chache zilizopita, ujumbe wa kuhimiza ghasia dhidi ya raia wa Rwanda zimekuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

    Lakini sauti zaidi zinawahukumu. Haya yanajiri huku kukiwa na mvutano kati ya DRC na Rwanda. Congo inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, tuhuma ambayo Kigali inakanusha.

    Msemaji wa serikali ya Congo Patrick Muyaya ameahidi kwamba wale wote wanaotishia kuwashambulia Watutsi watakamatwa na watakabiliwa na mkono wa sheria.

    Miongoni mwa watu waliozungumza dhidi ya vitendo hivyo, ni mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel,ni daktari maarufu Denis Mukwege.

    Wiki chache zilizopita, alitoa wito kwa watu kutotumbukia katika hotuba za kibaguzi ambazo kulingana naye, zitawanufaisha tu maadui wa DRC.

    Kuhusu mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, alikumbuka kuwa unyanyapaa wa sehemu ya jamii unadhoofisha mshikamano wa kitaifa, ambao ni muhimu katika nyakati kama hizi za mgogoro.

    Alitoa wito kwa serikali ya Congo kuwafungulia mashtaka waandishi wa ujumbe unaochochea uhasama dhidi ya watu kulingana na makabila yao au utaifa.

    Katika ujumbe uliorushwa Jumapili jioni kwenye televisheni ya taifa, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Congo alisema kwamba mzozo huu unahusu mamlaka na majeshi ya nchi zote mbili, lakini sio raia.

    Kuibuka tena kwa kundi la waasi la M 23 kwenye mpaka na Rwanda na Uganda kumezorotesha uhusiano kati ya DRC na Kigali.

    Nchi hizo mbili zimenyoosheana vidole zikishutumiana kuunga mkono wanamgambo wenye uhasama na upande mwingine, shutuma ambazo nchi zote zinapinga. Nchi za Afrika Mashariki zinapanga kutuma kikosi cha kikanda kupambana na makundi yenye silaha mashariki mwa DRC. Lakini kwa sasa, hakuna ratiba ya wazi ya kupelekwa kwa majeshi hayo.

    Unaweza pia kusoma

  2. Urusi yaionya Lithuania baada ya kupiga marufuku usafirishaji wa bidhaa kwenye eneo la Urusi la Kaliningrad

    Kaliningrad, ambayo haina mpaka wa ardhi na Urusi, inabakia kuwa eneo muhimu wa kimkakati kwa Moscow

    Urusi imemwita balozi wa Umoja wa Ulaya kujibu marufuku ya Lithuania kwa baadhi ya bidhaa kusafirishwa kwa njia ya reli hadi katika eneo la Urusi la Kaliningrad.

    Lithuania inasema inafungamana na vikwazo vya Umoja wa Ulaya, vilivyowekwa kama sehemu ya mfululizo wa hatua zilizochukuliwa kuhusu uvamizi wa Moscow nchini Ukraine.

    Ikulu ya Kremlin imeziita hatua hizo kuwa "hazijawahi kutokea" na "haramu". Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imetishia "kuchukua hatua kulinda maslahi yake ya kitaifa". Kaliningrad - ambayo haina mpaka wa ardhi na Urusi - ilichukuliwa kutoka Ujerumani mnamo 1945 na inabaki kuwa ya umuhimu wa kimkakati kwa Urusi.

    Wakati wa ziara ya Jumanne huko Kaliningrad, Bw Patrushev alisema kizuizi na Lithuania kilichochewa na Magharibi "katika ukiukaji wa... sheria za kimataifa".

    Katibu wa Baraza la Usalama la Urusi alionya kwamba "hatua zinazofaa" zitachukuliwa "katika siku za usoni". "Madhara yao yatakuwa na athari mbaya kwa idadi ya watu wa Lithuania," aliongeza, bila kutoa maelezo zaidi. Mapema Jumanne, balozi wa EU aliitwa na wizara ya mambo ya nje ya Urusi juu ya kizuizi hicho.

  3. Binti wa Elon Musk ataka kubadili jina kuepuka uhusiano na baba yake

    Elon

    Binti wa tajiri Elon Musk aliyebadili jinsia yake amewasilisha ombi la kubadilisha jina lake kulingana na utambulisho wa jinsia yake mpya na kwasababu anasema "Siishi au nisingependa kuwa na uhusiano na baba yangu mzazi kwa njia yoyote ile, kwa umbo au muundo ."

    Ombi la kubadilisha majina yake yote mawili na kupata cheti kipya cha kuzaliwa kinachoonyesha utambulisho wa jinsia yake mpya liliwasilishwa kwa Mahakama ya juu zaidi ya Kaunti ya Santa Monica mwezi Aprili. Taarifa hii ilijulikana hivi karibuni kupitia baadhi ya mitandao ya habari ya kijami.

    Mtoto huyo Bw Elon Must ambaye awali alijulikana kama Xavier Alexander Musk, ambaye hivi karibuni alitimiza umri wa miaka 18, umri ambao ni umri wa utu uzima katika California, ameiomba mahakama ibadili utambulisho wa jinsia yake kutoka ya kiume na kuwa ya kike na kumsajiri kwa jina jipya, kulingana na nyaraka za mahakama zinazopatikana kupitia mtandao wa PlainSite.org.

    Jina lake jipya liliondolewa katika waraka wa mtandao. Mama yake ni Justine Wilson, ambaye alitaliakiana na Musk mwaka 2008.

    Hakuna maelezo kuhusu nini kilichosababisha kutoelewana baina ya Bw Musk na binti yake.

    Unaweza pia kusoma:

    • Elon Musk atishia kujiondoa kwa mkataba wa Twitter
    • Twitter: Kwa nini Elon Musk alioa mwanamke mmoja mara mbili?
    • Elon Musk: Fahamu siri sita za ufanisi wa kibiashara kutoka kwa mtu tajiri zaidi duniani
  4. Mgahawa maarufu unaoelea wazama baharini Hong Kong

    th

    Mgahawa unaoelea ambao ulikuwa alama maarufu ya Hong Kong umezama siku chache baada ya kuvutwa kutoka bandarini ambako ulifanya kazi kwa takriban miaka 50.

    Mgahawa wa Jumbo ulitumbukia katika Bahari ya Kusini ya China wakati ukielekea eneo lisilojulikana, kampuni mama inayomiliki mgahawa huo ilisema.

    Kampuni ya Aberdeen Restaurant Enterprises ilisema "imehuzunishwa sana na tukio hilo" lakini hakuna wafanyakazi waliojeruhiwa.

    Mgahawa huo ulifungwa Machi 2020 wakati janga la Covid-19 liliposhamiri.

    Zaidi ya wageni milioni 3 wanaaminika kula vyakula vyake kwa miaka mingi, wakiwemo Malkia Elizabeth, Tom Cruise na Richard Branson.

    Pia umeangaziwakatika filamu kadhaa ikiwa ni pamoja na filamu ya Bond - lakini janga la corona lilifanya biashara hiyo kuwa mbaya zaidi baada ya wageni kutotembelea tena.

    Meli hiyo ilipaswa kukaa katika eneo lisilojulikana huku ikisubiri mwendeshaji mpya.

    Lakini ilizama siku ya Jumapili karibu na Visiwa vya Paracel baada ya "kukabiliana na hali mbaya" na kuanza kuingiza maji, Aberdeen Restaurant Enterprises ilisema.

  5. Wachezaji waliobadili jinsia wamepigwa marufuku kushiriki ligi ya kimataifa ya raga

    TH

    Wachezaji waliobadili jinsia wamepigwa marufuku kushiriki michuano ya kimataifa ya wanawake huku bodi inayosimamia ligi ya raga ikifanya utafiti zaidi kuhusu sera yake ya ujumuishaji.

    Ligi ya Kimataifa ya Raga (IRL) ilisema ilitaka "kusawazisha haki ya mtu binafsi ya kushiriki... dhidi ya hatari inayoonekana kwa washiriki wengine".

    Hatua hiyo inajiri huku baadhi ya wanamichezo wakizingatia kujumuishwa kwa watu waliobadili jinsia.

    Waogeleaji waliobadili jinsia Jumapili walipigwa marufuku kutoka kwa mbio za wasomi za wanawake ikiwa wamepitia kubalehe kwa wanaume.

    Rais wa Riadha Ulimwenguni Lord Coe alidokeza kwa BBC kwamba mchezo huo unaweza kufuata mfano wa kuogelea, akisema unatazamiwa kujadili kupitisha sera mpya ya kustahiki na kwamba "haki haiwezi kujadiliwa".

    IRL ilisema imezingatia "maendeleo yanayofaa katika michezo ya dunia" katika kufikia uamuzi wake wa kupiga marufuku "wachezaji wa kike kutoka kwa wanaume" hadi ikamilishe utafiti juu ya sera yake ya mwisho ya kujumuisha.

    Marufuku hiyo itatumika kwa Kombe la Dunia nchini Uingereza mnamo Oktoba, ambayo inashirikisha timu kutoka Australia, Brazil, Canada, Visiwa vya Cook, Uingereza, Ufaransa, New Zealand na Papua New Guinea.

  6. Hospitali Kenya yaasema mauzo ya figo yameongezeka mtandaoni

    TH

    Hospitali kuu ya umma nchini Kenya inasema kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu wanaouliza na kujitolea kuuza figo zao.

    Katika chapisho la Facebook, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ilisema " Figo yangu ni pesa ngapi?" lilikuwa swali lililoulizwa zaidi kupitia ujumbe kwenye ukurasa wao.

    Hospitali hiyo hata hivyo ilishauri kwamba viungo vya mwili vinaweza kutolewa kwa wagonjwa.

    "Tafadhali kumbuka kuwa uuzaji wa viungo ni marufuku kabisa na ni kinyume cha sheria. Unaweza tu kuchangia kwa hiari yako," ilisema.

    Bango la hospitali hiyo linaangazia hatua za kukata tamaa ambazo watu wanafikiria huku kukiwa na ongezeko la bei ya chakula na mafuta.

    Benki ya Dunia mapema mwezi huu ilionya kuwa Afrika mashariki ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na mdororo mkubwa wa uchumi kwa sababu ya vita vya Urusi nchini Ukraine na janga la Corona

  7. Mwanamke aliyekuwa msafishaji amshinda waziri katika kiti cha ubunge Ufaransa

    th

    Mwanasiasa mpya aliyechaguliwa Rachel Keke anaripotiwa kuwa mtu wa kwanza aliyekuwa akifanya kazi ya usafishaji kuwa mbunge nchini Ufaransa.

    Hapo awali Bi Keke alijulikana kwa kuongoza mojawapo ya mgomo mrefu zaidi wa hoteli katika historia ya Ufaransa, akifaulu kufanya kampeni ya malipo ya haki na mazingira bora ya kufanya kazi.

    Baadhi ya wafuasi wake wameuita ushindi wake "ushindi wa wasio na sauti."

    Mbunge huyo mpya alikuwa sehemu ya muungano mpya wa mrengo wa kushoto, NUPES. Keke mwenye umri wa miaka 48 aliahidi sauti kwa wasio na sauti.

    "Mimi ni sauti ya wasio na sauti. Mimi ni kijakazi, mimi ni msafishaji, mlinzi, mlezi, msaidizi wa nyumbani, mimi ni kazi hizi zote zisizoonekana. Na kwenye Bunge, kazi hizi zitaonekana", aliahidi hivi karibuni. -Mbunge mteule, Rachel Kéké.

    Raia huyo wa Ivory Coast anachukua nafasi ya waziri wa zamani wa michezo wa Rais Emmanuel Macron, Roxana Maracineanu, katika kiti kinachowakilisha kitongoji cha kusini mashariki mwa Paris.

    Rafiki wa Rachel Kéké, Emilienne Tai-Seba, hakuweza kuficha furaha yake.

    "Nimejawa na furaha, furaha kubwa, ni ushindi wa wasio na sauti!", alisema.

    Sylvie Kimissa, mwanamke msafishaji na mwenzake wa zamani wa Rachel Kéké aliongeza:

    "Tuko kwenye furaha kwa hiyo hatuna maneno ya kusema... Tuliamini, tupo, tunakwenda Bungeni, tuna mwakilishi ndani ya Bunge!".

    Kéké alikuwa mmoja wa kikundi cha wanawake wasafishaji ambao walipeleka mwajiri wao mahakamani kuhusu malipo na masharti ya kazi na akashinda. Kuwa mbunge hakukuwa katika mipango yake.

    “Nitakutana na vijana wote wa jimbo langu, kwa sababu hawa vijana ambao hawaamini tena maisha, vijana hawa waliokata tamaa, hawa wanaojisemea wenyewe: ‘Hapana, Ufaransa haifai, Ufaransa ni mbaya. Nasema hapana'. Tutafanya kazi pamoja ili kuwapa vijana Ufaransa sura mpya", aliahidi mbunge huyo mteule.

    Muungano wa mrengo wa kushoto wa NUPES uliibuka kuwa moja ya nguvu kubwa za kisiasa baada ya uchaguzi wa wabunge wa Jumapili ambao ulisababisha kupoteza kura nyingi za Rais Macron bungeni.

  8. Mchina ashikiliwa kwa video za ubaguzi wa rangi

    TH
    Maelezo ya picha, Lu Ke alisema alitengeneza video zake ili kueneza utamaduni wa China

    Mtayarishaji wa filamu wa China anayesakwa na Malawi kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wa watoto amekamatwa.

    Lu Ke alikuwa mkazi wa Malawi alipofichuliwa na BBC Africa Eye, ambayo iliripoti kuwa ametumia watoto wa eneo hilo kurekodi video ambazo baadhi zilikuwa na maudhui ya ubaguzi wa rangi.

    Video hizo zinaweza kununuliwa kwa hadi $70 (£55) kwenye mitandao ya kijamii ya China na majukwaa ya intaneti.

    Lu Ke alikana kufanya video hizo za kudhalilisha.Alisema alitengeneza video zake ili kueneza utamaduni wa Kichina kwa jamii ya wenyeji.

    Katika mojawapo ya video zilizoonekana na BBC, kikundi cha watoto wadogo wanaimbishwa kwa Kichina - "Mimi ni zimwi mweusi. IQ yangu iko chini", bila shaka hawajui wanachosema.

    Wakati akirekodiwa kwa siri na mwandishi wa habari za uchunguzi aliyejifanya mnunuzi, Lu Ke alikiri na kisha akakana mara moja kuwa alifanya video hiyo.

    Polisi wa Malawi wiki iliyopita walianza uchunguzi lakini hawakuweza kumkamata mtayarishaji huyo wa filamu wa China kwa kuwa hakupatikana.Msemaji wa Idara ya Uhamiaji na Huduma za Uraia Pasqually Zulu alithibitisha kuwa Lu Ke alikamatwa katika nchi jirani ya Zambia, katika mji wa mashariki wa Chipata.

    Zulu alisema kuwa nchi hizo mbili sasa zinafanya mawasiliano ili raia huyo wa China apelekwe Malawi kwa mamlaka kuendelea na uchunguzi wao.

  9. Samaki mkubwa zaidi duniani wa maji baridi avuliwa Mekong.

    th

    Samaki mwenye uzani wa kilo 300 (lb 661) aliyevuliwa katika mto Mekong nchini Cambodia ndiye samaki mkubwa zaidi wa maji baridi kuwahi kurekodiwa, wanasayansi wanasema.

    Samaki huyo (stingray) amempiku mwenye rekodi ya awali, samaki aina ya kambare mwenye uzito wa 646lb (293kg) aliyevuliwa nchini Thailand mwaka wa 2005.

    "Katika miaka 20 ya kutafiti samaki wakubwa katika mito na maziwa katika mabara sita, huyu ndiye samaki mkubwa zaidi wa maji baridi ambaye tumewahi kukutana nao au ambaye amerekodiwa mahali popote ulimwenguni," Zeb Hogan, mwanabiolojia katika mradi wa uhifadhi unaofadhiliwa.

    Hakuna uwekaji rekodi rasmi au hifadhidata ya samaki wakubwa zaidi wa maji baridi duniani.

    "Kupata na kuweka kumbukumbu za samaki huyu ni jambo la kushangaza, na ni ishara chanya adimu ya matumaini, hata zaidi kwa sababu imetokea katika Mekong, mto ambao kwa sasa unakabiliwa na changamoto nyingi," aliongeza Dk Hogan.

    Mradi wa uhifadhi unafanya kazi na Utawala wa Uvuvi wa Cambodia kuanzisha mtandao wa wavuvi ambao huwatahadharisha watafiti iwapo watakamata samaki wakubwa au walio hatarini kutoweka.

    Stringray kubwa ya maji baridi ni spishi iliyo hatarini kutoweka. Huyu ni stingray wa pili kuchunguzwa na timu hiyo tangu Mei - yule wa awali alikuwa na uzito wa kilo 181.

  10. Vita vitadumu kwa miaka-jitayarisheni kuipa Ukraine silaha zaidi-Mkuu wa Nato

    th

    Nchi za Magharibi lazima zijiandae kuendelea kuunga mkono Ukraine katika vita vinavyoweza kudumu kwa miaka mingi, mkuu wa Nato ameonya.

    Katibu Mkuu Jens Stoltenberg amesema gharama za vita ni kubwa, lakini bei ya kuiruhusu Moscow kufikia malengo yake ya kijeshi ni kubwa zaidi.

    Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson pia ameonya kuhusu mzozo wa muda mrefu.

    Na katika onyo kali, mkuu mpya aliyeteuliwa wa Jeshi la Uingereza alisema Uingereza na washirika walihitaji kuwa na uwezo wa kushinda vita vya ardhini na Urusi.

    Jenerali Sir Patrick Sanders, ambaye alianza kazi hiyo wiki jana, alisema katika ujumbe wake wa ndani ulioonekana na BBC: "Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unasisitiza lengo letu kuu - kulinda Uingereza na kuwa tayari kupigana na kushinda vita vya ardhini - na kuimarisha. hitaji la kuzuia uchokozi wa Urusi na tishio la nguvu."

    Bw Stoltenberg na Bw Johnson walisema kutuma silaha zaidi kutafanya Ukraine kupata ushindi.

    "Lazima tujiandae kwa ukweli kwamba inaweza kuchukua miaka. Hatupaswi kukata tamaa katika kuunga mkono Ukraine," mkuu wa Nato alisema katika mahojiano na gazeti la Ujerumani Bild.

    "Hata kama gharama ni kubwa, sio tu kwa msaada wa kijeshi, pia kwa sababu ya kupanda kwa bei ya nishati na chakula."

  11. Eto'o akiri ukwepaji wa kodi akiwa Barcelona

    TH

    Nyota wa kandanda wa Cameroon Samuel Eto'o amekiri kufanya ulaghai wa mamilioni ya dola kwenye ulipaji wa kodi yake wakati alipokuwa akiichezea Klabu kubwa ya Uhispania Barcelona.

    Mahakama katika jiji hilo imempa kifungo cha miezi 22 jela na faini - lakini ataepuka kwenda jela kwa sababu alikiri hatia.

    Kwa ujumla, Eto'o atalazimika kulipa zaidi ya $8m (£6.5).

    Uamuzi wa mahakama ulisema Eto'o na wakala wake walikwepa kwa makusudi ushuru wa mapato ulitokana na hatimiliki ya picha kati ya 2006 na 2009.

    Wakati wa enzi zake za uchezaji, Eto'o alionekana kuwa mmoja wa washambuliaji bora duniani. Sasa ni rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon.

  12. Viongozi wa Afrika Mashariki watoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mashariki mwa DR Congo

    th

    Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki wametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano na kusitishwa kwa uhasama kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na makundi kadhaa ya waasi wanaopigana katika eneo lake la mashariki.

    Katika mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, viongozi hao pia waliagiza kwamba makundi ya waasi yaachie maeneo yote wanayoshikilia, na kwamba mazungumzo ya amani yaimarishwe.

    Wakuu wa jeshi la kanda pia waliwaeleza marais juu ya taratibu za uendeshaji na sheria za ushiriki wa kikosi cha kijeshi cha Afrika Mashariki, ambacho kitatumwa hivi karibuni katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Mkutano huo pia umelaani matukio ya hivi karibuni ya matamshi ya chuki na mashambulizi dhidi ya makabila fulani nchini DR Congo, yanayodaiwa kuchochewa na shutuma kutoka DR Congo kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23.

    Kikosi hiki kitakachofanya kazi sanjari na jeshi na vikosi vya utawala vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kitakuwa chini ya uongozi wa Kenya.

    Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Kibochi ndiye mwenyekiti wa Kamati ya wakuu wa kijeshi wa nchi hizi.

    Kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa na ofisi ya rais wa Kenya, kikosi hicho kitaundwa kwa mujibu wa itifaki kuhusu amani na usalama pamoja na Kifungu cha 125 kuhusu ushirikiano katika ulinzi.

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari imeidhinisha kujiunga kwa Mkataba huo- kwa itifaki zote ikiwa ni pamoja na ile ya amani na usalama.

    Kundi la M23, mojawapo ya vikundi vingi vilivyoko Kivu Kaskazini, liliibuka kwa mara ya kwanza mwaka 2012 na kudai kuwa linapigania haki za Watutsi wa kabila la Kongo. Mapigano kati yao na vikosi vya serikali yameongezeka tangu Machi, na wiki iliyopita, waliteka mji wa Bunagana kwenye mpaka na Uganda.

  13. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo Jumanne tarehe 21 Juni 2022