Maandamano ya Upinzani Kenya: Wanaharakati wasema makumi ya watu wameuawa toka maandamano yaanze

Shirika la haki zi kibinadamu la Haki Afrika limewataka maafisa wa polisi kutotumia kile walichokitaja kuwa nguvu kupitia kiasi dhidi ya waandamanaji wanaopigania haki yao.

Moja kwa moja

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo tukutane tena hapo kesho majaaliwa

  2. Ulinzi au ugaidi - majibu yaliyogawanyika kuhusu namna polisi wa Kenya walivyoshugulikia maandamano

    g
    Maelezo ya picha, Polisi walikabiliana na waandamanaji jijini Nairobi kwa siku ya pili mfululizo siku ya Alhamisi

    Rais wa Kenya William Ruto amewapongeza polisi kwa kuhakikisha amani inakuwepo wakati wa maandamano yaliyofanyika hivi karibuni ya upinzani huku kundi kuu la kutetea haki za binadamu likielezea namba walivyokabiliana nayokama "kitendo cha kigaidi".

    Katika kipindi cha miezi minne iliyopita ya maandamano kumekuwa na vifo kadhaa, ikiwa ni pamoja na watu 10 kupigwa risasi na polisi wiki iliyopita. Vyombo vya habari vya ndani ya Kenya vinaripoti kuwa watu sita walikufa siku ya Jumatano katika makabiliano na polisi.

    Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC), ilisema "kulikuwa na mtindo wa kutatiza kuonyesha kwamba vitendo vya [polisi] na utumiaji nguvu wa mauaji vilipangwa".

    Lakini Bw Ruto alisema polisi walikuwa wakiwalinda watu na mali.

    “Nawapongeza polisi kwa kusimama kidete, kwa kuhakikisha amani inakuwepo na kuhakikisha wahalifu wote wanachukuliwa hatua,” Bw Ruto alisema.

    Hakuna idadi rasmi ya vifo lakini Amnesty International inasema kuwa polisi wamewaua watu wasiopungua 30 tangu Machi, tangu maandamano ya kuipinga serikali yalipoanza.

    Mwanachama wa mtandao wa mashirika ya kiraia anayefuatilia jinsi polisi wanavyoshughulikia waandamanaji katika kaunti za magharibi za Kisumu na Migori alisema kuwa vikosi vya usalama vinaonekana "kutekeleza amri ya kuua".

    Mwanaharakati huyo ambaye alitaka kutotajwa jina, alisema wana ushahidi wa picha wa watu waliopigwa risasi mgongoni na risasi za moto.

    Wiki jana Jumatano, afisa mmoja wa polisi alikataa kufuata agizo la kuwafyatulia risasi waandamanaji na alipigwa na wenzake na kulazwa hospitalini,” aliongeza mtu huyo.

    Upinzani umeitisha misururu ya mikutano ya kupinga kubuniwa kwa ushuru mpya na kupanda kwa gharama ya maisha. Hivi sasa nchi hiyo inakabiliwa na siku ya pili ya maandamano ya siku tatu.

    Makundi ya ndani na ya kimataifa pampja na wanadiplomasia wa kigeni wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu hali nchini Kenya na kuzitaka pande zote mbili kutafuta suluhu la mazungumzo.

  3. Ndege ya Jeshi iliyokua kwenye msafara wa Waziri wa Ulinzi Kenya yaanguka

    Ajali

    Helikopta ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) imeanguka jioni hii katika uwanja wa Chemolingot Kaunti ya Baringo.

    Ndege hiyo ilikuwa imebeba maafisa waliokuwa sehemu ya msafara ulioandamana na Waziri wa Ulinzi Aden Duale katika ziara ya usalama katika eneo hilo lenye hali tete.

    Ikithibitisha kisa hicho, KDF ilisema kuwa helikopta hiyo iligonga mti na kuanguka wakati wa kupaa.

    Watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo waliojumuisha maafisa wa serikali wamenusurika bila kujeruhiwa.

    "Abiria wote walishuka salama na wako katika hali shwari," ilinukuliwa na Citizen Digital ya Kenya.

  4. Saudi Pro League: Cristiano Ronaldo anavyoongoza mapinduzi katika soka la Asia

    g
    Maelezo ya picha, Cristiano Ronaldo alicheza mchezo wake wa kwanza kwa Al-Nassr mwezi Januari

    Huenda timu za Ligi Kuu ya Uingereza zinatatizika kukubaliana na vilabu vya Saudi Arabia vinavyowahamisha baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa lakini mashabiki wa Riyadh, Jeddah na miji mingine mikubwa ya Mashariki ya Kati na Asia pia wanalazimika kuzoea hali mpya ya soka.

    Tangu Cristiano Ronaldo ajiunge na Al-Nassr - moja ya vilabu vya 'Big Four' pamoja na wapinzani wa Riyadh Al-Hilal na wababe wa Jeddah Al-Ittihad na Al-Ahli – tangu mwezi Desemba, nchi hiyo imekuwa katika uangalizi wa kimataifa wa soka na Jezi ya njano ya klabu inazidi kufahamika Ulaya na kwingineko.

    "Kutazama rangi ya manjano au 'The Yellow' ikienea duniani kote kunaniridhisha na kunifurahisha sana lakini pia ninahisi mwaminifu kwa ligi ya nchini," shabiki wa Nassr

    Ligi ya Saudia itatawala barani Asia?

    Huku timu ya taifa ikishiriki katika michuano sita ya Kombe la Dunia na vile vile kushinda makombe matatu ya bara la Asia huku vilabu vikiwa vimeshinda Ligi ya Mabingwa wa Asiamara sita, Saudi Arabia imekuwa ikitamba katika kanda na bara.

    Nguvu mpya ya kifedha ya nchi katika soka, hata hivyo, imeiweka katika kiwango tofauti kabisa uwanjani.

    'Cristiano alifanya kile kinachochukua miaka kufanya'

    g
    Maelezo ya picha, Al-Nassr wameshuhudia kuongezeka kwa mauzo ya shati, hasa yenye jina la Ronaldo

    Wachezaji nyota sio tu kwamba huleta ubora zaidi lakini pia wameundwa ili kusababisha mashabiki zaidi, mikataba ya matangazo, udhamini, mauzo ya bidhaa na uwekezaji.

    Lengo la Saudi Arabia ni kwamba ligi hiyo iwe katika 10 bora zaidi duniani kwa kupata mapato ifikapo 2030.

    Tayari, kuna ishara chanya za kibiashara.

    Al-Nassr watacheza na Benfica siku ya Alhamisi kisha watamenyana na Paris St-Germain na Inter Milan nchini Japan baadaye mwezi huu.

    Klabu hiyo pia imetia saini mkataba wa jezi na kampuni ya Nike, huku afisa mmoja akiambia BBC kwamba miamba hiyo ya mavazi ya Marekani inaweza kusaidia kuhakikisha shati za njano zinazovaliwa kote ulimwenguni ni rasmi.

    Mnamo Novemba, kulikuwa na ziara 10,000 kwa ukurasa wa bidhaa wa tovuti ya klabu.Mnamo Januari - mwezi ambao Ronaldo alisaini - idadi hiyo iliongezeka hadi 300,000.

    "Tumeona mashati mengi ya Al-Nassr tangu msimu uliopita na inaongezeka sana," anasema Mohammed.

    "Cristiano alifanya mara moja kile kinachochukua kampeni za uuzaji na nyara miaka mingi kufanya.

    "Tulicheza dhidi ya Celta [Jumatatu] na mashabiki wengi walikuwa pale wakiwa wamevalia shati ya Nassr yenye jina la Cristiano nyuma na nembo ya Nassr mbele.

    "Yote ni juu ya kuongeza kiwango, ni uboreshaji kama huo."

  5. Ndege nyingine yaanguka katika Ziwa Victoria, Bukoba

    Ajali

    Ndege ya kijeshi iliyokuwa na marubani wawili imeanguka ndani ya maji ya Ziwa Victoria, nchini Tanzania mita chache kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba.

    Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasia Chatanda tukio hilo limetokea saa 3 asubuhi ya leo na kuhusisha ndege ya Jeshi yenye namba JW 9127.

    Kamanda Chatanda anasema ndege hiyo na marubani wake wawili walikuwa katika mazoezi ya kawaida kabla ya kuanguka ziwani.

    Marubani hao Leonard Nkundwa (45) na Alex Venance (30) wamekimbizwa kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.

    Ni miezi minane tu imepita tangu tukio hilo la Novemba 6, 2022 la kuanguka kwa ndege ya Precision Air namba ATR 42-5H PWF katika eneo hilo kutokana na hali mbaya ya hewa na kuua watu 19 na wengine 26 kunusurika.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

  6. Maandamano ya Upinzani Kenya: Wanaharakati wasema makumi ya watu wameuawa toka maandamano yaanze

    g

    Mashirika mawili tofauti ya haki za binadamu yametaja idadi ya waliofariki katika maandamano nchini Kenya kufikia kati ya watu 30 tangu maandamano ya kuipinga serikali yaanze wiki mbili zilizopita.

    Shirika la Amnesty International kupitia Mkurungenzi wake Mkuu Irungu Houghton wakati huohuo limeshtumu utumiaji wa nguvu kupitia kiasi unaotekelezwa na maafisa wa polkisi dhidi ya waandamanaji.

    ‘’Tangu maandamano ya Machi, 2023, Amnesty imegundua matukio ya mauaji yasiyopungua 30 ya mauaji ya polisi ya waandamanaji. Ni pamoja na maandamano ya tarehe 20 Machi na 27 (mauaji 12), maandamano ya saba Saba( mauaji 12) na Julai 19 (mauaji 6). Vifo hivyo vimehusishwa na kukosa hew ana gesi ya kutoa machozi na risasi zenye sumu’’, alisema Bw Houghton.

    Wakati huohuo shirika la haki zi kibinadamu la Haki Afrika limewataka maafisa wa polisi kutotumia kile walichokitaja kuwa nguvu kupitia kiasi dhidi ya waandamanaji wanaopigania haki yao.

    Kiongozi wa shirika hilo Hussein Khalid amesema kwamba takriban watu 27 wameripotiwa kufariki tangu maandamano hayo ya kuipinga serikali yalipoaza wiki mbili zilizoisha kutokana na nguvu za kupitia kiasi zinazotumiwa na maafisa wa polisi.

    Hivyobasi Shirika hilo limetoa wito kwa vinara wawili Rais William Ruto na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

    Kulingana na Amnesty uchunguzi wake wa awali ulibaini i kuwa polisi walitumia vipigo, kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini kwa waandamanaji, matumizi mabaya ya gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha na ukiukaji mwingine mkubwa wa haki za polisi kwa maandamano.

    ‘’Tunatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa polisi wa vurugu na uhalifu wa maandamano ya serikali’’, imesema Amnesty katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, na kuongeza kuwa:

    ‘’Tunadai uchunguzi wa haraka na mashtaka ya maafisa wa polisi na makamanda wao kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi na Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma’’.

    Shirika hilo limewataka Inspekta Jenerali wa Polisi, Japhet Koome naWaziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Serikali ya Kitaifa, Kithure Kindiki wachukue hatua za vitendo kuhakikisha haki ya kila mtu kukusanyika kwa amani na kuandamana.

  7. Kevin Hart atembelea Kumbukumbu ya mauaji ya kimbari Rwanda

    g

    Mchekeshaji maarufu na muigizaji wa sinema nchini Marekani - Kevin Hart amezulu Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Kigali na kutoa heshima kwa wahanga wa Mauaji ya Kimbari ya 1994 ya Rwanda mapema leo asubuhi, vimeripoti vyombo vya habari nchini humo.

    Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Kigali, ni mahala ambapo miili ya weahanga 250,000 ya mauji ya kimbari imezikwa.

    Kulingana na gazeti la The New Times nchini humo, awali Haute Baso, alitembelea jumba la mitindo ya mavazi yanabuniwa na kutengenezwa Rwanda al maarufu Made in Rwanda, ambako alinunua mavazi.

    Kevin Hart na familia yake wamekuwa Kigali tangu Julai 19. Walionekana kwa mara ya kwanza katika Haute Baso, chapa ya mitindo ya Rwanda.

    Hart alijulikana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha Televisheni 'Undeclared'.

    Alifanya filamu yake ya kwanza katika 'Paper Soldiers', kisha akapata umaarufu zaidi kutoka kwa filamu nyingine kama vile 'Soul Plane', 'The 40-Old Virgin', 'Death at a Funeral' na 'Little Fockers'.

    Taarifa zinasema kuwa Hart atazuru kaskazini-magharibi mwa Rwanda, hasa Mbuga ya Kitaifa ya Volkano - nyumbani kwa sokwe walio hatarini kutoweka, na pia kushiriki katika shughuli tofauti za kitamaduni na kijamii nchini humo.

  8. Vita vya Ukraine: Urusi yaipiga Odessa kwa usiku wa tatu mfululizo

    g

    Askari wa Urusi wamefyatua risasi tena katika maeneo ya Nikolaev na Odessa - mara ya pili na ya tatu, usiku wa Alhamisi, na kuyafanya mashambulio hayo kuwa ya tatu tangu mwanzo wa wiki, mtawaliwa.

    Utawala wa Ukraine inasema kuwa Urusi inajaribu kuinyima Ukraine fursa ya kusafirisha chakula nje kwa kupiga makombora miji ya bandari.

    Jeshi la Wanahewa la Ukraine limeripoti kuwa, jeshi la Urusi lilirusha makombora 19 ya meli na ndege zisizo na rubani 19 za Kamikaze hadi Odessa na Nikolaev. Miongoni mwa makombora hayo ni pamoja na makombora saba ya Onyx, makombora matatu ya baharini ya Kalibr, na makombora matano ya Iskander-K ya ardhini.

    Ulinzi wa anga wa Ukraine ulipiga shabaha 18 kati ya 38.

    "Kutokana na mashambulio ya Urusi, kuna uharibifu katikati ya Odessa, moto ulizuka kwenye eneo la mita 300 za mraba. Waathiriwa wawili wa shambulio hilo pia wamelazwa hospitalini, "aliandika Oleg Kiper, mkuu wa Utawala wa Kijeshi wa Mkoa wa Odessa.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  9. Idadi ya waliokufa katika kanisa la kufunga hadi kufa Kenya yafikia 425

    g

    Serikali ya Kenya imesitisha awamu ya nne ya uteketezaji wa miili katika msitu unaohusishwa na ibada ya siku za kiama.

    Miili 6 zaidi imefukuliwa katika msitu wa Shakahola leo, na kufanya idadi ya vifo kufikia 425.

    Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Rhoda Onyancha anasema shughuli hiyo imesitishwa ili kuruhusu magari ya mizigo kufanyika katika miili 87 iliyofukuliwa katika awamu hii ya hivi karibuni.

    Waziri wa usalama wa Kenya, Julai 10, alidai kuwa polisi wametambua makaburi 40 ya pamoja katika msitu huo uliokuwa na watu wengi.

    Wafuasi wa ibada hiyo wanaaminika kuwa ama walijiua kwa njaa, walipigwa vibaya au kunyongwa.

    Unaweza pia kusoma:

    • BBC yazungumza na mmoja wa waokoaji wa Shakahola, na mengine mengi na Roncliffe Odit.
    • Dhehebu la Mchungaji Mackenzie Kenya: Mama aliyetoroka msitu wa Shakahola kuokoa watoto wake
    • Mackenzie aliwasifu wafuasi wanaokufa kama mashujaa, na kutaja mazishi yao kuwa harusi
  10. Polisi Ujerumani wamsaka simba anayeshukiwa kuzurura ndani ya jiji la Berlin

    g

    Polisi wa Ujerumani wanamsaka mnyama anayeaminiwa kuwa simba jike kuenekana katika eneo la kusini-magharibi mwa jiji la Berlin.

    Video iliyotumwa kwenye Twitter Jumatano asubuhi inaonekana kuonyesha simba jike katika msitu uliopo katika eneo la Kleinmachnow.

    Wakaazi wameagizwa kusalia majumbani mwao huku polisi wakimsaka mnyama huyo wa porini.

    Zoo za mitaa, na hifadhi za nyingine za wanyama zimesema hakuna simba aliyetoroka kutoka katika vituo vyao.

    "Hatujui alitoka wapi," msemaji wa polisi aliviambia vyombo vya habari vya ndani.

    Shahidi mmoja aliwaambia polisi kuwa walikuwa wamemtazama simba huyo akimkimbiza ngiri, vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti.

    Wakaazi wa Brandenburg wametahadharishwa na polisi kuhusu tishio la mnyama huyo na wametakiwa kusalia ndani hadi ilani nyingine itakapotolewa kuhusu tukio hilo.

    Wakazi pia wameshauriwa kuwahifadhi wanyama wao wanaofugwa ndani ya nyumba.

    Helikopta zimetumwa kujaribu kumtafuta mnyama huyo asiyeweza kupatikana, mamlaka ilisema.

    Madaktari wa mifugo na wawindaji walio na bunduki pia wanahusika katika kumtafuta mnyama huyo. Gazeti la udaku la Ujerumani Bild lilisema maafisa wanatumai kumkamata simba huyo salama.

  11. Maandamano ya Azimio Kenya: Sita wameripotiwa kufariki katika maandamano ya kuipinga serikali

    TH

    Watu sita waliuawa Jumatano katika makabiliano kati ya polisi wa Kenya na waandamanaji, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.

    Vitoa machozi vilirushwa katika mji mkuu, Nairobi, na mji wa pwani wa Mombasa kwa wale waliokuwa wakiandamana kulalamikia gharama ya juu ya maisha.

    Watu kadhaa walijeruhiwa baada ya kupigwa risasi wakati polisi wakipambana na waandamanaji.

    Shule zilifungwa katika miji miwili mikuu nchini humo huku maandamano ya upinzani ya siku tatu yakianza na yameingia siku ya pili leo.

    Takriban watu 300 walikamatwa kote nchini.

    Biashara nyingi zimesalia kufungwa kwa hofu ya uporaji, huku watu wakiogopa kukamatwa katika mapigano makali.

    Wiki iliyopita, takriban watu 14 walikufa katika maandamano - 10 walipigwa risasi na polisi.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamewakosoa vikali polisi kwa kile wanachokiita matumizi yao ya nguvu kupita kiasi Jumatano iliyopita.

    Upinzani uliitisha msururu wa maandamano baada ya nyongeza ya ushuru kuanzishwa mwezi uliopita na serikali ya Rais William Ruto.

    Unaweza pia kusoma

  12. Usalama waimarishwa katika sehemu mbali mbali katika siku ya pili ya maandamano

    th

    Usalama umeimarishwa katika sehemu mbali mbali za Kenya huku maandamano yaliyoitishwa na upinzani kulalamikia gharama ya juu ya maisha yakiingia siku ya pili .

    Katika mji mkuu Nairobi na mji wa pwani wa Mombasa ,wafanyibiashara wengi wamezifungua biashara zao kuendelea na shughuli ingawaje kwa uangalifu.

    Hali mjini Kisumu -magharibi mwa nchi ni shwari huku barabara zikionekana kuwa tupu bila magari au watu wengi na maduka mengi yamesalia kufungwa .

    Serikali jana ilitangaza kuwa shule zilizokuwa zimefungwa kwa siku ya kwanza ya maandamano zifunguliwe leo na masomo yaendelee .

    Upinzani hata hivyo unasisitiza kwamba maandamano yataendelea licha ya kulalamikia hatua ya kukamatwa kwa viongozi wake kadhaa ambao wameripotiwa kuzuiliwa katika vitu mbali mbali vya polisi .

    Mmoja wa waliokamatwa ni mbunge wa Embakasi masharikI-eneo bunge lililopo jijini Nairobi ambaye familia yake inadai amezuiliwa katika kitu kimoja cha polisi katika kaunti ya Kirinyaga,nje kidogo ya Nairobi .

    Unaweza pia kusoma

  13. Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner asema shughuli zao zinaendelea Afrika

    .
    Maelezo ya picha, Yevgeny Prigozhin aliongoza maasi ya muda mfupi dhidi ya serikali ya Urusi mwezi uliopita.

    Mwanzilishi wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner, Yevgeny Prigozhin, ameiambia Afrique Media TV kwamba mamluki wake wataendelea kufanya kazi katika nchi za Afrika waliko.

    "Tunaendelea kufanya kazi katika nchi zote tulikoanza au tunakofanya kazi hii ya ushirikiano na maendeleo kwa sasa," alisema katika mahojiano yaliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa pro-Kremlin TV.

    "Iwapo usaidizi wa Kundi la Wagner unahitajika mahali popote ili kukabiliana na magenge na magaidi na kulinda maslahi ya watu wa nchi hizi, tuko tayari kuanza mara moja kutekeleza jukumu hili baada ya kukubaliana juu ya masharti."

    Aliongeza kwamba "hakukuwa na hakutakuwa na kupungua kwa shughuli zetu barani Afrika".

    Matamshi yake yalifuatia uvumi kuhusu uwezekano wa kuondolewa kwa mamluki wa Wagner kutoka Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

    Uvumi huo ulianza kuenea baada ya Bw Prigozhin kuandaa maasi ya muda mfupi nchini Urusi mnamo 24 Juni.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameshutumu mamluki wa Wagner kwa kujihusisha na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Mali na CAR.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Tanzania yanufaika na ufadhili wa mradi wa elimu kutoka Canada

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC News, Dodoma
    .

    Nchi ya Canada hii leo imetangaza kutoa msaada wa dola milioni 25 zitakazotumika katika mradi wa elimu uitwao ‘Kila Binti Asome’.

    Mradi huu una lengo la kuwawezesha kielimu watoto wa kike katika ngazi ya shule za msingi na sekondari Tanzania Bara na Zanzibar.

    Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dodoma katika sherehe za utiaji saini wa makubaliano hayo kati ya Waziri wa Canada anayehusika na Maendeleo ya Kimataifa na Waziri wa Elimu wa Tanzania.

    “Mradi huu utawezesha mabinti, wenye umri kati ya 10-19, kujifunza na kuongeza ujuzi wao ili kuendana na mahitaji ya soko la sasa na baadae nchini Tanzania,” amesema Waziri Harjit Sajjan.

    Kwa upande wake, Profesa Adolf Mkenda ambae ni Waziri wa Elimu nchini Tanzania, amesema Tanzania iko katika hatua za mwisho za kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ikiwemo kuwa na miaka 10 ya elimu ya lazima badala ya miaka 7.

    “Vile vile elimu ya sekondari itajikita zaidi katika kutoa elimu ya jumla pamoja na elimu ya amali, mageuzi ambayo yatahitaji rasilimali nyingi,” amesema Mkenda.

    Katika kipindi cha miaka 14, Canada imetoa zaidi ya dola milioni 250 za Canada kwenye mifumo ya elimu ikiwemo kuboresha viwango vya elimu na upatikanaji wa elimu.

    Mradi huu utakuwa chini ya UNICEF.

  15. WHO yatoa tahadhari kuhusu dawa ya kikohozi nchini Cameroon

    .

    Shirika la Afya Duniani limetoa tahadhari kuhusu kundi la dawa ya kikohozi ya NATURCOLD inayosemekana kuwa sio salama kwa binadamu huko Cameroon.

    Shirika hilo linasema viambato vitatu vilivyotumika kutengeneza dawa hiyo ya maji ni mchanganyiko unaotumika kupunguza dalili za homa ya kawaida, mafua na mzio wa puani.

    Hata hivyo, uchambuzi wa sampuli za dawa ya Naturcold uligundua kuwa bidhaa hiyo ilikuwa na kiasi kisichokubalika cha diethylene glikoli.

    Kiasi cha 28.6 % (mara 286 zaidi ya kiwango cha ukomo kinachokubalika) kiligunduliwa kwenye dawa hiyo.

    Kikomo kinachokubalika sio zaidi ya 0.10%.

    Diethylene glikoli kwa kawaida hutumiwa kama kiyeyusho, lakini inaweza kuwekwa katika dawa kinyume cha sheria kama mbadala wa bei nafuu kwa viambato vya gharama kubwa zaidi.

    Mchanganyiko huu pamoja na mwingine: ethylene glycol, ni sumu kwa binadamu na inaweza kusababisha kifo.

    Kundi la dawa hiyo lenye kiwango kisichokubalika lilitambuliwa kwa mara ya kwanza nchini Cameroon na kuripotiwa kwa WHO tarehe 13 Machi 2023.

    Sampuli hizo zilifikishwa WHO tarehe 27 Juni 2023 na kufanyiwa uchunguzi zaidi katika maabara ya WHO yenye mkandarasi aliyehitimu.

    Mtengenezaji aliyebainishwa wa bidhaa iliyoathiriwa ameorodheshwa kwenye kifungashio cha bidhaa kama FRAKEN INTERNATIONAL (England).

    Mamlaka ya udhibiti wa kitaifa ya Uingereza, MHRA, hata hivyo, imethibitisha kuwa hakuna kampuni kama hiyo nchini Uingereza.

    WHO inasema kuna uwezekano mkubwa dawa hiyo ya kikohozi ina idhini ya kuuzwa katika nchi au maeneo mengine.

    Inaweza pia kuwa imesambazwa kwa nchi jirani kupitia masoko yasiyo rasmi.

    WHO inapendekeza zaidi kwamba ikiwa mtu ana bidhaa hiyo, haipaswi kutumiwa.

    Na mtu yeyote ambaye anaweza kuwa ameitumia na kupata athari isiyotarajiwa au athari mbaya anashauriwa kutafuta matibabu ya haraka.

    Pia unaweza kusom:

  16. Amri ya kutotoka nje yatangazwa magharibi mwa Ethiopia huku ghasia zikianza upya

    .

    Mamlaka katika eneo la magharibi mwa Ethiopia la Gambella imeweka marufuku ya kutotoka nje usiku baada ya watu wengi kuuawa katika ghasia zilizoanza upya.

    Amri ya kutotoka nje - ambayo inaanza kutekelezwa mara moja - inakataza harakati za magari na mtu binafsi kati ya 7pm na 6am.

    Serikali ya eneo haijataja takwimu za majeruhi lakini iliapa katika taarifa yake kuwawajibisha "wajumbe uongozini" ambao ilisema walihusika katika "uvurugaji wa amani."

    Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani ghasia hizo zilianza mapema wiki hii na zimekuwa na mwelekeo wa kikabila huku takriban maeneo mawili yakishuhudia mapigano.

    Vyanzo vya habari katika mji mkuu wa mkoa wa Gambella vilisema biashara na ofisi zilifungwa siku ya Jumatano.

    Eneo hilo ambalo linapakana na nchi jirani ya Sudan Kusini, limeshuhudia vurugu za mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni.

    Mwezi Mei takriban watu saba waliripotiwa kuuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika mapigano katika mji mkuu wakati mwaka jana mji huo ulivamiwa na wapiganaji waasi kutoka mkoa jirani wa Oromia ambapo makumi ya watu waliuawa.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Prigozhin: Kiongozi wa Wagner aonekana kwenye video akiwa Belarus

    .
    Maelezo ya picha, Video inayodaiwa kumuonyesha kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin (kushoto) huko Belarus

    Kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner Yevgeny Prigozhin amehusishwa na video kwenye mtandao wa Telegram inayoonekana kumuonyesha akiwa Belarus.

    Kiongozi huyo anaonekana kwenye video hiyo akiwakaribisha wapiganaji na kuelezea maendeleo ya hivi karibuni vitani huko Ukraine kama "aibu".

    Pia amedokeza kwamba Wagner inaweza kujiunga tena na vita siku zijazo.

    Video hiyo pia inaonekana kuthibitisha taarifa ya Belarus kwamba wapiganaji wa Wagner sasa walikuwa wakufunzi wa kijeshi wa jeshi la nchi hiyo.

    Hii itakuwa video ya kwanza ya Prigozhin kuonekana tangu Wagner kuzindua uasi wa kutumia silaha ndani ya Urusi mwishoni mwa Juni.

    Video hiyo imepigwa imetolewa ikiwa na mwanga hafifu, na inaonyesha Prigozhin akiwa amesimama kwenye njia ya lami uwanjani, akiwa amezungukwa na miti na kile kinachoonekana kama maghala na mahema.

    Uthibitisho wa BBC umehakiki kwamba mpangilio wa mahema, miti na majengo unalingana na eneo lililo kwenye ukingo wa magharibi wa kambi.

    Watu wengi waliojificha wanaweza kuonekana nyuma, na wanasikika wakishangilia.

    Licha ya mwanga hafifu, Prigozhin anatambulika tu na mwonekano wake, na wazungumzaji wa Kirusi wanaofahamu taarifa zake za awali wanasema sauti na namna ya kuzungumza ni yake bila shaka.

    Katika video hiyo, Prigozhin anasema kwamba wapiganaji "walipigana vyema" nchini Ukraine na "wamefanya mengi" kwa Urusi, na anakosoa vikali mwenendo wa sasa wa vita.

    “Kinachoendelea hivi sasa vitani ni fedheha ambayo hatutaki kuhusika kwa vyovyote vile, na tunatakiwa kusubiri hadi tuweze kuonyesha uwezo wetu kikamilifu,” anasikika akisema.

    Anaendelea kusema kwamba "uamuzi umechukuliwa wa kukaa hapa Belarus kwa muda fulani" na Wagner angetumia wakati huo kulifanya jeshi la Belarusi kuwa "jeshi la pili duniani".

    Kiongozi wa Wagner pia amedokeza kwamba wapiganaji wake "wangeendelea kujiandaa" na ikiwezekana kurejea vitani nchini Ukraine "wakati tuna uhakika kwamba hatutalazimika kujitia aibu sisi wenyewe na uzoefu wetu".

    Soma zaidi:

  18. Manipur: Ghadhabu India baada ya wanawake wawili kusimamishwa uchi katika jimbo linalokumbwa na ghasia

    Manipur imekumbwa na ghasia za kijamii tangu mqwzi Machi
    Maelezo ya picha, Manipur imekumbwa na ghasia za kijamii tangu mqwzi Machi

    Video inayowaonyesha wanawake wawili wakisimamishwa uchi na kundi la watu katika jimbo lililokumbwa na ghasia kaskazini mashariki mwa Manipur imezua hasira nchini India.

    Polisi wanasema wamefungua kesi ya ubakaji na utekaji nyara wa genge dhidi ya "wahalifu wasiojulikana wenye silaha".

    Hili pia huenda likatawala mijadala katika kikao cha bunge, ambacho kitaanza Alhamisi.

    Wanasiasa wa upinzani wamemtaka Waziri Mkuu Narendra Modi kutoa tamko kuhusu mgogoro wa Manipur.

    Polisi wanasema kisa hicho kilitokea tarehe 4 Mei lakini kesi hiyo iligonga vichwa vya habari vya kitaifa siku ya Alhamisi baada ya video ya tukio hilo kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

    Serikali imezitaka kampuni zote za mitandao ya kijamii kufuta video hiyo kwenye majukwaa yao.

    Takriban watu 130 wamefariki na maelfu wameyahama makazi yao tangu mapigano ya kikabila yaanze mwezi Mei huko Manipur.

  19. New Zealand:Shambulizi la ufyatuaji risasi latokea saa chache kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia la Wanawake

    ..

    Shambulizi ya ufyatuaji risasi limesababisha vifo vya watu wawili katikati mwa Auckland, New Zealand, saa chache kabla ya jiji hilo kufunguliwa kwa Kombe la Dunia la Wanawake la Fifa.

    Watu wengine sita, wakiwemo maafisa wa polisi, walijeruhiwa na mtu aliyejihami pia amefariki baada ya tukio hilo lililotokea saa 07:22 (19:22 GMT) kwenye eneo la katikati mwa mji.

    Waziri Mkuu Chris Hipkins alisema shambulio hilo halikuonekana kama kitendo cha kigaidi na mashindano hayo yataendelea kama ilivyopangwa.

    Umma, aliongeza, unaweza kuhakikishiwa kwamba polisi wameondoa tishio hilo na hakukuwa na hatari inayoendelea baada ya tukio hilo kwenye mtaa wa Queen.

    Hakuna sababu za kisiasa au kiitikadi za shambulio hilo zilizotambuliwa, waziri mkuu alisema.

    Mtu aliyetekeleza shambulizi hilo alikuwa amejihami kwa bunduki.

    Bw Hipkins alishukuru "polisi wanaume na wanawake wa New Zealand ambao walikimbia kulikotokea milio ya risasi, moja kwa moja ili kuokoa maisha ya wengine".

    "Matukio ya aina hii hutokea haraka na vitendo vya wale wanaohatarisha maisha yao ili kuokoa wengine sio kingine zaidi ya ushujaa," aliongeza.

    Kulingana na Meya wa Auckland Wayne Brown, wafanyakazi wote wa Fifa na timu za kandanda wamehesabiwa na kuthibitishwa kuwa salama.

    Fifa ilitoa "rambi rambi" zake kwa familia za waathiriwa na kusema ilikuwa katika mawasiliano na mamlaka ya New Zealand.

    "Timu shiriki zilizo karibu na tukio hili zinapata usaidizi kuhusiana na athari yoyote ambayo inaweza kutokea," ilisema.

    Mechi ya ufunguzi itafanyika kati ya New Zealand na Norway katika uwanja wa Eden Park wa jiji hilo.

    Kombe la tisa la Dunia la Wanawake linaandaliwa kwa pamoja na New Zealand na Australia.

  20. Mwanajeshi wa Marekani aliyekamatwa Korea Kaskazini alikuwa amezuiliwa Seoul kwa kupigana

    .

    Travis King, mwanajeshi wa Marekani aliyekimbilia Korea Kaskazini, alikuwa amezuiliwa kwa kupigana huko Korea Kusini kabla ya kuvuka mpaka.

    Nyaraka za mahakama zilionyesha pia aliharibu gari la polisi huko Seoul.

    Mwanajeshi huyo mwenye umri wa miaka 23 alikuwa ameachiliwa hivi majuzi na alikuwa akirudishwa Marekani alipotoroka.

    Alijiunga na ziara ya eneo la Usalama wa Pamoja na kukimbilia Korea Kaskazini, ambayo haijasema chochote hadi sasa.

    Bado haijafahamika nia yake ilikuwa nini kuvuka mpaka.

    Mamlaka za Marekani zimesema kwamba alifanya hivyo "kwa makusudi, kwa hiari yake mwenyewe" na ilionyesha wasiwasi kuhusu ustawi wake.

    Mamake King, Claudine Gates aliambia ABC News kwamba hangeweza kufikiria mwanawe akifanya kitu kama hicho. Lazima awe "na matatizo ya akili", alisema.

    Bi Gates alisema mara ya mwisho kuwasiliana na mwanajeshi huyo wa Marekani ilikuwa "siku chache zilizopita", alipomwambia kwamba hivi karibuni atarejea Fort Bliss, kituo chake cha jeshi huko Texas.

    King aliripotiwa kuchunguzwa kwa shambulio nchini Korea Kusini mnamo Septemba 2022. Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, alishukiwa kumpiga raia wa Korea katika klabu ya usiku huko Seoul.

    Mahakama ilimtoza faini ya won 5m (£,3,000; $3,950) kwa "kupiga mateke mara kadhaa" mlango wa nyuma wa gari la polisi na kupiga kelele huku akitumia "lugha chafu" kwa maafisa waliojaribu kumkamata.

    Ripoti za ndani zilizowanukuu maafisa zilisema aliachiliwa mnamo Julai 10 baada ya kutumikia kifungo cha miezi miwili jela kwa makosa ya kushambulia, lakini hakufafanua.

    Soma zaidi: