Titan: Nyambizi huenda imesalia na chini ya saa 20 za oksijeni

Nyambizi ndogo ya kitalii ambayo imetoweka katika Bahari ya Atlantiki Kaskazini ikiwa na watu watano imesalia na chini ya saa 20 za hewa kulingana na makadirio rasmi.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunahitimisha habari zetu za leo

  2. Tunisia: Mwandishi habari akamatwa kwa kumtusi Rais

    Mwandishi habari maarufu nchini Tunisia amekamatwa na kufunguliwa mashitaka ya kumtusi Rais Kais Said.

    Jaji aliamuru kushikiliwa kwa Zied el Heni na kufunguliwa kesi ambayo akipatikana na hatia anaweza kuhukumiwa miaka mitano gerezani.

    Wanaharakati nchini Tunisia wameelezea wasiwasi juu ya afya yake, ikielezwa aliwahi kuugua kiharusi siku za nyuma.

    Miezi ya hivi karibuni, majaji nchini Tunisia wame washikilia na kufungua uchunguzi kwa zaidi ya wanasiasa, wanahabari, wafanyabiashara, majaji 20 wanaohusishwa na kumpinga rais Said.

    Chama kikuu cha upinzani kimelaani kamatakamata na kueleza ina chochewa kisiasa.

  3. Titan: Nyambizi huenda imesalia na chini ya saa 20 za oksijeni

    .

    Admiral Mauger alisema kuwa kulingana na maelezo ambayo operator alikuwa ametoa hapo awali, nyambizi ilikuwa na takriban saa 96 walipokata mawasiliano kwa mara ya kwanza.

    Kuhusu kwa nini ni hesabu ngumu kutabiri alisema sababu moja ni kwamba inategemea matumizi ya abiria waliopo ndani:

    "Moja ya sababu zinazofanya iwe vigumu kutabiri ni kiasi gani cha oksijeni kilichosalia ni kwamba hatujui kiwango cha matumizi ya oksijeni kwa kila abiria ndani yake."

    Alisema kikosi cha upekuzi kinafanya kazi kwa kudhania kwamba wamebakisha takriban saa 20 kutafuta na kuokoa nyambizi hiyo ambapo mwisho ni kesho asubuhi kwa saa za huko.

  4. Kenya: Mtuhumiwa wa dhehebu la kufunga hadi kufa afia kizuizini

    .

    Mmoja kati ya watuhumiwa 30 wanao shikiliwa na Polisi nchini Kenya kwa tuhuma za kuhusika na dhehebu la kufunga hadi kufa amefariki dunia.

    Joseph Juma Bayuku pamoja na watuhumiwa wengine – walianza mgomo wa kutokula kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu kupinga kushikiliwa kwao. Alipelekwa hospitali kusini-mashariki mwa mji wa Malindi, ambako alifariki.

    “Tunashuku amefariki kutokana na changamoto zilizochangiwa na kugoma kula. Tunasubiri uchunguzi wa maabara tuwe na uhakika juu ya chanzo cha kifo chake,” mwendesha mashitaka mkuu ameiambia mahakama katika mji wa pwani ya Kenya wa Mombasa.

    Hakuna mtuhumiwa ameshitakiwa akiwemo kiongozi wa dhehebu hilo Paul Nthenge Mackenzie, wakati Polisi ikiendelea na uchunguzi. Muhubiri huyo na watuhumiwa wengine wanaaminika kuwashawishi waumini wa kanisa la Good News International kukaa na njaa hadi kufa.

    Tangu mwezi Aprili, miili 336 imefukuliwa kutoka katika makaburi ya kina kifupi katika eneo la msituni. Zaidi ya watu wengine 600 hawajulikani walipo.

    Watuhumiwa wengine wawili ambao wako katika mgomo wa kutokula wamepelekwa hospitali wakiwa hali mbaya.

    Mahakama itaamua Jumanne ijayo ikiwa Bwana Mackenzie ataendelea kusalia kuzuizini kwa siku nyingine 60.

  5. Kai Havertz: Arsenal wakubali mkataba wa £65m na Chelsea kumnunua mshambuliaji wa Ujerumani

    .

    Arsenal wamekubali mkataba na Chelsea wenye thamani ya takriban £65m kumnunua mshambuliaji wa kimataifa wa Ujerumani Kai Havertz.

    Inafahamika kuwa vilabu hivyo vimefanya makubaliano kimsingi ambayo yatamruhusu mchezaji huyo kujadili masuala ya kibinafsi na kupimwa afya yake.

    Ada ya Havertz, ambaye alifunga mabao tisa katika mechi 47 kwa The Blues msimu uliopita, inaweza kuongezeka kwa nyongeza.

    Havertz, 24, alijiunga na Chelsea kutoka Bayer Leverkusen mnamo 2020 kwa dili la takriban pauni milioni 71.

    Pia alifunga bao la ushindi kwa Chelsea katika fainali ya Ligi ya Mabingwa 2021 dhidi ya Manchester City.

    Havertz anatazamiwa kuhamia London huku Mikel Arteta akitafuta kuimarisha timu yake ya Arsenal kufuatia kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa.

    Arsenal pia inamwinda kiungo wa kati wa Uingereza Declan Rice, nahodha wa West Ham, lakini ofa ya pili kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 - yenye thamani ya hadi £90m - ilikataliwa Jumanne.

  6. Nyambizi iliyotoweka inaweza kuwa inaolea juu ya maji – kamanda wa zamani wa nyambizi

    .

    Mtaalamu wa utafutaji na uokoaji wa nyambizi nchini Australia, Frank Owen, aliambia BBC "imani yake iliongezeka kwa kiwango cha juu " aliposikia ripoti za sauti kubwa kugunduliwa na vigunduzi vya sauti vinavyoelea.

    "Kuna sababu kadhaa za hilo," anaeleza. "Kwanza, ndani ya meli hii kuna mpiga mbizi mstaafu wa jeshi la wanamaji wa Ufaransa. Angejua itifaki ya kujaribu kutahadharisha vikosi vya utafutaji ... unapiga kelele kwa nguvu."

    Anasema ishara ya sauti iliochukuliwa na boya juu ya maji inaonesha kuwa nyambizi yenyewe inaweza kuwa karibu na juu pia

    Hata iwapo Titan ipo juu ya maji ni vigumu kuiona. Ni vyombo viachache vinavyosalia juu ya maji

    Lakini kutumia safu ya maboya ya kugundua sauti ili kuzunguka ishara hizo kunaweza kulipata eneo ambalo nyambizi hiyo ipo

  7. Eneo lenye mabaki ya meli ya Titanic ni hatari sana – Mpiga mbizi

    .

    Dik Barton, mpiga mbizi wa kwanza wa Uingereza kuona ajali ya Titanic, anasema eneo hilo ni "hatari" sana.

    "Kuna mteremko wa ndani na mkondo wa maji ambao huzunguka. Nguvu ya chini ya maji ni ndogo," aliiambia Good Morning Britain ya ITV.

    Akizungumzia kuhusu jinsi chombo hicho kingeweza kupatikana, Barton aliongeza kuwa huenda itabidi kurejeshwa ardhini kwa kuwa hakuna njia ya kuipata nyambizi hiyo chini ya bahari .

  8. Titan: Roboti za chini ya maji ziko tayari kusaidia kupata eneo la nyambizi iliotoweka

    .

    Tumesikia kutoka kwa Klabu ya Wagunduzi, ambao wanajitolea kusaidia kutafuta mahali ambapo nyambizi iliotoweka ipo kwa kutumia roboti za chini ya maji kutoka kampuni ya Magellan ya Uingereza .

    Magari yanayoendeshwa kwa njia ya rimoti yanaweza kwenda umbali wa hadi mita 6,000 na yamekuwa kwenye mabaki ya Titanic hapo awali, rais wa Klabu ya Explorers Richard Garriott amesema.

    Wawili waliomo kwenye meli ya chini ya maji, Hamish Harding na Paul-Henri Nargeolet, ni wanachama wa klabu hiyo, mtandao wa kimataifa wa uchunguzi wa kisayansi.

    Garriott alibainisha kuwa kumekuwa na dalili za uhai wakati msako huo ulipoingia katika saa muhimu - sauti za kishindo ziliripotiwa hapo awali katika eneo ambalo ndege hiyo inaaminika kuwa ipo.

  9. Nyota wa Ghana Asamoah Gyan astaafu soka

    Mchezaji soka huyu mwenye umri wa miaka 37- alianza kucheza soka ya kulipwa mwaka 2003
    Maelezo ya picha, Mchezaji soka huyu mwenye umri wa miaka 37- alianza kucheza soka ya kulipwa mwaka 2003

    Nyota wa soka wa Ghana Asamoah Gyan ametangaza rasmi kustaafu soka.

    "Ni wakati wa kutundika jezi na buti kwa heshima ninapostaafu rasmi kutoka kwa kandanda.'' Gyan alisema katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Twitter.

    Mshambuliaji huyo alifunga mabao 51 katika mechi 109 alizoichezea nchi hiyo, na kumfanya kuwa mfungaji bora wa Ghana.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 alianza soka ya klabu mwaka 2003 akiichezea timu ya kwanza ya Ghana, Liberty Professionals, na baadaye akacheza Ulaya katika klabu za Udinese ya Serie A ya Italia, Rennes ya Ligue 1 ya Ufaransa na Sunderland ya Ligi Kuu ya Uingereza, ambapo alivunja rekodi ya uhamisho wa klabu hiyo.

    Aliwahi kucheza katika Milki ya Falme za Kiarabu, akiichezea Al Ain, akiisaidia timu hiyo kushinda taji la Ligi ya UAE na kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo akiwa amefunga mabao 28 katika mechi 32.

    Pia alichezea Shanghai SIPG, Kayserispor na North East United. Akiwa nyumbani kwao Ghana, Gyan aliichezea timu ya taifa ya wakubwa, Black Stars, katika Kombe la Dunia la Fifa mara tatu - mwaka wa 2006, 2010 na 2014.

    Ndiye mfungaji bora wa Kombe la Dunia barani Afrika, akiwa na jumla ya mabao sita.

    Aliichezea nchi yake katika michuano saba ya Kombe la Mataifa ya Afrika, ambapo Black Stars ilimaliza nafasi ya tatu mwaka wa 2008 na katika nafasi za pili mwaka wa 2010 na 2015.

    Gyan alitumia siku zake za mwisho za maisha ya soka akichezea Legon Cities FC ya nchini Ghana. Pia aliandika kwa jina LeGYANDry, akielezea maisha yake na safari ya mpira wa miguu.

  10. Ghasia mbaya zakumba maeneo mawili ya Somalia

    Takriban watu 36 wamekufa katika matukio mawili tofauti ya ghasia nchini Somalia - katika jimbo la Puntland na eneo la Lower Shabelle.

    Madaktari walisema takriban watu 26 waliuawa katika mapigano makali siku ya Jumanne huko Garowe, mji mkuu wa jimbo la Puntland.

    Wengine 10 walikufa baada ya mabomu yaliyokuwa yakidhibitiwa kwa mbali kulipuka katika kijiji kilicho kusini-magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

    Walioshuhudia walisema watu kadhaa waliuawa katika mlipuko wa kwanza na bomu la pili kulipuka wakati raia na wanajeshi walipokuwa kuwaokoa waliojeruhiwa.

  11. Vikosi vya Sudan vyalaumiana kufuatia shambulio dhidi makao makuu ya shirika la ujasusi

    Mapigano kati ya vikosi hasimu nchini Sudan yalianza tarehe 15 Aprili
    Maelezo ya picha, Mapigano kati ya vikosi hasimu nchini Sudan yalianza tarehe 15 Aprili

    Vikosi hasimu vya Sudan vimerushiana lawama baada ya makao makuu ya kijasusi kushambuliwa katika mji mkuu Khartoum, huku picha mtandaoni zikionyesha moto mkubwa ukiwaka juu ya jengo hilo.

    Jeshi lilisema Kikosi maalum cha (RSF) kilishambulia jengo hilo, huku RSF ikisema jengo "lililopo chini ya udhibiti [wake]" lilikumbwa na mashambulizi ya angani na mizinga kutoka kwa jeshi.

    RSF katika taarifa ilishutumu jeshi la Sudan kwa "jaribio la wazi la kufuta ushahidi wa matendo yao ya kikatili wakati wa utawala wao wa kidhalimu".

    Makao makuu ya kijasusi yapo katika jengo moja na wizara ya ulinzi, makao makuu ya jeshi na makazi ya rais.

    Shambulio dhiddi ya jengo hilo lilikuja siku ya mwisho ya usitishaji mapigano wa saa 72 - ambao ulitarajiwa kukamilika alfajiri ya Jumatano.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan: Jeshi na RSF zalaumiana kwa kutoheshimu makubaliano ya kusistisha vita
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  12. N'Golo Kante: Kiungo wa kati wa Chelsea akubali kujiunga na mabingwa wa Saudia Al-Ittihad

    th

    Kiungo wa kati wa Chelsea na Ufaransa N'Golo Kante amekubali kusajiliwa na mabingwa wa Saudi Arabia Al-Ittihad.

    Mkataba wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 huko Stamford Bridge unamalizika mwishoni mwa Juni.

    Kante amekuwa na majeraha na aliichezea Chelsea mechi tisa wakati wa kampeni ya 2022-23.

    Ataungana na Karim Benzema katika klabu ya Al-Ittihad baada ya Mfaransa mwenzake kuondoka Real Madrid na kukubaliana nao mkataba wa miaka mitatu mwezi huu.

    Hatua hiyo inahitimisha kipindi cha mafanikio makubwa katika soka la Uingereza kwa Kante.

    Aliisaidia Leicester City kushinda Ligi ya Premia msimu wa 2015-16 kabla ya kuhamia Stamford Bridge.Akiwa Chelsea Kante alishinda Champions League, Premier League, Europa League na FA Cup.

    Aliteuliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Chama cha Waandishi wa Soka na Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Wachezaji Soka kwa 2016-17.

    Pia alitekeleza jukumu muhimu wakati Ufaransa iliposhinda Kombe la Dunia mnamo 2018.

    Kante amesaini mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo wenye thamani ya £86m.

  13. Vurugu gerezani Honduras: Takriban 41 wauawa katika ghasia za jela ya wanawake

    th

    Takriban watu 41 wameuawa katika ghasia katika gereza la wanawake nchini Honduras siku ya Jumanne.

    Inafahamika kuwa mapigano yalizuka kati ya magenge hasimu, ambapo genge moja liliwasha moto katika seli.

    Maafisa wanasema moto huo ulisababisha vifo vingi lakini baadhi ya waathiriwa walipigwa risasi.

    Naibu Waziri wa Usalama wa nchi hiyo, Julissa Villanueva, ametangaza hali ya hatari na kuahidi kukabiliana na ghasia hizo.

    Pia aliidhinisha "kuingilia kati mara moja" kwa wazima moto, polisi na wanajeshi.

    "Hasara ya maisha ya binadamu haitavumiliwa," Bi Villanueva alisema.

    Haijulikani ikiwa wote waliouawa walikuwa wafungwa wa jela hiyo, ambayo iko takriban kilomita 20 kutoka mji mkuu wa Honduras, Tegucigalpa, na inashikilia karibu watu 900.

    Wafungwa wengine kadhaa wamepelekwa hospitalini.

    Delma Ordonez, ambaye anawakilisha wanafamilia wa wafungwa, aliviambia vyombo vya habari vya ndani sehemu ya gereza "imeharibiwa kabisa" katika ghasia hizo.

    Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha wingu kubwa la moshi wa kijivu ukipanda kutoka kwa gereza la wanawake.

  14. Mlio wa sauti wasikika katika msako wa chombo cha majini kilichotoweka baharini

    th

    Waokoaji waliokuwa wakitafuta sehemu ya chini ya maji ya chombo cha watalii kilichopotea karibu na eneo la ajali ya Titanic wameripotiwa kusikia sauti za kishindo karibu na eneo ambalo nyambizi hiyo ndogo hiyo ilipotea.

    Kwa mujibu wa arifa ya ndani ya serikali ya Marekani iliyoonekana na vyombo vya habari vya Marekani, sauti hizo zilisikika na ndege kila baada ya muda wa dakika 30 siku ya Jumanne.

    Sona ya ziada ilitumiwa saa nne baadaye na sauti hizo bado zilisikika.

    BBC imewasiliana na Idara ya Usalama wa Taifa na Walinzi wa Pwani kwa maoni.

    CNN na Rolling Stone zote zililiripoti juu ya hatua hiyo.

    Watu watano walikuwa kwenye chombo hicho wakati mawasiliano yalipopotea saa moja na dakika 45 ndani ya kuanza safari yake siku ya jumapili.

    Kulingana na Walinzi wa Pwani ya Marekani , watu hao wana chini ya masaa 30 ya oksijeni iliyobaki.

    Operesheni ya utafutaji katika jimbo la Newfoundland nchini Canada hadi sasa imeshindwa kupata chochote.

    Hata hivyo, imeongezwa kwa upana ili kujumuisha rasilimali zaidi na utaalamu wa uokoaji kutoka kwa makampuni binafsi.

    Unaweza pia kusoma

  15. Biden amtaja Xi kuwa 'Dikteta' siku moja baada ya mazungumzo ya Beijing

    th

    Rais wa Marekani Joe Biden amemtaja rais wa China Xi Jin ping kuwa dikteta katika hafla ya kuchangisha fedha huko California.

    Matamshi yake yanakuja siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kukutana na Bw Xi kwa mazungumzo mjini Beijing, ambayo yalilenga kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu.

    Bw Xi alisema baadhi ya mafanikio yamepatikana mjini Beijing, huku Bw Blinken akidokeza kwamba pande zote mbili ziko tayari kwa mazungumzo zaidi.

    China bado haijajibu maoni ya Bw Biden.

    Rais Biden, katika hafla ya kuchangisha pesa Jumanne usiku kwa saa za huko, pia alisema Bw Xi alikuwa na aibu juu ya mvutano wa hivi majuzi kuhusu puto ya kijasusi ya Uchina ambayo ililipuliwa juu ya Marekani.

    Ziara ya Bw Blinken mjini Beijing - ya kwanza kwa mwanadiplomasia mkuu wa Marekani katika takriban miaka mitano - ilianzisha upya mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili.Biden na Bw Xi waliipongeza hatua hiyo kama nzuri .Lakini Bw Blinken aliweka wazi kuwa tofauti kubwa zimesalia kati ya nchi hizo mbili.

    Washington na Beijing zimekuwa zikipingana kwa muda mrefu kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo biashara, haki za binadamu na Taiwan.

    Lakini mahusiano yamezorota hasa katika mwaka uliopita.

  16. Titan:Nyambizi ndogo iliyotoweka baharini imesalia na takriban saa 30 za oksijeni

    TH

    Nyambizi ndogo ya kitalii ambayo imetoweka katika Bahari ya Atlantiki Kaskazini ikiwa na watu watano imesalia na chini ya saa 30 za hewa kulingana na makadirio rasmi.

    Haya hapa ya hivi punde tunayojua kuhusu shughuli ya uokoaji hadi sasa

    Makamanda wa Walinzi wa Pwani ya Merika wanaendelea kuongoza msako tata kwenye eneo la bahari "kubwa kuliko jimbo la Connecticut" - karibu kilomita za mraba 20,000.

    Vikosi vya uokoaji kutoka jeshi la wanamaji la Kanada, jeshi la anga na walinzi wa pwani, pamoja na walinzi wa anga wa jimbo la New York wanasaidia.

    Chombo cha utafiti cha Ufaransa pia kimejiunga na utafutaji

    Nyambizi ya chini ya maji ya Titan inadhaniwa kuwa takriban maili 900 (1,450km) mashariki na maili 400 (643km) kusini mwa mji mkuu wa Newfoundland, St Johns.

    Mawasiliano yalipotea kwa mwendo wa saa moja na dakika 45 baada ya kuzama kwa saa mbili hadi kwenye eneo la ajali la Titanic ambalo liko kwenye kina cha 3,800m.

    Kulingana na makadirio ya Walinzi wa Pwani ya Marekani , Titan ina takriban masaa 30 ya oksijeni iliyobaki ndani ya chombo hicho

    Unaweza pia kusoma

  17. Walio ndani ya nyambizi ya Titan wanatumia hewa gani?

    Lee Kibblewhite anauliza je ni "hewa" gani ambayo waliomo ndani ya Titan wanatumia?

    Sehemu ya chini ya maji ina sehemu ya shinikizo ili kuhimili shinikizo la nje chini ya maji. Kwa hivyo, walio ndani wanapaswa kuwa chini ya shinikizo la kawaida la anga kama juu ya ardhi na kupumua hewa ya kawaida.

    Hata hivyo, baada ya muda mrefu, oksijeni itatumika na CO2 itazalishwa.

    Kulingana na maelezo ya kampuni, manowari hiyo ina uwezo wa kuishi chini ya maji kwa saa 96.

  18. 'Sehemu ya bahari ni nyeusi sana, huwezi kuona mkono wako mbele ya uso wako'

    .
    Maelezo ya picha, Mabaki ya meli ya Titanic yanaonekana wakati wa kupiga mbizi kwenye ajali ya Titanic mnamo 1986.

    Mtaalamu wa meli ya Titanic Tim Matlin ameambia shirika la habari la Reuters kwamba sakafu ya Bahari ya Atlantiki – eneo ambalo meli ya Titanic - ni "jeusi na lenye baridi kali".

    Mbali na hayo, "sehemu ya bahari ni matope na inatiririka. Huwezi kuona mkono wako mbele ya uso wako. Njia pekee ya kupata mahali ulipo ni kwa kitu kinachoitwa sonar. Hata rada haifanyi kazi," alisema.

    Matlin aliongeza: "Kwa hiyo ninahofia maisha ya watalii hao ambao wako kwenye meli."

  19. Mwana wa rais wa Marekani Hunter Biden kukiri makosa ya ushuru na bunduki

    .
    Maelezo ya picha, Hunter Biden

    Mwana wa Rais wa Marekani Joe Biden, Hunter Biden, anatarajiwa kukiri makosa mawili ya uhalifu wa kodi na kukiri kumiliki bunduki kinyume cha sheria akiwa mtumiaji wa dawa za kulevya, baada ya uchunguzi wa miaka mitano.

    Mwanasheria wa Marekani huko Delaware amewasilisha nakala zinazoonyesha makubaliano ya ombi yameafikiwa.

    Anatarajiwa kukubaliana na matibabu na ufuatiliaji wa madawa ya kulevya.

    Masharti ya makubaliano hayo huenda yakamweka nje ya jela.

  20. Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda aomba hifadhi nchini Afrika Kusini

    .
    Maelezo ya picha, Mshukiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda Fulgence Kayishema,

    Mawakili wanaomwakilisha mshukiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda Fulgence Kayishema, ambaye alikuwa mtoro kwa miaka 22 kabla ya kukamatwa mwezi uliopita, wameiambia Mahakama ya Cape Town kwamba mteja wao ataomba hifadhi kwa misingi ya kisiasa nchini Afrika Kusini.

    Inaweza kuchelewesha uwezekano wake wa kurejeshwa nchini Rwanda kwa miaka kadhaa na kuchelewesha kwa kiasi kikubwa kesi yake kwa tuhuma za mauaji ya halaiki, kushiriki katika mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

    Anashutumiwa kwa kuhusika moja kwa moja katika mauaji hayo pamoja na kuamuru mauaji ya tarehe 15 Aprili 1994 ya watu 2,000 wa kabila la Kitutsi waliokuwa wamejificha katika Kanisa Katoliki magharibi mwa Rwanda.

    Alifunguliwa mashitaka mwaka 2001 na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ya Umoja wa Mataifa, ambayo imefunga, huku kesi yake ikihamishiwa Rwanda kwa ajili ya kusikilizwa.

    Bw Kayishema, ambaye sasa ana umri wa miaka sitini, alikamatwa kwenye shamba la zabibu katika jimbo la Western Cape nchini Afrika Kusini mwezi uliopita.

    Pia anakabiliwa na mashtaka 54 nchini Afrika Kusini yanayohusiana na ulaghai na kukiuka sheria ya uhamiaji.

    Mnamo Jumanne, wakili Juan Smuts alisema Bw Kayishema alitupilia mbali ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana, ambalo lilipaswa kusikilizwa Jumanne.

    Mamlaka ya Kitaifa ya Mashtaka ya Afrika Kusini imesema ombi la Bw Kayishema la hifadhi halina uhusiano wowote na mwenendo wa mahakama nchini Afrika Kusini na kwamba mashtaka zaidi yataongezwa atakapofikishwa mahakamani mwezi Agosti.

    Anasalia kizuizini.

    Takriban Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa nchini Rwanda na Wahutu wenye msimamo mkali katika muda wa siku 100 mwaka 1994.