Vita vya Ukraine: Urusi yashambulia maghala ya nafaka ya Odesa mpakani mwa Romania

Wakuu wa kijeshi kutoka kambi ya kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, wanakutana baadaye Jumatano kujadili mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Niger wiki iliyopita.

Moja kwa moja

  1. AFCON 2027: CAF yakamilisha ukaguzi wa miundombinu Kenya, Tanzania na Uganda

    AFCON 2027

    Timu ya Wakaguzi wa utayari wa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kuwa wenyeji AFCON 2027, kutoka Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) imehitimisha ukaguzi wao salama Agosti 2, 2023 Zanzibar kwa kikao cha majumuisho kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo wa Tanzania Saidi Yakubu.

    Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Wallace Karia amezishukuru Serikali za nchi hizo kwa ushirikiano waliotoa kufanikisha ukaguzi huo ikiwemo nia ya kuomba kuwa wenyeji wa mashindano hayo.

    “Ukaguzi umemalizika vizuri, kwa kweli wameona tupo ‘serious’ na kuna mambo ambayo wametuelekeza tuyafanye, kwa upande wetu kama Tanzania bara na Zanzibar yapo mengi yamefanyika kwa sababu wakandarasi wapo site na vitu vinaonekana, wameelekeza hili jambo hili tulifanye kwa pamoja na wametoa siku 10 ili kukamilisha nyaraka zote zinazohitajika kulingana na maelekezo yao” amesema Rais Karia.

    Aidha, Rais Karia ametoa rai kwa mataifa yote matatu kutekeleza kwa pamoja maelekezo yaliyotolewa ili kufikia lengo la Afrika Mashariki kuandaa mashindano hayo ambayo hayajawahi kufanyika katika ukanda huo na nchi hizo zinatakiwa kukamilisha miundombinu ya michezo itakayotumika kwenye mashindano hayo kabla ya Desemba 2025.

  2. Serikali Somalia yaomba radhi kwa kupeleka mkimbiaji 'anayekimbia taratibu' kwenye mbio za kimataifa

    Somalia

    Waziri wa michezo wa Somalia ameomba radhi baada ya mshiriki mwanamke katika mbio za kimataifa za mita 100 kuonekana akikimbia taratibu kiasi kwamba watu wanahoji aliwezaje kuchaguliwa.

    Katika mashindano ya michezo ya vyuo vikuu katika mji wa Chengdu nchini China, Nasra Abubakar Ali alitumia karibu sekunde 22 kumaliza mbio hizo - karibu mara mbili ya muda aliyoutumia mshindi.

    Katika video ya tukio hilo, ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii, mwanariadha huyo wa Somalia alionekana kukimbia kama sio mwanariadha, taratibu na kuonekana kama vichekesho.

    Waziri wa Michezo Mohamed Barre Mohamud alitaja tukio hilo kuwa la aibu. "Kilichotokea leo haikuwa uwakilishi wa watu wa Somalia... tunaomba radhi kwa watu wa Somalia," alisema.

    Inaelezwa kuwa ukweli wa kwamba hakuwa na uzoefu wa kushindana umewafanya baadhi ya Wasomali kushangaa kwa nini alichaguliwa.

    Kama kilichofanyika ni kupata umaarufu na kujulikana inaelezwa kwenye mitandao kwamba, ameshinda sawa na medali ya dhahabu.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

  3. Rais Kagame amteua binti yake kushika wadhifa nyeti Rwanda

    Ange Kagame

    Rais wa Rwanda Paul Kagame amemteua binti yake kushika wadhifa muhimu katika ofisi yake. Ange Kagame, 29, ameteuliwa kuwa naibu mkurugenzi mtendaji anayesimamia baraza la mikakati na sera, kwa mujibu wa taarifa za kikao cha baraza la mawaziri kilichoongozwa na Rais Kagame siku ya Jumanne.

    Taarifa hiyo pia ilitangaza uteuzi wa watu wengine wakiwemo mabalozi wapya wa Ethiopia, Morocco, Misri na Guinea.

    Bi Ange Kagame amekuwa akifanya kazi katika ofisi ya rais kama mchambuzi mkuu wa sera tangu 2019 akiwa na shahada za sayansi ya siasa na masuala ya kimataifa kutoka vyuo vikuu vya Marekani.

    Watoto wengine wawili wa Rais Kagame pia wana nyadhifa serikalini. Mwanawe mkubwa, Ivan Kagame, aliteuliwa mwaka 2020 kwenye Bodi ya Maendeleo ya Rwanda - ambayo ina jukumu la kuharakisha ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya kibinafsi.

    Mtoto wa tatu wa kiume, Ian, ni afisa wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda, na mwaka jana aliingizwa katika katika kikosi cha ulinzi wa rais.

  4. Watu 60 wanaodaiwa kuwa magaidi wauawa Kenya

    Kindiki
    Maelezo ya picha, Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya, Kithure Kindiki

    Watu 60 wanaotajwa kuwa ni magaidi 60 na waliohusika katika shambulizi la Jumanne juko Lamu nchini Kenya wameuawa, kwa mujibu wa Waziriwa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki.

    Waziri Kindiki alisema watu hao walidhibitiwa na maafisa wa usalama katika operesheni iliyokamilika leo asubuhi.

    "Watu wote walioshambulia watu wetu jana wameuawa, wote," Kindiki aliwaambia wabunge Jumanne.

    Hata hivyo, BBC haiwezi kuthibitisha kwa uhuru alichosema waziri kuhusu suala hilo. Washambuliaji hao wanaoaminika kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la al Shabaab walishambulia mabasi manne yaliyokuwa yamebeba takriban abiria 200 katika makutano ya kaunti za Lamu na Tana River. Watu wawili walithibitisha kupoteza maisha katika shambulio hilo.

    Kwa mujibu wa Kindi, Operesheni hiyo ilifanikiwa kuwadhibiti magaidi hao kwa sababu ya doria za mara kwa mara za maafisa wa usalama katika barabara ya Lamu-Garsen.

  5. Watu 20 wahofiwa kufariki katika ajali nyingine ya boti Ziwa Victoria

    Accident - Lake Victoria

    Takriban watu 20 wanahofiwa kufariki dunia baada ya boti ya abiria waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama katika Ziwa Victoria nchini Uganda.

    Tukio hilo limetokea alfajiri ya leo Jumatano, 02 Agosti, 2023 wakati boti hiyo kubwa inayojulikana kama Kinaala, ilikuwa ikisafirisha abiria na mizigo kutoka Lwanabatya katika Kaunti ya Kyamuswa, Wilaya ya Kalangala kwenda Kasenyi karibu na Entebbe katika Wilaya ya Wakiso, kwa mujibu wa wavuvi.

    Mpaka sasa watu 5 wameshathibitishwa kufariki na wengine hawajulikani walipo.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani na kuthibitishwa na Mwandishi wa BBC wa Kampala, boti hiyo iliripotiwa kupigwa na upepo mkali karibu na kisiwa cha Nsazi kwenye Ziwa Victoria wilayani Mukono.

    Inaelezwa kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba watu thelathini ambapo watu kumi wameokolewa na wavuvi, kulingana na mvuvi Noah Kizza.

  6. Miili 13 yapatikana ajali ya Mitumbwi Ziwa Victoria

    Ajali Ziwa Victoria

    Miili 12 kati ya 13 ya watu waliozama maji katika ziwa Victoria nchini Tanzania imepatikana kufuatia shughuli za uokoaji zilizofanyika kwa siku tatu.

    Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya ndani, idadi hiyo inafikisha jumla miili 13 iliyoopolewa hadi kufikia asubuhi ya leo Agosti 2, 2023, baada ya mwili wa mtoto wa mwaka mmoja kuopolewa siku ya ajali.

    Julai 30, 2023 mitumbwi miwili iliyokuwa imebeba waumini 28 wa Kanisa Takatifu la Mungu wa Kiroho (KTMK) ilizama ziwani ambapo watu 14 waliokolewa na kukimbizwa hospitalini.

    Walikuwa wakitoka katika kijiji cha Mchigondo kwenda Kitongoji cha Bulomba katika Kijiji cha Igundu, huko Bunda mkoani Mara kabla ya kukutana na dhoruba iliyopiga mitumbwi yao na kuzama.

    Wengi katika ajali hiyo na waliopoteza maisha ni watoto na wanafunzi wa Shule ya Msingi Bulomba wilayani Bunda.

  7. Maelfu ya Wanawake Afrika kupoteza maisha kwa Uingereza kupunguza misaada - Ripoti

    UK-Africa

    Maelfu ya wanawake barani Afrika watapoteza maisha wakiwa wajawazito na wengine wakati wa kujifungua kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya misaada ya Uingereza inayokwenda nje ya nchi, mawaziri wameonywa.

    Kwa mujibu wa tathmini ya ndani ya watumishi wa umma, karibu wanawake 200,000 zaidi pia watakabiliwa na utoaji mimba usio salama.

    Ripoti yao inaonyesha athari za kupunguzwa kwa bajeti ya misaada ya nje mwaka huu. Hata hivyo Ofisi ya Mambo ya Nje inasema bajeti yake kwa nchi za kipato cha chini imepunguzwa kwa musa tu ili kufikia lengo la kuweka akiba, lakini itapanda na kukaribia mara mbili.

    Waraka wa ndani unasema kupunguzwa kwa misaada kwa 76% kwa Afghanistan kutaacha baadhi ya wanawake na wasichana walio hatarini zaidi duniani bila huduma muhimu. Na nusu milioni ya wanawake na watoto nchini Yemen hawatapata huduma za afya.

    Bajeti ya Idara ya Usaidizi wa Maendeleo ya Nje ina thamani ya zaidi ya £900m kwa mwaka huu. Hitimisho hilo linakuja katika tathmini iliyofanywa na watumishi wa umma wa Ofisi ya Mambo ya Nje mapema mwaka huu, ili kuwafahamisha mawaziri kabla hawajaamua cha kupunguza.

  8. Kimbunga Khanun chaua 34 Japan

    Khanun

    Kimbunga kimepiga eneo la Kusini mwa Japan, na kulazimisha maelefu ya watu kuhama na kusababisha umeme kukatika karibu robo tatu ya nyumba zote kwenye visiwa vya Okinawa.

    Kimbunga Khanun kinachosonga mbele polepole - ni cha tatu kupiga Asia Mashariki katika wiki kadhaa - kikitishia kuzidisha mvua kubwa zaidi huko Beijing katika kipindi cha zaidi ya karne moja.

    Kimbunga hicho kilichosababisha mafuriko pia kimsababisha vifo vya takriban watu 34 nchini China hadi sasa. Wataalamu wanasema kwamba hali mbaya ya hewa kama hii itatokea mara kwa mara kwa sababu ya ongezeko la joto duniani.

    Khanun kinakuja baad aya vimbunga vingine viwili, Talim na Doksuri, kusababisha dhoruba kali, ambayo pia iligusa Ufilipino na Taiwan, na kuua zaidi ya watu 30, katika wiki chache zilizopita.

    Visiwa vya joto vya Japan vya Okinawa vinatarajiwa kukabiliwa na dhoruba ya kimbunga hocho kasi ya kilomita 252 kwa saa (156mph) siku ya leo Jumatano.

    Takriban watu 20,000 wameshauriwa kuhama na takriban safari 900 za ndege zimekatishwa katika uwanja wa ndege wa Naha wa Okinawa. Huu ni msimu wa kilele wa watalii kwa kisiwa hicho. Dhoruba kali kama hizo ni nadra wakati huu wa mwaka huko Japani.

  9. Viongozi wa kijeshi wa Afrika Magharibi wakutana kuhusu mapinduzi ya Niger

    .

    Wakuu wa kijeshi kutoka kambi ya kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, wanakutana baadaye Jumatano katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, kujadili mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Niger wiki iliyopita.

    Jumuiya hiyo hapo awali ilionya kuwa inawapa watawala wapya wa Niger wiki moja kumrejesha madarakani Rais Mohamed Bazoum kabla ya kufikiria kutumia nguvu.

    Usiku, ndege ya kwanza kati ya tatu za Ufaransa iliyotumwa kuwahamisha raia wa Ulaya iliwasili Paris ikiwa na zaidi ya watu 250.

    Uhamisho huo unafanyika baada ya waandamanaji kushambulia ubalozi wa Ufaransa siku ya Jumapili.

    Italia pia imesafirisha raia wake kadhaa na pia wengine kutoka Ulaya, na raia mmoja wa Marekani.

    Serikali ya kijeshi imetangaza kufungua tena mipaka ya Niger na Algeria, Burkina Faso, Libya, Mali na Chad.

    Hata hivyo, mpaka wa Nigeria bado umefungwa.

    Soma zaidi:

    • Mapinduzi ya Niger: Raia wa Ulaya waliohamishwa Niger wawasili Paris na Roma
    • Mapinduzi Niger: 'Kwa nini naitaka Urusi na si Ufaransa'
    • Mapinduzi Niger: Makao makuu ya chama tawala yashambuliwa baada ya Rais Bazoum kuondolewa madarakani
    • Mapinduzi ya Niger: Viongozi wa Afrika Magharibi watishia kuingilia kijeshi
    • Mapinduzi ya Niger: EU yasitisha ushirikiano wa kiusalama na misaada ya kibajeti
    • Mapinduzi ya Niger: Rais Bazoum aonesha ukaidi baada ya kuondolewa madarakani
  10. Kulipia samaki kutumia ngono: Jinsi wanawake hawa nchini Kenya walivyojinasua kutoka mtego huu

    Kaunti ya Kisumu, Magharibi mwa Kenya, inajivunia juhudi zake za kubadilisha , tabia iliyokithiri miaka ya hapo awali iliyohusisha baadhi ya wanawake wanaofanya biashara ya kuuza Samaki kuuza miili yao kwa wavuvi ili kupata samaki wa kuuza badala ya kutumia pesa kama malipo ya kawaida .

    Elizabeth Atieno, ambaye alishiriki tabia hii inayofahamika kama ‘jaboya’ anasimullia mabadiliko makubwa ambayo yamefanyika baada ya wanawake wafanyabiashara wa samaki katika ufuo wa ziwa Victoria nchini Kenya kupata uhamasisho na kupunguza kutegemea wanaume kupata samaki ili kuendelea na biashara .Tazama

    Maelezo ya video, Kulipia samaki kutumia ngono:'Niliuza mwili wangu kwa wavuvi kupata samaki'
  11. Chelsea yaweza kumtoa Lesley Ugochukwu kwa mkopo baada ya kumsajili kwa miaka saba

    .

    Meneja Mauricio Pochettino anasema mchezaji mpya Lesley Ugochukwu huenda akatolewa kwa mkopo baada ya kiungo huyo kujiunga na Chelsea kwa euro 27m (£23.2m) kutoka Rennes.

    Ugochukwu amesaini mkataba wa miaka saba lakini Pochettino bado hajaamua mustakabali wa haraka wa Mfaransa huyo.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 amecheza mechi 47 za Ligue 1 akiwa na Rennes na pia ameshiriki Ligi ya Europa.

    "Tunahitaji kumpima atakapoanza mazoezi leo na kisha London baada ya kufanya ziara," alisema Pochettino.

    "Ni mchezaji mchanga, mwenye kipaji. Sasa ni wakati wa kumtathmini hadi mwisho wa dirisha la uhamisho na kuona kama atakuwa nasi au pengine kuna uwezekano wa kumtoa kwa mkopo."

    Ugochukwu, ambaye mpango wake una chaguo la mwaka mwingine, bado hajacheza kwa mara ya kwanza katika timu ya taifa ya Ufaransa lakini ameichezea Les Bleus katika viwango vya chini ya miaka 17, 18 na 19.

    Anaweza kurejea Ligue 1 kwa msimu ujao kwa sababu kundi la umiliki wa Blues lilinunua hisa nyingi katika klabu ya Alsace Strasbourg mwezi Juni.

    Chelsea imekuwa ikimwinda kiungo wa Brighton Moises Caicedo katika kipindi chote cha uhamisho wa wachezaji - huku dau la pauni milioni 80 lilikataliwa wiki iliyopita - na Pochettino amekuwa akitaka wachezaji wenye uzoefu zaidi kuongeza kwenye kikosi chake.

    Chelsea wana mkakati wa kusajili vipaji vya vijana wenye uwezo wa kuwa nyota wa siku za usoni huku wakiondoa kikosi chao kilichojaa baada ya kutumia pauni milioni 600 katika madirisha mawili yaliyopita.

    Kai Havertz, Mateo Kovacic na Mason Mount wote wameondoka msimu huu kwenda Arsenal, Manchester City na Manchester United mtawalia, huku N'Golo Kante, Kalidou Koulibaly na Edouard Mendy wakihamia Saudi Pro League.

    Ruben Loftus-Cheek na Christian Pulisic wote walihamia klabu ya AC Milan ya Italia, huku Conor Gallagher akipewa ofa ya pauni milioni 40 kutoka West Ham United.

    Chelsea tayari imewaongeza washambuliaji Christopher Nkunku na Nicolas Jackson kwenye kikosi chao pamoja na chipukizi wa Brazil Angelo Gabriel.

    Pia unaweza kusoma

    • Sadio Mane aondoka Bayern Munich kujiunga na Ronaldo Al-Nassr
    • Tetesi za Soka Ulaya Jumatano 02.08.2023
  12. Changamoto ya upatikanaji wa dola ya Marekani yaathiri bei ya mafuta Tanzania

    Ongezeko la zaidi ya shilingi 440 kwa mafuta ya petroli na zaidi ya shilingi 390 kwa mafuta dizeli jijini la Dar es Salaam

    Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania, EWURA, imetangaza bei mpya za mafuta ambazo zinaonesha, mafuta aina ya Petroli imepanda kwa shilingi 443 na dizeli ikipanda kwa shilingi 391 kwa kila lita moja kwa mafuta yanayouzwa katika jiji kuu la kibiashara Dar es Salaam. Hivyo bei ya lita moja katika kituo cha mafuta kswa Dar ni shilingi 3199 kwa petroli na shilingi 2935 kwa dizeli.

    EWURA imesema sababu ya mabadiliko hayo bei ambayo huanza kutumia kila jumatano ya kwanza ya mwezi ni tatizo la upatikanaji wa dola ya Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi, kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani, sababu nyingine ikiwa ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji wa bidhaa hiyo.

    Ongezeko la zaidi ya shilingi 440 kwa mafuta ya petroli na zaidi ya shilingi 390 kwa mafuta dizeli jijini la Dar es Salaam ndiyo la chini zaidi kulinganisha na maeneo mengine yaliyo mbali na bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara yanakoshushwa mafuta. Kwa mfano mji wa Bukoba mkoani Kagera ulio ubali wa zaidi ya kilomita 1400 kutoka Dar es Salaam lita moja ya mafuta petroli inauzwa shilingi 3415 kwa lita moja wakati dizeli ni shilingi 3151 kwa lita moja.

  13. Serikali ya Kenya yasitisha shughuli za Worldcoin ikitaja hofu za kiusalama

    th

    Serikali ya Kenya imesitisha shughuli zote zinazohusiana na mradi wa sarafu fiche za kidijitali wa WorldCoin.

    Waziri wa Usalama wa Ndani nchimi humo Kithure Kindiki amesema kupitia taarifa kwamba serikali ina wasiwasi kuhusu mradi huo tata ambao kufikia sasa umesajili maelfu ya Wakenya, na kwamba marufuku hiyo itaendelea kutekelezwa hadi mashirika husika yatakapothibitisha kutokuwepo kwa hatari yoyote ya kiusalama .

    “Vyombo husika vya usalama, huduma za kifedha na ulinzi wa data vimeanza uchunguzi ili kubaini ukweli na uhalali wa shughuli zilizotajwa hapo juu, usalama na ulinzi wa takwimu zinazokusanywa , na jinsi wahusika wanavyokusudia kutumia data,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

    "Zaidi ya hayo, itakuwa muhimu kwamba uthibitisho wa usalama wa umma na uadilifu wa miamala ya kifedha inayohusisha idadi kubwa ya raia utolewe kwa njia ya kuridhisha mapema."

    Kindiki aliongeza kuwa iwapo mtu yeyote atapatikana kusaidia au kujihusisha zaidi na shughuli hizo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

    Siku ya Jumanne, foleni ndefu zilishuhudiwa katika Jumba la (KICC) jijini Nairobi ambapo maelfu walimiminika kwa siku ya pili ili kujiandikisha kwa mradi huo, ambapo wanaruhusu kuchanganuliwa kwa data ya mboni zao za macho kwa tokeni maalum za sarafu za kidijitali zenye thamani ya shilingi 7,700

    Maafisa waliiomba timu ya Worldcoin kusitisha zoezi hilo na kuwatimua watu hao kutokana na kile walichosema ni hatari za kiusalama.Waliambia timu hiyo itafute uwanja mkubwa zaidi kama vile viwanja vya Nyayo au Kasarani.

    Kamishna wa Data Immaculate Kassait alisema tume hiyo inafanya tathmini yake kwa mchakato mzima wa Worldcoin ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria.

    Mradi huo wa Mkurugenzi Mtendaji wa OpenAI Sam Altman umekosolewa vikali kuhusu masuala ya usiri na usalama wa data.

    Unaweza pia kusoma

  14. Iran yatoa likizo ya siku mbili kutokana na joto kali

    .

    Iran imetangaza likizo ya siku mbili, Jumanne kwa wafanyikazi wa serikali na benki kutokana na hali ya joto inayoongezeka kote nchini humo.

    Uamuzi huo umewadia wakati nchi duniani kote, ikiwa ni pamoja na Iran, zinakabiliwa na ongezeko la joto la kihistoria na ambalo halijawahi kutokea.

    Ofisi ya hali ya hewa ya Iran ilitabiri joto linaweza kuwa kati ya nyuzi joto 40 na 50 katika miji mingi.

    Miji, ikiwa ni pamoja na majimbo ya Ilam, Bushehr na Khuzestan, imerekodi viwango vya joto kuongezeka zaidi ya nyuzi joto 45 hivi karibuni, kama ilivyoripotiwa na chombo cha habari cha Iran kinachomilikiwa na serikali, IRIB.

    Dehloran, mji ulioko magharibi mwa Iran, ulirekodi joto la juu zaidi la nyuzi joto 50 nchini Iran katika muda wa saa 24 zilizopita huku wizara ya afya ya Iran ikiendelea kutoa maonyo kuhusu kiharusi cha joto kutokana na kupigwa na jua kupita kiasi.

    Pia unaweza kusoma:

    • Hofu yatanda dunia ikikumbwa na joto kali zaidi kuwahi kutokea
  15. Mapinduzi ya Niger: Raia wa Ulaya waliohamishwa Niger wawasili Paris na Roma

    .
    Maelezo ya picha, Watu waliohamishwa kutoka Niger waliwasili katika uwanja wa ndege wa Paris Charles de Gaulle mapema asubuhi ya Jumatano

    Ndege zinazowahamisha Wazungu kutoka Niger zimewasili Ufaransa na Italia.

    Ufaransa ilianza kuwahamisha raia wake kutoka Niger huku kukiwa na chuki dhidi ya Wafaransa kufuatia mapinduzi ya wiki iliyopita – ambapo watu 262 waliwasili Paris mapema Jumatano.

    Mapinduzi hayo yamesababisha maandamano dhidi ya utawala wa kikoloni wa zamani, huku ubalozi wa Ufaransa ukishambuliwa.

    Hata hivyo, Ufaransa inasema haina mpango wa kuwarejesha nyumbani takriban wanajeshi 1,000 wa Ufaransa walioko humo kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu.

    Ujerumani imewataka raia wake kuchukua ofa ya Ufaransa kusaidia Wazungu wengine huku Italia ikipanga safari ya ndege ambayo iliwasili Roma baada tu ya 05:00 saa za eneo siku ya Jumatano na watu 87 waliohamishwa.

    Ndege hiyo ilikuwa imebeba Waitaliano 36, Wamarekani 21 na Mwingereza mmoja, kulingana na shirika la habari la Reuters.

    Juntas nchini Burkina Faso na Mali wameonya kuwa jaribio lolote la nguvu la kumrejesha madarakani rais aliyepinduliwa litaonekana kama tangazo la vita.

    Majirani hao wawili, pia koloni za zamani za Ufaransa, wote wameachana na Ufaransa na kukumbatia Urusi, baada ya kufanya mapinduzi yao wenyewe katika miaka ya hivi karibuni.

    Onyo lao linaashiria mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kuzidisha hali tete katika eneo linalopambana na wapiganaji wa Kiislamu.

    Niger, ambayo ina utajiri mkubwa wa madini ya uranium, imekuwa mshirika mkuu wa Magharibi katika vita dhidi ya itikadi kali za kijihadi katika eneo la Sahel.

    Ufaransa na Marekani zina kambi za kijeshi huko.

    Baada ya viongozi wa kijeshi wa Mali kuchagua kushirikiana na mamluki wa Wagner wa Urusi mwaka 2021, Ufaransa ilihamisha kitovu cha operesheni zake za kikanda za kukabiliana na ugaidi hadi Niger.

    Niger:

    Soma zaidi:

    • Mapinduzi Niger: 'Kwa nini naitaka Urusi na si Ufaransa'
    • Mapinduzi Niger: Makao makuu ya chama tawala yashambuliwa baada ya Rais Bazoum kuondolewa madarakani
    • Mapinduzi ya Niger: Viongozi wa Afrika Magharibi watishia kuingilia kijeshi
    • Mapinduzi ya Niger: EU yasitisha ushirikiano wa kiusalama na misaada ya kibajeti
    • Mapinduzi ya Niger: Rais Bazoum aonesha ukaidi baada ya kuondolewa madarakani
  16. Habari za hivi punde, Vita vya Ukraine: Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yanalenga vituo vya bandari ya Ukraine

    .
    Maelezo ya picha, Wazima moto katika mkoa wa Odesa (picha kutoka maktaba)

    Shambulizi la ndege zisizo na rubani za Urusi limepiga bandari ya Ukraine katika eneo la Izmail kwenye Mto Danube, umbali mfupi kutoka nchi wanachama wa Nato Romania.

    Ghala la nafaka na lifti ya kupakia nafaka ziliharibiwa. Takriban tani 40,000 za nafaka zilizokuwa zikipelekwa nchi za Afrika, China na Israel ziliharibiwa, Ukraine ilisema.

    Urusi ilianza kulenga bandari za Ukraine baada ya kuachana na makubaliano ya Umoja wa Mataifa yaliyowezesha usafirishaji wa nafaka salama kati ya nchi zote mbili katika Bahari Nyeusi.

    "Hizi ndizo bandari ambazo zimekuwa msingi wa usalama wa chakula duniani leo," waziri wa Ukraine Oleksandr Kubrakov alisema kwenye Twitter yake.

    Video, iliyorekodiwa kutoka upande wa Romania wa Danube takriban kilomita 3 (maili 1.9) , ilionyesha moto mkubwa ukiendelea katika eneo la bandari la Izmail mapema Jumatano.

    Rais wa Romania Klaus Lohannis alilaani kuendelea kwa mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya Ukraine "karibu na Romania" kuwa jambo lisilokubalika.

    Pia unaweza kusoma:

    • 'Ni kama kucheza na kifo' - askari wa kike wa mstari wa mbele Ukraine
  17. Canada yawa ya kwanza duniani kuchapisha maonyo kwa kila sigara

    .

    Canada itakuwa taifa la kwanza kuanza kuchapisha maonyo moja kwa moja kwenye sigara katika jitihada za kuwazuia vijana kuanza kuvuta sigara na kuwahimiza wengine kuacha.

    Maonyo hayo, ambayo yatakuwa kwa Kiingereza na Kifaransa, yatajumuisha misemo kama vile "Sigara husababisha saratani" na "Sumu kila unapovuta pumzi".

    Kanuni hizo mpya zitaanza kutekelezwa Jumanne.

    Kuanzia mwaka ujao, Wakanada wataanza kuona lebo mpya za onyo kwenye sigara.

    Kufikia Julai 2024 watengenezaji watalazimika kuhakikisha kuwa maonyo yanapatikana kwa sigara zote kubwa zinazouzwa, na kufikia Aprili 2025 sigara zote za ukubwa wa kawaida na sigara ndogo zilizo na karatasi na mirija lazima zijumuishe maonyo hayo.

    Maneno hayo yataonekana kwenye kichungi, ikijumuisha maonyo kuhusu kuwadhuru watoto, kuharibu viungo, kusababisha kutokuwa na nguvu za kiume na lukemia.

    Mnamo mwezi Mei, wizara ya afya ilisema kanuni mpya "itaifanya iwe vigumu kukwepa maonyo ya afya" kwenye bidhaa za tumbaku.

    Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Canada kupunguza matumizi ya tumbaku hadi chini ya 5% ifikapo mwaka 2035 na inafuatia muda wa siku 75 wa mashauriano ya umma ambao ulizinduliwa mwaka jana.

    Canada imehitaji uchapishaji wa lebo za onyo kwenye vifurushi vya sigara tangu 1989 na mwaka wa 2000 nchi hiyo ilipitisha mahitaji ya onyo ya picha kwa vifurushi vya bidhaa za tumbaku.

    Wizara ya afya ilisema inapanga kupanua maonyo kwa kuchapisha lebo za onyo zaidi ndani ya vifurushi vyenyewe, na kuanzisha jumbe mpya za onyo za nje.

    Matumizi ya tumbaku yanaendelea kuua Wakanada 48,000 kila mwaka.

    • Je wajua kuwa tumbaku ilikua ikitibu maradhi?
    • Tumbaku chanzo cha maradhi ya zinaa
  18. Sadio Mane aondoka Bayern Munich kujiunga na Ronaldo Al-Nassr

    .

    Mshambulizi wa zamani wa Liverpool Sadio Mane ameondoka Bayern Munich kujiunga na Cristiano Ronaldo katika klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alifunga mabao 12 katika mechi 38 alizoichezea Bayern katika msimu ambao haukuwa na matokeo ya kuridhisha licha ya awali kuonyesha kiwango kizuri cha mchezo.

    Mchezaji huyo wa Senegal pia alihusika katika ugomvi wa kimwili na Leroy Sane katika chumba cha kubadilishia nguo cha Manchester City baada ya kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa.

    Ripoti zinaonyesha kuwa mabingwa hao wa Ujerumani wamerudishiwa sehemu kubwa ya pauni milioni 35 walizolipa Liverpool kwa Mane mwaka mmoja uliopita.

    Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern, Jan-Christian Dreesen alisema mchezaji huyo wa zamani wa Southampton - ambaye amesaini mkataba wa miaka minne na Al-Nassr – "hakuwa na msimu rahisi" tangu kuhama kutoka Anfield.

    "Hakuwa na uwezo wa kuchangia kama sisi sote na yeye mwenyewe kama alivyotarajia," alisema Dreesen.

    Mapema Jumanne meneja wa Bayern Thomas Tuchel alisema yeye na Mane walikubaliana "ilikuwa umauzi bora zaidi kuhama".

    "Tulikumbatiana kwa muda mrefu na sote tulikubaliana kuwa hatupendi kinachotokea sasa, lakini tunafikiri ni uamuzi bora zaidi katika hali hii," alisema kocha wa Bayern.

    "Wakati mwingine mambo hayaendi jinsi kila mtu anavyotaka. Nimekuwa na uhusiano mzuri sana naye na hii itaendelea kusalia hivyo.

    "Naweza kuelewa kabisa anahisi kuumia na pia singefurahi ikiwa mambo kama haya yangetokea.

    "Ni wazi kwamba hatukuweza kutumia uwezo wote kamilifu, ambalo ni jukumu langu, lakini katika hali hii ilikuwa uamuzi bora zaidi kuondoka."

    Al-Nassr walimsajili Ronaldo mshindi mara tano wa Ballon d'Or mwezi Desemba na wamefuata mtindo huo msimu huu kwa kuwaongeza kiungo wa kati wa Croatia Marcelo Brozovic, beki wa pembeni wa Brazil Alex Telles na kiungo wa kati wa Ivory Coast Seko Fofana.

    Pia unaweza kusoma:

    • Tetesi za Soka Ulaya Jumatano 02.08.2023
  19. Trump ashtakiwa kwa jaribio la kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020

    .

    Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ameshtakiwa kwa makosa ya kupanga njama ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020.

    Anatuhumiwa kwa makosa manne, ikiwa ni pamoja na kula njama ya kulaghai Marekani, kuharibu ushahidi na kula njama dhidi ya haki za raia.

    Hati ya mashtaka inahitimisha uchunguzi wa matukio yanayohusu ghasia za Januari 6, 2021 katika Ikulu ya Marekani.

    Bw Trump, 77, ambaye anawania tena urais, anakanusha makosa hayo.

    Katika mitandao ya kijamii aliitaja kesi hiyo kuwa ya kipuuzi.

    Tayari ameshtakiwa katika kesi nyingine mbili: kwa kutunza vibaya faili zilizoainishwa, na kughushi rekodi za biashara ili kuficha malipo ya pesa aliyofanya kimya-kimya kwa nyota wa ponografia.

    Uchunguzi wa uchaguzi huo umezingatia hatua za Bw Trump katika kipindi cha miezi miwili kati ya kushindwa kwake na ghasia zilizotokea Washington DC, ambapo wafuasi wake walivamia Bunge la Congress huku wabunge wakiidhinisha ushindi wa Rais Joe Biden wa chama cha Democratic.

    Mwanamume anayeongoza uchunguzi huo, wakili maalum aliyeteuliwa na idara ya sheria ya Marekani Jack Smith, alisema Jumanne jioni: "Shambulio dhidi ya mji mkuu wa taifa letu mnamo Januari 6, 2021 lilikuwa shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya demokrasia ya Marekani."

    Kama ilivyoelezwa katika hati ya mashtaka ilichochewa na uwongo."

    Bw Smith alimalizia taarifa yake fupi kwa kuahidi mchakato wa "kushtakiwa kwa haraka", huku akisisitiza kwamba rais huyo wa zamani "lazima achukuliwe kuwa hana hatia hadi ithibitishwe kuwa na hatia".

    Bw Trump anatarajiwa kufika mahakamani siku ya Alhamisi mjini Washington DC.

    Hati ya mashitaka yenye kurasa 45 inaorodhesha washiriki sita ambao hawakutajwa majina: mawakili wanne, afisa wa idara ya haki na mshauri wa kisiasa.

    Hati hiyo ya mahakama inamshutumu Bw Trump kwa "njama ya kudhoofisha, kuzuia, na kushindwa kwa kazi ya serikali kuu kupitia ukosefu wa uaminifu, ulaghai na udanganyifu".

    Pia unaweza kusoma:

    • Je, Donald Trump anakabiliwa na mashtaka gani ya jinai kuhusu nyaraka za siri?
    • Mashitaka ya Donald Trump: Rais wa zamani wa Marekani kushtakiwa kwa kutoa pesa kununua kimya cha muigizaji wa filamu za utupu
    • ‘Trump alijua wafuasi wake walikuwa wamejihami na aliwataka wavamie bunge’
  20. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja 02/08/2023