Wasiwasi waongezeka, saa chache zikisalia kabla ya Ecowas kuchukua hatua za kijeshi
Wanajeshi wa Niger wana saa chache tu za kumrejesha madarakani Rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum la sivyo wakabiliane na uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi kutoka jumuiya ya kikanda ya Ecowas.
Moja kwa moja
Gari-moshi la abiria Pakistani laanguka na kuua watu 30

Chanzo cha picha, AFP
Takriban watu 30 wameuawa na wengine 100 kujeruhiwa wakati treni ilipoacha njia na kuanguka kusini mwa Pakistan, msemaji wa polisi amethibitisha.
Mabehewa kadhaa ya Hazara Express yalipinduka karibu na kituo cha reli cha Sahara huko Nawabshah, takriban kilomita 275 (maili 171) kutoka mji mkubwa zaidi wa Karachi.
Abiria waliojeruhiwa walipelekwa hospitali za karibu.
Vikundi vya uokoaji vinajaribu kuwakomboa watu kutoka kwenye mabaki ya treni.
Ajali kwenye mfumo wa reli ya zamani wa Pakistani sio kawaida.
Waziri wa Reli Saad Rafiq alisema uchunguzi wa awali ulionyesha treni hiyo ilikuwa ikisafiri kwa mwendo wa kawaida na wanajaribu kubaini kilichosababisha kuacha njia.
Msemaji wa shirika la reli huko Karachi alisema angalau mabehewa manane yalitoka kwenye njia.
Baadhi ya watu bado wamenasa ndani ya behewa la treni, kulingana na shirika la utangazaji la eneo hilo Geo.
Hali ya dharura imetangazwa katika hospitali kuu za Nawabshah na wilaya jirani za Sindh.
Video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha makumi ya watu wakiwa eneo la ajali, huku baadhi ya abiria wakitoka nje ya mabehewa yaliyopinduka.
Wasiwasi waongezeka, saa chache zikisalia kabla ya Ecowas kuchukua hatua za kijeshi

Chanzo cha picha, GIFT UFUOMA/BBC
Wanajeshi wa Niger wana saa chache tu za kumrejesha madarakani Rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum la sivyo wakabiliane na uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi kutoka jumuiya ya kikanda ya Ecowas.
Jumapili iliyopita, viongozi wa Afrika Magharibi waliwapa viongozi wa mapinduzi wiki moja kutekeleza matakwa yake au "itachukua hatua zote ... [ambazo] zinaweza kujumuisha matumizi ya nguvu".
Lakini katika nchi jirani ya Niger, Nigeria - ambako huenda idadi kubwa ya wanajeshi wakatoka - sauti dhidi ya kuhusika kwa jeshi zinazidi kuongezeka.
Nchi hizo mbili pia zina uhusiano wa karibu wa kikabila na kihistoria.
Siku ya Jumamosi, seneti ya Nigeria iliitaka serikali kuangalia "chaguo za kisiasa na kidiplomasia".
Na katika mji wa kaskazini wa Nigeria wa Sokoto unaopakana na Niger, ambayo ni nyumbani kwa kitengo cha 8 cha jeshi wasiwasi unaongezeka.
Upo kwenye makutano makubwa katika barabara inayoelekea Niger na kuna uwezekano kuwa mahali pa kukusanya wanajeshi kabla ya hatua zozote za kijeshi.
Mtengenezaji wa vito Sulaiman Ibrahim mwenye umri wa miaka hamsini na mmoja anaishi katika mojawapo ya maboma yenye uzio na milango.
Mmoja wa wake zake na baadhi ya watoto wake wako katika mji mkuu wa Niger, Niamey, wamekwama huko kwa sababu ya mapinduzi ya mwezi uliopita.
"Sasa nataka kumpigia simu mke wangu Fatima ili nisikie kutoka kwake, kwa sababu tangu siku ya mapinduzi hayo, sijasikia kutoka kwake," aliambia BBC, akishika simu yake katika mkono wake wa kushoto.
Anapitia anwani zake na kupiga tena nambari ya mke.
Kila simu inarudisha ujumbe ule ule: "Nambari unayopiga haipatikani kwa wakati huu."
“Kila nikipiga simu, hivi ndivyo wanavyoniambia, ama hakuna huduma na sijui,” anasema kwa uchungu na kushindwa kuficha wasiwasi wake.
"Ikiwa hatua za kijeshi zitachukuliwa dhidi ya Niger, hii italeta wasiwasi zaidi. Niko katika hali mbaya kwa sababu familia yangu haiko nami na sina taarifa zozote kuwahusu."
Soma zaidi:
'Mabachela' 70 waoa kwa pamoja Dar es Salaam

Chanzo cha picha, Tanzania
Ndoa 70 za vijana wasiokuwa na uwezo wa kutoa mahari zimefungwa leo kwa pamoja jijini Dar es Salaam katika moja ya matukio nadra kwa dini ya kiislamu nchini Tanzania katika miongo ya hivi karibuni.
Ndoa hizo zimefungwa kwenye ukumbi wa DYCCC, Chang'ombe na kushuhudiwa na maelfu ya watu pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Spika wa bunge la Tanzania, Mussa Azan Zungu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally
Mkurugenzi wa Taasisi iliyoratibu ndoa hizo, Al Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki amesema kilichowasukuma kuwasaidia vijana hao kwa kuwatolea mahali ni kutokana na gharama za ndoa kuwa juu kulinganisha na uwezo wa maisha yao...
"Tulipokea ujumbe zaidi ya 1000 baada ya kutangaza jambo hili mwezi wa nne, waliojaza fomu za kutaka kusaidiwa kuoa walikua zaidi ya 200 lakini baada ya usaili tumepata 70 ambao leo wameoa", alisema Kishki.
Moja ya vigezo muhimu vilivyotumika kuwapata vijana hao ni nia yao ya kuoa, uwezo wa kumudu ndoa na wale ambao hawaongezi mke wa pili.
Mbali na kupewa nasaha za uvumilivu kwenye ndoa kutoka kwa viongozi karibu wote walioshiriki, mmoja wa vijana aliyeoa leo, Ally Ismail Mwaluka, mlemavu pekee katika kundi la waliooa anasema ni ndoto iliyotimia.
"Sikutarajia, wakati mwaka unaanza sikua hata na ndoto ya kuoa, leo nmeoa bure na nimepata vitu vingine juu kutoka kwa viongozi wa serikali, bajaji, mafuta ya bajaji kwa mwaka mzima na fedha mbalimbali, sina cha kusema namshukuru Mungu", alisema Ally.
Vijana hao wametoka mikoa 12 ya Tanzania bara na Visiwani na mahari waliozosaidia zimegharimu shilingi zaidi ya milioni 70 za kitanzania.
Bado Taasisi ya Al Hikma Foundation haijaamua kama mpango huu wa kuwasaidia kuoa vijana wasio na mahari ni endelevu ama ni wa mpito, itaamua hilo baadae.
Tetemeko Uturuki: Mtoto aliyeokolewa kimuujiza kitovu chake kikiwa bado kimeshikana na mama yake yu buheri wa afya

Maelezo ya picha, Miezi sita baada ya kuokolewa, Afraa ni mzima wa afya na mwenye furaha Wakati Afraa alipopatikana kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka nchini Syria, kitovu chake kilikuwa bado kimeshikana na mama yake, ambaye alifariki baada tu ya kujifungua.
Video ya kuokolewa kwa mtoto kutoka kwa tetemeko la ardhi mnamo Februari ilivutia ulimwengu.
Tangu wakati huo amepata ahueni ya ajabu.
Leo, Afraa ana umri wa miezi sita - mtoto wa kawaida mwenye furaha, na afya tele.
Shangazi na mjomba wake wanamlea pamoja na watoto wao saba katika mji wa Jindayris nchini Syria, karibu na mpaka wa Uturuki.
"Yeye bado ni mdogo sana lakini ananikumbusha baba yake na dada yake Nawara, hasa tabasamu lake. Waliaga dunia katika tetemeko la ardhi pia," anasema mjomba wake, Khalil al-Sawadi, huku akiwa anacheza cheza ma mtoto huyo.
"Mara nyingi wangetumia wakati wetu. Yeye hatupi wakati mgumu hata kidogo.
Mnamo tarehe 6 Februari, tetemeko kubwa la ardhi lilitokea kusini-mashariki mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria, na kuua zaidi ya watu 44,000.
Mara tu baada ya tetemeko kubwa la ardhi kupiga Jindayris, mama yake Afraa alipata uchungu na kujifungua chini ya kifusi cha nyumba yake.
Na alifariki dunia kabla ya waokoaji kuwapata.
Mtoto Afraa alikuwa mwanafamilia pekee aliyesalimika - baba yake, Abu Rudaina, na ndugu zake wanne wote walifariki dunia, pamoja na mama yake.
"Tuliona nyumba ya Abu Rudaina ilikuwa imeanguka," anasema Khalil.
"Mke wangu alianza kupiga kelele: 'Ndugu yangu, kaka yangu'."
Khalil anakumbuka vizuri wakati alipomtoa Afraa kutoka chini ya kifusi: "Paa lilikuwa limewaangukia. Mtu mmoja alinipigia simu na kusema wamepata mwili wa mwanamke. Nilipofika tu nilianza kuchimba, kisha nikasikia sauti. Alikuwa mtoto Afraa wakati huo akiwa bado anashikamana na mama yake. Tulidhamiria kumuokoa, tulijua angekuwa kumbukumbu pekee iliyosalia ya familia yake."
Video ya kusisimua ya uokoaji wake ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii tena kasi.
Mtoto huyo alipelekwa hospitali na mwai alipewa jina la Aya, ambalo linamaanisha muujiza kwa Kiarabu.
Soma zaidi:
Mariupol: Warusi waanza kutafuta nyumba za bei nafuu katika mji wa Ukraine waliouteka

Ni mwaka mmoja tangu mji wa Mariupol wa Ukraine ulipoharibiwa kwa kiasi kikubwa na majeshi ya Urusi na kutekwa.
Sasa unabadilishwa na kuwasilishwa kama onyesho la utawala kutoka Urusi - na Warusi wengine hata wanatumai ya kununua nyumba huko.
Urusi ilidai kutwaa Mariupol, pamoja na maeneo mengine yote yanayokaliwa, kufuatia msururu wa kura za maoni ambazo zimeshutumiwa vikali kuwa ni za udanganyifu.
Takriban 90% ya majengo ya jiji hilo yaliharibiwa na makombora ya Urusi wakati wa kuzingirwa kwa miezi miwili.
Maelfu ya raia waliuawa na takriban watu 350,000 waliondoka, kati ya watu 430,000 kabla ya vita, kulingana na UN.
Sasa, mamlaka za uvamizi zinaonekana kuwa na dhamira ya "Kufanya jiji hilo kuwa la Urusi", kubadilisha alama za barabara za lugha ya Ukraine hadi za Kirusi, kuanzisha mtaala wa Kirusi shuleni na kushinikiza wakazi waliobaki kupata pasipoti za Kirusi.
BBC Verify imetumia picha za satelaiti kuweka ramani jinsi Urusi inavyounda upya jiji hilo.
Pia imegundua kuwa wakati maendeleo mapya yanaendelea, uharibifu mkubwa bado unaendelea - na imesikia kutoka kwa wakaazi waliobaki wale waliokuwepo kabla ya vita ambao wanahofia mustakabali usio na uhakika.
Pia unaweza kusoma:
- Vita vya Ukraine: Urusi yashambulia kituo cha utoaji damu - Zelensky
- Wakati ndege isio na rubani ya Ukraine iliposhambulia meli ya Urusi katika bahari nyeusi
- Vita vya Ukraine: Zijue boti zisizo na nahodha zinavyotumika
- Vita vya Ukraine: Vita visivyoonekana vya Ukraine vya kuzuia silaha za Urusi
- 'Ni kama kucheza na kifo' - askari wa kike wa mstari wa mbele Ukraine
US Classic: Simone Biles arejea kwa kishindo katika mashindano ya mazoezi ya viungo baada ya mapumziko ya miaka miwili

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mchezaji wa mazoezi ya viungo Simone Biles Bingwa mara nne wa Olimpiki Simone Biles amerejea kwa kishindo kwenye mashindano ya mazoezi ya viungo baada ya mapumziko ya miaka miwili.
Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 26 aliufurahisha umati wa watu wa Chicago kwa onyesho maridadi na kushinda US Classic katika hafla yake ya kwanza tangu Olimpiki ya Tokyo.
Biles alitangaza mnamo 2021 kuwa alikuwa akipumzika kufanyia kazi afya yake ya akili.
"Kila mtu ambaye alikuwa akishangilia - alitengeneza mabango, yote hayo kwenye umati - yaligusa moyo wangu kwamba bado wananiamini," Biles alisema.
"Inamaanisha ulimwengu mzima kwangu kwa sababu baada ya kila kitu kilichotokea Tokyo, nilijishughulikia sana.
"Bado mimi hufanya tiba kila wiki na imekuwa ya kusisimua sana kuja hapa na kuwa na ujasiri niliokuwa nao hapo awali.
Biles alipokelewa kwa shangwe katika Ukumbi wa Now Arena huko Hoffman Estates, Illinois, na akashinda kwa alama za pande zote pointi 59.100.
"Kila kitu kimeenda sawa. Najisikia vizuri sana kuhusu mahali nilipo sasa kiakili na kimwili," alisema.
"Bado nadhani kuna baadhi ya mambo ya kufanyia kazi katika utaratibu wangu lakini, kwa mara ya kwanza baada ya kurejea tena, naweza kusema ilikwenda vizuri. Nimeshtuka sana na kushangaa. Nina furaha sana sasa kwamba sasa inawezekana."
Soma zaidi:
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga atoa onyo kwa serikali ikiwa mazungumzo yatafeli maandamano yataanza tena

Chanzo cha picha, Reuters
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametoa uamuzi wake kwa serikali, Jumamosi, juu ya mazungumzo ya kumaliza mgogoro unaokumba Kenya kuhusiana na kupanda kwa gharama ya maisha.
Bwana Odinga alisisitiza umuhimu wa kufanya mazungumzo hayo bila masharati lakini pia akatoa onyo juu ya kushindwa kufanyika kwa mazungumzo hayo.
‘’Kushindwa kufikia makubaliano hadi Agosti 31, kutamaanisha kufanyika kwa maandamano zaidi’’, Raila alisema.
Bwana Odinga aliongeza kuwa wao kama wana Azimio wako tayari kuzungumza na wamewapa wenzao wa muungano wa Kenya Kwanza siku 30 kufanikisha mazungumzo hayo na ikiwa hayatakuwa yamefanyika kufikia wakati huo, atatoa amri nyingine.
Bwana Odinga alikubali mazungumza ya pande mbili yenye kujumuisha watu 5 kutoka kila upande huku upinzani ukiongozwa na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na serikali ikiongozwa na kiongozi wa walio wengi bungeni Kimani Ichung’wah katika kikao ambacho kitaongozwa na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo.
Jumanne, 25 Julai, Rais William Ruto alisema yuko tayari kukutana ana kwa ana kufanya mazungumzo na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ‘’wakati wowote’’.
Soma zaidi:
AfroBasket ya Wanawake: Nigeria wachukua ubingwa kwa mara ya 4 mfululizo

Nigeria wamekuwa mabingwa wa Afrika kwa mara ya nne mfululizo baada ya kuifunga Senegal katika mchezo wa fainali kwa pointi 84 kwa 74 katika uwanja kamili wa Kigali Arena katika mji mkuu wa Rwanda.
Nigeria imefikia rekodi ya Senegal ambayo ilishinda kombe hilo mara nne mfululizo kati ya 1970 na 1981.
Ifanya Okoro aliidondoshea Nigeria pointi 16 ili kumsaidia kocha wao Rena Wakama - kocha mkuu wa kike pekee mwaka huu - kuwa kocha wa kwanza wa kike kushinda ubingwa huu katika AfroBasket ya wanawake.
Nigeria inanyakua taji hilo baada ya kushinda michezo yote minne mjini Kigali, huku Amy Okonkwo akifanya vyema katika michuano hiyo ambaye pia anakuwa Mchezaji wa Thamani Zaidi.
Mlinzi wa uhakika Ciarra Dillard aliifungia Senegal pointi 19, lakini hii haikuwasaidia Simba kwenye vita hivi hadi kufikia kile ambacho kingekuwa taji lao la kumi na mbili.
Mapema leo Mali ilishinda nafasi ya tatu dhidi ya mwenyeji Rwanda.
"Ilikuwa mashindano makubwa, tulijaribu kadiri ya uwezo wetu, lakini hatukufaulu." Charlotte Umugwaneza, nahodha wa timu ya Rwanda aliwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo huo.

Maelezo ya picha, Kocha wa timu ya Nigeria Soma zaidi:
Mtoro wa Kiitaliano anaswa baada ya kuonekana kwenye picha akisherehekea ushindi wa Napoli

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Napoli ilishinda taji lao la kwanza la Serie A kwa miaka 33 mwezi wa Mei walipotoka sare na Udinese (Picha ya mechi kutoka maktaba) Mmoja wa watoro hatari zaidi wa Italia amenaswa eneo la Corfu baada ya kuonekana kwenye picha akishangilia timu yake ya soka kutoka mahali alipokuwa.
Vincenzo La Porta, 60, anafikiriwa kuwa na uhusiano wa karibu na genge la uhalifu wa kupangwa la Camorra huko Naples.
Amekuwa akitoroka kwa miaka 11 - lakini mapema mwaka huu alionekana kwenye picha ya mashabiki waliokuwa wakisherehekea nchini Ugiriki.
Polisi wa Naples Carabinieri walisema: "Kilichomsaliti ni mapenzi yake kwa soka hasa timu ya Napoli."
Maafisa walisema picha hizo zilipigwa baada ya Napoli kushinda ubingwa wake wa kwanza wa Italia katika zaidi ya miongo mitatu mapema mwaka huu.
"Kwa ushindi wa ubingwa, La Porta haikuweza kujizuia kusherehekea," polisi walisema.
La Porta tayari amehukumiwa bila kuwepo nchini Italia kwa kuhusishwa na uhalifu, kukwepa kulipa kodi na udanganyifu.
Hatimaye polisi walimkamata siku ya Ijumaa alipokuwa akiendesha gari lake kwenye kisiwa cha Ugiriki na sasa yuko jela akisubiri kurejeshwa nchini Italia.
Iwapo atarejeshwa nchini Italia, atatumikia kifungo cha miaka 14 na miezi minne jela.
Wakili wa La Porta aliliambia shirika la habari la AP: "Ameanzisha familia mpya nchini Ugiriki... Ana mvulana wa miaka tisa na anafanya kazi ya upishi ili kujikimu. Anasumbuliwa na maradhi ya moyo. Iwapo atarudishwa nyumbani, yeye na familia yake itaangamia."
Mamlaka hazikukata tamaa katika harakati zao za kumsaka La Porta, na walikuwa wakifuatilia kwa karibu mienendo yake ya kifedha na mtandaoni na "kungoja afanye makosa kidogo tu".
Mnamo mwezi Mei, La Porta hakuweza kuzuia furaha yake wakati Napoli iliposhinda taji lake la kwanza la Serie A baada ya miaka 33.
Polisi walimwona kwenye picha nje ya mkahawa wa Corfu miongoni mwa mashabiki wa Napoli akiwa amevalia kofia ya besiboli na kupeperusha bendera ya rangi za buluu na nyeupe za timu hiyo.
Wapelelezi walijua walikuwa na mtu wao wanayemsaka na wakamfuata hadi Ugiriki.
Kwa usaidizi mdogo kutoka kwa wenzao wa Ugiriki, walimkamata siku ya Ijumaa, polisi wa Ugiriki walisema.
Mnamo mwezi Januari mwaka huu, bosi wa mafia wa Italia ambaye alikuwa ametoroka kwa miongo kadhaa alikamatwa baada ya kuonekana kwa Ramani za Google.
Vita vya Ukraine: Urusi yashambulia kituo cha utoaji damu - Zelensky

Chanzo cha picha, Telegram/Volodymyr Zelensky
Maelezo ya picha, Rais Zelensky ameweka picha inayodaiwa kuonyesha kituo cha kutoa na tia damu cha Kupiansk kikiwaka moto baada ya shambulio la Urusi. Bomu la angani lililoongozwa na Urusi limeshambulia kituo cha damu kaskazini-mashariki mwa Ukraine, na kuua na kujeruhi raia, rais wa Ukraine amesema.
Volodymyr Zelensky amesema waokoaji sasa wanajaribu kukabiliana na moto baada ya shambulio hilo lililotokea eneo la Kupiansk katika mkoa wa Kharkiv Jumamosi usiku.
Urusi hadi sasa haijatoa maoni yoyote hadharani kuhusu shambulio hilo lililoripotiwa.
"Kushinda magaidi ni jambo la heshima kwa kila mtu anayethamini maisha," aliongeza.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii, Bw Zelensky aliwataja wahalifu hao kama "wanyama" ambao walikuwa wakitafuta "kuharibu kila kitu kinachoruhusu uhai".
"Uhalifu huu wa kivita pekee unasema kila kitu kuhusu uvamizi wa Urusi," alisema.
Hakusema ni watu wangapi wameuawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo.
Hata hivyo, BBC haijaweza kuthibitisha ripoti hiyo mara moja.
Hapo awali Urusi ilikanusha madai yote ya uhalifu wa kivita au kuwalenga raia.
Mji wa Kupiansk na makazi ya karibu yalitekwa na wanajeshi wa Urusi katika siku chache za kwanza za uvamizi wake nchini Ukraine, uliozinduliwa mnamo Februari 2022.
Eneo hilo lilikombolewa wakati wa shambulio la kushtukiza la Ukraine lililofanyika Septemba iliyopita.
Rais Zelensky pia alisema kuwa siku ya Jumamosi Urusi ilifanya shambulio jingine la kombora, ikilenga kampuni ya masuala ya angani inayoendeshwa na kundi la Motor Sich katika mkoa wa Khmelnytskyi magharibi.
Mashambulizi ya Urusi yanafanyika baada ya Moscow kuishutumu Ukraine kwa kuishambulia meli ya mafuta ya Urusi iliyokuwa na wafanyakazi 11 katika Bahari Nyeusi - shambulio la pili la ndege zisizo na rubani ndani ya siku nyingi.
Maafisa wa baharini wa Urusi walisema chumba cha injini ya meli ya mafuta ya Sig kiliharibiwa katika shambulio hilo kwenye Mlango Bahari wa Kerch na hakuna aliyejeruiwa.
Pia unaweza kusoma:
- Wakati ndege isio na rubani ya Ukraine iliposhambulia meli ya Urusi katika bahari nyeusi
- Vita vya Ukraine: Zijue boti zisizo na nahodha zinavyotumika
- Vita vya Ukraine: Vita visivyoonekana vya Ukraine vya kuzuia silaha za Urusi
- 'Ni kama kucheza na kifo' - askari wa kike wa mstari wa mbele Ukraine
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya leo 06/08/2023
