Takriban watu 500 wauawa katika shambulio la hospitali Gaza - maafisa wa Palestina
Msemaji wa jeshi la Israel anasema chanzo cha tukio hilo hakijajulikana na jeshi linachunguza undani wake
Moja kwa moja
Habari za hivi punde, Mabomu lazima yakome sasa - kiongozi wa kanisa la Israeli
Hospitali ya Al Ahli inafadhiliwa na Kanisa la Anglikana, na Richard Sewell, Mkuu wa Chuo cha St George's - mmoja wa viongozi wakuu wa kanisa huko Jerusalem - amechapisha kwenye X, zamani Twitter, kwamba hospitali ya Gaza "ilipata pigo moja kwa moja kutoka kwa kombora la Israeli”.
Anasema ripoti za awali zinaonyesha mamia ya wanawake na watoto wameuawa, na anakiita kitendo hicho "mauaji ya kimakusudi ya raia walio hatarini".
"Mabomu lazima yakome sasa. Hakuwezi kuwa na sababu inayowezekana kwa hili.
"Kama tulivyoripoti, jeshi la Israeli halijathibitisha kuwa vikosi vyao vilihusika na shambulio hilo.
Siku tatu za maombolezo zatangazwa Palestina kufuatia shambulio la hospitali
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ametangaza siku tatu za maombolezo kufuatia shambulizi la angani katika hospitali ya Al Ahli huko Gaza, vyombo vya habari vya serikali ya Palestina vinaripoti.
Kama tulivyoripoti hapo awali, Waisraeli walisema chanzo cha moto katika hospitali hiyo hakijabainika na kwamba wanajeshi wanachunguza.
Habari za hivi punde, Hamas imelitaja shambulio la hospitali huko Gaza kuwa uhalifu wa kivita
Ofisi ya vyombo vya habari ya serikali ya Hamas huko Gaza imetaja shambulio hilo dhidi ya hospitali ya Ukanda wa Gaza kuwa ni uhalifu wa kivita.
Katika taarifa, inaongeza: "Hospitali hiyo ilikuwa na makazi ya mamia ya wagonjwa na waliojeruhiwa, na watu walihamishwa kutoka kwa nyumba zao" kutokana na mashambulizi mengine.
Taarifa hiyo inasema "mamia ya waathiriwa bado wako chini ya vifusi".
Kama tulivyoripoti hapa chini, msemaji wa jeshi la Israeli hangethibitisha mara moja ikiwa vikosi vyake vilihusika. "Tutazingatia," alisema katika runinga.
Habari za hivi punde, Takriban watu 500 wauawa katika shambulio la hospitali - maafisa wa Palestina
Maelezo ya picha, Hii ni picha ya kwanza kutoka kwa tukio la shambulio linalodaiwa kufanywa katika hospitali moja huko Gaza
Idadi ya watu waliouawa imefikia 500 kufuatia madai ya shambulizi la anga dhidi ya hospitali - kulingana na msemaji wa wizara ya afya ya Gaza.
Wakati huo huo, msemaji wa jeshi la Israel anasema chanzo cha tukio hilo hakijajulikana na jeshi linachunguza undani wake.
BBC inajitahidi kuthibitisha maelezo ya tukio hilo.
Tayari picha zinazotoka katika hospitali ya Al Ahli Arab zinaonyesha matukio ya kutisha - huku watu waliojeruhiwa wakitolewa nje kwa machela gizani.
Miili na magari yaliyoharibiwa yanaonekana yakiwa kwenye barabara iliyojaa vifusi.
Video ambazo hazijathibitishwa zilionekana kuonyesha mlipuko mkubwa muda mfupi kabla.
Mamia ya watu waliokimbia makazi yao walikuwa wamejihifadhi katika ukumbi kwenye uwanja wa hospitali, kulingana na wenyeji.
Maafisa wa ulinzi wa raia wanasema mlipuko huo ulitokana na shambulizi la anga la Israel na kwamba mamia wamenasa kwenye vifusi.
Jeshi la Israel linasema linachunguza tukio hilo.
Daktari azungumzia kuhusu uharibifu mkubwa uliofanyika
BBC imefanikiwa kuzungumza na daktari ambaye jina lake halikutajwa anayefanya kazi katika hospitali hiyo ambayo imeshambuliwa katikati mwa Gaza.
Aliambia kipindi cha Newshour cha BBC World Service kwamba kulikuwa na uharibifu mkubwa katika eneo la shambulizi - ambapo watu 4,000 waliokimbia makazi walikuwa wakitafuta hifadhi.
Aliongeza kuwa asilimia 80 ya hospitali hiyo haina huduma, na kwamba mamia ya watu waliuawa au kujeruhiwa katika mlipuko huo.
Alisema hospitali hiyo ilikuwa tupu huku watu wakiendelea na shughuli ya kuwaokoa manusura wa shambulio hilo
Katika eneo la Khan Younis lenye msongamano watu 90 wanaishi katika nyumba moja
Chanzo cha picha, Ibrahim AlAagha
Familia ya Ibrahim imejaribu kuchukua jamaa na marafiki wengi kadiri wawezavyo.
Kuna watu 90 katika nyumba ya wazazi wake kwa sababu anasema familia yake haitamkataa mtu yeyote.
Kundi hili linajaribu kulala kwa zamu, watu wawili kwa kila godoro. Hakuna mtu anayeweza kupumzika kweli.
"Kutoka wakati tunaamka hadi wakati tunalala, tunajaribu tu kuishi."Ugavi wa chakula ni haba na waliopo hujaribu kwenda nje kila siku kuona iwapo chakula cha ufadhili kinagawanywa.
Kikundi kina maji na ngano ya kuoka mkate lakini bado haitoshi kwa zaidi ya mlo mmoja kwa siku. Ni ngumu kwa watoto - 10 kati yao ni chini ya miaka mitano.
"Kila mara wanaomba chakula na maji, na tunajaribu kuwapatia kadri tuwezavyo. Ni kidogo sana na ni vigumu sana.
"Namaanisha, sisi wazee, tunaweza kuvumilia kidogo, tunaweza kukaa na njaa, lakini watoto wanapouliza chakula hatuwezi kukataa.
"Mwanamke mjamzito na mzee mwenye kisukari ni miongoni mwa kundi lao, na Ibrahim anasema mwanamume huyo ana dawa za kutosha kwa siku kadhaa zaidi.
"Ikiwa chochote kibaya kitatokea kwa mtu yeyote, hakuna njia ambayo tutafika hospitalini sasa ... hilo ni jambo ambalo huwa na wasiwasi nalo."
Habari za hivi punde, Mkuu wa Ujasusi Israel ajitwika lawama la uvamizi wa Hamas
Zaidi ya Wapalestina 100 wameuawa katika mashambulizi ya angani kusini mwa Gaza, maafisa wanasema, huku jeshi la Israel likiendelea kulenga eneo hilo licha ya kuwaamuru raia kutorokea huko.
Wengi wa waliouawa waliripotiwa kukimbia makwao kaskazini mwa nchi kabla ya kile kinachotarajiwa kuwa mashambulizi makubwa ya ardhini dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hamas.Jeshi lilisema lilishambulia meneo Hamas kusini.
Pia kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu hali ya kibinadamu huko Gaza.
Marekani ilisema imekubali kuandaa mpango na Israel ambao utawezesha msaada kuwafikia raia katika eneo linalotawaliwa na Hamas, kwani mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yameonya kuwa mafuta ya hospitalini hayawezi kudumu kwa zaidi ya saa 24, huku maji yakiwa machache mno huku maduka yakisalia na chakula kichache .
Kumekuwa na matumaini ya kufungua kivuko cha Rafah cha Misri ili kuruhusu mizigo ya misaada inayohitajika haraka nao Wapalestina walio na hati za kusafiria pia wakiruhusiwa kuondoka.
Lakini shambulio la Israel liliripotiwa kuharibu jengo kwenye kivuko hicho siku ya Jumatatu.
Israel ilikata umeme na maji na kusitisha usafirishaji wa chakula na dawa kupitia vivuko vyake kujibu shambulio la kuvuka mpaka la wanamgambo wa Hamas tarehe 7 Oktoba ambapo takriban watu 1,300 waliuawa na wengine 199 kuchukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 2,800 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na maafisa wa afya.
Hakuna mpango wa kupeleka wanajeshi wa Marekani kupigana ardhini Israel - Marekani
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Joe Biden
Tunasikia baadhi ya habari za kwanza za Israel-Gaza kuhusu Marekani leo, huku Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin na msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa John Kirby wakizungumza kabla ya safari ya Joe Biden nchini Israel.
Austin alisema wanajeshi 2,000 wamewekwa kwenye "kujiandaa kupelekwa" agizo kwa Mashariki ya Kati - ikiwa hali itazorota hadi kiwango ambacho kitaonekana kuwa kibaya.
Lakini Ikulu ya Marekani imesisitiza kuwa haina nia ya kupeleka vikosi vya jeshi la Marekani katika ardhi ya Israel. Kupigana.
Agizo hilo linaruhusu tu wanajeshi "kujibu kwa haraka zaidi" mzozo huo, Austin aliwaambia waandishi wa habari mapema.Wakati huo huo, katika mahojiano na CNN, Kirby alisema kuandaa wanajeshi kwa ajili ya kupelekwa "ni sawa na kutoa onyo ".
Aliongeza: "Hakuna mipango au nia ya kupeleka wanajeshi wa Marekani kupambana nchini Israel.
"Inafikiriwa kuwa safari ya kesho ya Rais Joe Biden nchini Israel inalenga zaidi kuzuia vita hivyo kusambaa hadi kufikia mzozo mkubwa zaidi wa eneo la Mashariki ya Kati.
Miili 47 yapatikana katika ajali ya boti mto Kongo
Chanzo cha picha, Reuters
Miili 47 imeopolewa kutoka Mto Kongo huku juhudi za utafutaji na uokoaji zikiendelea kufuatia ajali ya boti wikendi iliopita, waziri mmoja amesema.
Marc Ekila, Waziri wa Uchukuzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alisema ajali ya boti ilisababishwa na mizigo kupita kiasi na kusafiri usiku, hatua ambayo ni kinyume na sheria.
Alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye televisheni Jumatatu usiku, siku mbili baada ya tukio hilo baya ambapo mashua ilipinduka.
Boti hiyo ilikuwa ikitoka mji wa magharibi wa Mbandaka kuelekea magharibi zaidi ndani ya eneo la msitu wa mvua wa DR Congo wakati tukio hilo lilipotokea.
Bw Ekila alisema uchunguzi unaendelea na wale waliohusika na tukio hilo watachukuliwa hatua.
Kwa sasa, mmiliki wa boti hiyo - ambaye hakuwa kwenye boti wakati ikipinduka - na nahodha wanaaminika kuwa pamoja.
Ilani ya abiria haikupatikana, hivyo basi katika hatua hii kushindwa kujua ni wangapi waliokuwemo na wangapi bado hawajapatikana.
Kulingana na waziri huyo, mwaka huu pekee kumeshuhudiwa matukio 88 kwenye maji ya DR Congo.
Nigeria yateketeza magamba ya kakakuona yenye thamani ya $1.4m
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Kakakuona
Nigeria imeteketeza magamba ya kakakuona yenye thamani ya $1.4m (£1.2m), maafisa wanasema.
Tangazo hilo linaadhimisha mara ya kwanza taifa hilo la Afrika Magharibi kuteketeza hadharani bidhaa za wanyamapori zilizokamatwa ili kuzuia usafirishaji haramu.
Kakakuona, mnyama mwenye haya na aliye katika hatari kubwa ya kuangamia, ni mmoja wa mamalia wanaosafirishwa zaidi duniani.
Magamba yao yanahitajika sana katika dawa za jadi za Kichina.Nigeria imekuwa kitovu kikuu cha kupitisha magamba ya mnyama huyo barani Afrika na bidhaa zingine za wanyamapori zinazosafirishwa kwenda Asia.
"Uharibifu wa vitu hivi vilivyokamatwa ni kauli yenye nguvu ya azimio letu la kulinda mazingira yetu, kuhifadhi wanyamapori wetu, na kupambana na biashara haramu ambayo inasababisha viumbe kufikia tishio la kuangamia," Aliyu Jauro, mkurugenzi mkuu wa Viwango vya Kitaifa vya Mazingira.
Wakala wa Udhibiti na Utekelezaji (NESREA) aliwaambia waandishi wa habari, na kuongeza kuwa magamba yalioharibiwa yalifikia uzani wa tani nne.
Afrika Kusini yazungumza na mkuu wa Hamas
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Afrika Kusini yazungumza na mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Afrika Kusini amezungumza na kiongozi wa Hamas ili "kujadili kupata msaada wa kibinadamu kwa Palestina", ofisi yake ilisema.
Baada ya kundi la wanamgambo wa Hamas kufanya shambulio baya dhidi ya Israel mwishoni mwa juma lililopita, jeshi la Israel limeizingira Gaza, eneo lenye wakazi wengi wa Palestina ambako Hamas inakaa.
Waziri wa Mambo ya Nje Naledi Pandor Jumanne alithibitisha kuwa aliwasiliana na mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh, kwa niaba ya serikali ya Afrika Kusini.Hamas, badala ya Afrika Kusini, ndiyo iliyoanzisha mazungumzo hayo, ofisi hiyo ilisema.
"Wakati wa wito huo, na kwa kuzingatia msimamo wa serikali, Waziri Pandor alisisitiza mshikamano na uungaji mkono wa Afrika Kusini kwa watu wa Palestina na alionyesha huzuni na masikitiko kwa kupoteza maisha ya watu wasio na hatia Wapalestina na Waisraeli," ilisema taarifa hiyo.
"Waziri Pandor na kiongozi wa Hamas walijadili jinsi ya kupata misaada muhimu ya kibinadamu Gaza na maeneo mengine ya ardhi za Palestina.
"Ofisi ya waziri huyo ilikanusha ripoti za shirika la habari la eneo hilo kwamba alionyesha kuunga mkono shambulio la Hamas dhidi ya Israel.
Afrika Kusini ni mojawapo ya nchi chache zilizothibitisha hadharani kuwa imekuwa na mazungumzo na Hamas tangu vita vilipoanza mwishoni mwa juma lililopita.
Habari za hivi punde, Ukraine 'yadai kuangusha helikopta 9 za Urusi huko Berdyansk na Luhansk'
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Ndege aina ya helikopter
Ukraine inasema kuwa imeharibu helikopta tisa za Urusi katika shambulizi la anga katika miji miwili ya mashariki mwa nchi inayokaliwa na Urusi.
Taarifa ya vikosi maalum ilisema mfumo wa ulinzi wa anga na vifaa vingine vilishambuliwa, pamoja na dampo la silaha, katika miji ya Berdyansk na Luhansk.
Makumi ya wanajeshi wa Urusi waliuawa au kujeruhiwa katika operesheni hiyo, iliongeza.Hakujakuwa na uthibitisho huru wa shambulio hilo, na hakuna maoni kutoka kwa jeshi la Urusi.
Vladimir Rogov, gavana aliyeteuliwa na Urusi wa sehemu inayokaliwa ya mkoa wa Zaporizhzhia, alisema mifumo ya ulinzi wa anga "ilifanikiwa kunasa makombora ya adui" juu ya Berdyansk, akiongeza kuwa habari kuhusu majeruhi na uharibifu ilikuwa ikikaguliwa na itatolewa baadaye.
Lakini video ambayo haijathibitishwa kwenye akaunti ya mtandao wa kijamii inayoiunga mkono Urusi - ambayo inasemekana kurekodiwa huko Berdyansk - inaonekana kuonyesha milipuko na roketi zinazoruka, huku sauti ikieleza kuwa dampo la risasi limeshambuliwa.
Mwanablogu mwingine wa Urusi ameandika kuhusu shambulio kwenye uwanja wa ndege kwa roketi za ATACMS zilizotengenezwa Marekani, na kusababisha kile mwandishi alichoeleza kuwa ni "pigo kubwa", na kupoteza watu na teknolojia.Jeshi la Ukraine lilisema shambulio la Berdyansk lilitokea saa 04:00 kwa saa za huko (01:00 GMT) na Luhansk saa 11:00 kwa saa za huko.
Berdyansk iko takriban 85km (maili 53) kutoka mstari wa mbele wa karibu wakati Luhansk iko karibu 100km.
Mapigano yameendelea kuripotiwa katika mstari wa mbele, ikiwa ni pamoja na karibu na miji inayoshikiliwa na Ukraine ya Avdiivka, Kupyansk na Lyman, ambayo imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi makubwa ya vikosi vya Urusi katika siku za hivi karibuni.
Huduma za dharura za Ukraine zimesema jengo la bweni limeharibiwa katika shambulizi la Urusi katika mji wa mashariki wa Sloviansk, huku watu wawili wakiaminika kukwama chini ya vifusi.
Huko Odesa, viongozi wanasema uchafu kutoka kwa ndege zisizo na rubani za Urusi ambazo zilidunguliwa zimeharibu kilabu cha mashua na boti kadhaa, lakini hakuna majeruhi.Ukraine imekuwa ikijaribu kurudisha eneo linalokaliwa na Urusi mashariki na kusini mwa nchi hiyo kupitia makabiliano makubwa, lakini hadi sasa ihaijapiga hatua kubwa .
Pia imefanya mashambulizi ya angani ya mara kwa mara kwenye maeneo ya Urusi huku ikilenga kudhoofisha juhudi za vita za Moscow.
Urusi pia imekuwa ikishambulia maeneo ya Ukraine mashariki karibu na Avdiivka na Kupyansk, lakini kulingana na ripoti za Ukraine imepata hasara kubwa katika siku za hivi karibuni.
Habari za hivi punde, Tupatieni ruhusa ya kuingia Gaza ili kuwasaidia watu 11,000 waliojeruhiwa - WHO
Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Afya Duniani WHO linasema linahitaji kuingia kwa haraka Gaza ili kutoa misaada na vifaa vya matibabu, huku likionya kuhusu janga la muda mrefu la kibinadamu.
Takriban nusu ya Wapalestina 2,800 waliouawa ni wanawake na watoto huku watu 11,000 wakijeruhiwa katika eneo la Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel kufuatia mashambulizi mabaya ya Hamas, maafisa kutoka WHO walisema katika taarifa fupi iliyoripotiwa na shirika la habari la Reuters.
Shirika la Umoja wa Mataifa linakutana na "wafanya maamuzi" leo kufungua njia ya kuelekea Gaza haraka iwezekanavyo - kwa sasa hakuna njia ya kuingia au kutoka.
Maafisa walisema kumekuwa na mashambulizi 115 kwenye vituo vya huduma za afya na hospitali nyingi huko Gaza hazifanyi kazi, huku maji na umeme vikiwa vichache.
"Wasiwasi juu ya upungufu wa maji mwilini na magonjwa yanayosababishwa na maji ni mkubwa kutokana na kuporomoka kwa huduma za maji na vyoo," shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA lilisema katika taarifa yake. "Watu wataanza kufa bila maji."
Tazama video: Mlipuko wakumba kivuko cha Rafah kati ya Gaza na Misri
Maelezo ya video, Mzozo wa Israel - Gaza: Mlipuko wakumba kivuko cha Rafah kati ya Gaza na Misri
Picha
za CCTV ambazo zimethibitishwa na BBC baada ya kurushwa hewani na kituo cha
habari cha Misri, zinaonekana kuonyesha wakati shambulizi la angani lilipiga
eneo la kivuko cha Rafah kati ya Gaza na Misri.
Kiwango
cha uharibifu hakijajulikana na hakuna ripoti za majeruhi.
Wapalestina
wamekuwa wakikusanyika katika kivuko cha mpaka cha Rafah na Misri kusini mwa
Ukanda wa Gaza kwa matumaini ya kuondoka kabla ya mashambulizi ya ardhini ya Israel.
Siku ya
Jumatatu, umati wa watu ulikusanyika kwenye kivuko kufuatia ripoti kwamba
kitafunguliwa tena kwa muda wakati wa usitishwaji wa mapigano, lakini hakikufunguliwa
tena.
Mwandishi wa habari wa Runinga Somalia auawa katika shambulio la kujitoa mhanga
Chanzo cha picha, SOMALI CABLE TELEVISION/FACEBOOK
Maelezo ya picha, Abdifatah Moalim Nur aliwahi kupokea vitisho siku za nyuma, waandishi wenzake wanasema
Risala za rambirambi zimetolewa kwa mwandishi wa habari maarufu wa TV ya Somalia baada ya kuuawa katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga katika mgahawa mmoja katika mji mkuu, Mogadishu.
Abdifatah Moalim Nur, maarufu kama Qeys, alielezewa na wenzake kama mtu "wa kipekee" na "mwenye ushawishi.
Anakuwa mwanahabari wa kwanza kuuawa nchini Somalia mwaka huu, kulingana na shirika la uangalizi wa vyombo vya habari nchini humo.
Kundi la wanamgambo wenye uhusiano na al-Qaeda, al-Shabab, lilisema lilifanya shambulio la kujitoa mhanga katika mgahawa wa Blue Sky.
Polisi walisema watu wengine wanne walijeruhiwa nje ya mgahawa huo ambao uko karibu na ikulu ya rais.
Muungano wa Kitaifa wa Waandishi wa Habari wa Somalia (NUSOJ) ulisema "umetikiswa sana" na mauaji ya "kipumbavu na ya kikatili" ya Nur, mkurugenzi wa Televisheni ya kibinafsi ya Somali Cable.
"Kazi yake ya ajabu na kujitolea kwake kumeacha alama isiyofutika katika uandishi wa habari wa Somalia, na kuwatia moyo waandishi wengi wachanga kujitahidi kwa ubora," umoja huo ulisema.
Nur, mtetezi mkuu wa uhuru wa vyombo vya habari, hapo awali alikabiliwa na vitisho, Shirika la Wanahabari wa Somalia (SJS), lilisema.
Mwezi Oktoba mwaka jana, mwanahabari Mohamed Isse Hassan alikuwa miongoni mwa zaidi ya watu 100 waliouawa katika milipuko miwili ya magari mjini Mogadishu.
Mwezi mmoja kabla, ripota wa Televisheni ya Taifa ya Somalia inayomilikiwa na serikali, Ahmed Mohamed Shukur, aliuawa na bomu lililotegwa ardhini karibu na mji mkuu.
Tazama Video: Roketi zarushwa juu ya anga ya mji mkuu wa Israel Tel Aviv huku watu wakikimbilia hifadhi
Maelezo ya video, Mzozo wa Israel - Gaza: Makombora ya roketi kutoka Gaza yaonekana juu ya mji mkuu wa Israel Tel Aviv huku ving'ora vikisikika
Raia wa Israel katika mji mkuu wa Tel Aviv walionekana wakikimbilia hifadhi baada ya ving'ora vya onyo kusikika.
Hamas ilisema imerusha "msururu wa makombora" juu ya mji mkuu wa Tel Aviv na Jerusalem.
Katika picha zilizoonekana kwenye mitandao ya kijamii, roketi zilionekana angani juu ya mji huo.
Ni tukio la hivi karibuni katika kuongezeka kwa mvutano kati ya Israel na Hamas.
Mapema siku hiyo, video iliyochambuliwa na BBC ilionekana kuonyesha shambulizi la anga kwenye kivuko cha Rafah kwenye mpaka wa Misri, ambapo ilitarajiwa usitishaji mapigano ungefanyika kwa raia wa Gaza na wale wa kigeni kuondolewa.
Eneo lote la mashariki ya kati linakaribia kutumbukia kwenye shimo - Mfalme wa Jordan
Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Mfalme Abdalla II wa Jordan
Jordan, ambayo inapakana na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Israel na ina idadi kubwa ya Wapalestina, inatazama mzozo wa sasa kwa wasiwasi mkubwa.
"Eneo zima liko kwenye ukingo wa kutumbukia shimoni," Mfalme Abdullah II wa Jordan ameonya akiwa ziarani Berlin.
Amekuwa akifanya mazungumzo na Kansela Olaf Scholz kabla ya kiongozi wa Ujerumani mwenyewe kuelekea Israel.
Mfalme Abdullah II, ambaye ana mamlaka makubwa kama mfalme wa Jordan, alisema tishio la kuongezeka kwa vita ni "halisi".
Pia alionya dhidi ya kujaribu "kuwasukuma" wakimbizi wa Kipalestina kuingia Misri au Jordan.
"Huo ni mstari mwekundu, kwa sababu nadhani huo ni mpango wa... washukiwa wa kawaida kujaribu kuzua masuala mengine."
Video inaogofya: Mtu aliye na bunduki awafyatulia watu risasi kiholela mtaani
Maelezo ya video, Ufyatulianaji wa risasi mjini Brussels Wakati mshambuliaji alipowafyatulia raia risasi mtaani
Mtu mwenye silaha mjini Brussels amewaua kwa kuwapiga
risasi raia wawili wa Uswidi na kumjeruhi mtu wa tatu.
Waendesha mashtaka wanachukulia tukio hilo kuwa la
kigaidi, na Jumanne waliripoti kwamba polisi walimpiga risasi mtu mmoja katika
msako mkubwa wa kumtafuta mtu aliye na bunduki.
Huu ndio wakati mtu huyo anaonekana kufyatua risasi
katika barabara ya mji mkuu wa Ubelgiji.
Mahakama ya Juu zaidi nchini India yakataa kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja
Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama ya
Juu ya India imekataa kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja, ikisema haina
uwezo wa kufanya hivyo.
Badala yake,
ilikubali ombi la serikali la kuunda jopo litakalozingatia kutoa haki na manufaa
ya kijamii na kisheria kwa wapenzi wa jinsia moja.
Mahakama
ilikuwa imesikiliza maombi 21 mwezi Aprili na Mei kutoka kwa wapenzi wa jinsia
moja na wanaharakati ambao walisema kutoweza kuoa kuliwafanya kuwa "raia
wa daraja la pili".
Uamuzi huo
utakatiza matumaini ya watu wa LGBTQ+ nchini India, wanaoaminika kuwa katika
makumi ya mamilioni.
Serikali na
viongozi wa kidini walikuwa wamepinga vikali vyama vya watu wa jinsia moja
wakisema vinapingana na utamaduni wa Wahindi.
Pia unaweza kusoma:
LGBTQ: 'Nilipogundua kijana wangu amebadili jinsia, nilifikiria kujiua lakini ...'
Mzozo wa Israel-Gaza:Kinachoendelea kwa sasa
Chanzo cha picha, EPA
Ikiwa unajiunga nasi au unahitaji muhtasari wa haraka, haya ndio matukio unayohitaji kujua.
Biden nchini Israel:Rais wa Marekani Joe Biden amethibitisha kuwa atazuru Israel kesho, kabla ya kuelekea Jordan ambako atakutana na maafisa akiwemo Mahmoud Abbas wa Palestina.
Onyo kutoka Iran:Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Israel haitaruhusiwa kuchukua hatua katika Ukanda wa Gaza bila matokeo - na kuonya"hatua za mapema"katika saa zijazo.
Mashambulizi ya usiku wa manane:Zaidi ya watu 100 waliuawa jana usiku kufuatia shambulio la nyumba huko Rafah na Khan Younis kusini mwa Gaza, maafisa wa eneo hilo wanasema.(Wakazi wengi wa Gaza wamekimbilia huko baada ya serikali ya Israel kuwaambia wahamie kusini.)
Wengi bado wako kaskazini mwa Gaza:Katika taarifa yake ya kila siku kuhusu vita, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel Jonathan Conricus alisema karibu watu 600,000 hadi sasa wamekimbia kaskazini mwa Gaza - kabla ya mashambulizi ya ardhini - lakini akaonya "laki chache"bado wamesalia.Aliwahimiza kufanya jambo la "salama" na kuondoka.
Hali ya Gaza inazidi kuwa mbaya:Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina limezidiwa nguvu baada ya kuhamisha shughuli zake hadi kwenye ghala kusini mwa Gaza, limesema.Kumekuwa na matumaini ya kufungua kivuko cha Rafah cha Misri kwenye mpaka wa kusini wa Gaza - kuruhusu mizigo ya lori kuingia - lakini hadi sasa haijafanyika.
Korea Kaskazini inaweza kuwa ilitoa silaha zilizotumika katika shambulio la Hamas – Korea Kusini
Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la
Korea Kusini linasema limekuwa likifuatilia ishara kwamba Korea Kaskazini
iliipatia Hamas silaha zilizotumiwa katika shambulio lake dhidi ya Israel.
“Tunaendelea
kuona ushahidi kuwa Korea Kaskazini imekuwa ikisafirisha silaha mbalimbali
katika nchi za Mashariki ya Kati na makundi ya wapiganaji, ikiwa ni pamoja na
ugunduzi wa hivi karibuni wa makombora ya milimita 122 yaliyotengenezwa na
Korea Kaskazini karibu na mpaka wa Israel, ambayo yanaaminika kutumiwa wanamgambo
wanaounga mkono kikamilifu Hamas au wanaoshirikiana na Hamas," afisa mmoja
wa kijeshi alisema katika mkutano na waandishi wa habari wa ndani.
Afisa huyo
pia alipendekeza kuwa mbinu ya Hamas ya kuvamia kwa njia ya kupaa kwa mwavuli inaweza
kuwa ilianzia Korea Kaskazini, akiashiria mafunzo ya utawala yaliyoimarishwa ya
kupenyeza kwenye anga hewa kwa kutumia miavuli maalum.