Vifaru vya Israel vyaonekana nje ya hospitali, huku vikosi vikiingia zaidi katika mji wa Gaza
Kanda za video zinaonyesha vifaru nje ya kituo cha watoto cha Al-Rantisi huku milipuko ikiripotiwa karibu na hospitali nyingine muhimu.
Moja kwa moja
Paul Mackenzie apatikana na hatia ya kuendesha studio haramu ya filamu

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Paul Mackenzie amekuwa akizuiliwa tangu kukamatwa mwezi Aprili Paul Mackenzie, Mkenya anayetuhumiwa kuongoza dhehebu lenye utata na kuhusika na vifo vya zaidi ya watu 400, amepatikana na hatia kwa mashtaka tofauti.
Mahakama ya Malindi pwani ya Kenya ilimtia hatiani kwa kuendesha kinyume cha sheria studio ya filamu inayohusishwa na mahubiri yake na kusambaza filamu bila leseni halali.
Baadhi ya mahubiri yake bado yanapatikana mtandaoni.
Hakimu, hata hivyo, alimwachilia huru kwa kosa la kuwachochea watoto dhidi ya kwenda shule.
Mackenzie anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitano au kulipa faini.
Hukumu imepangwa kutolewa mwezi ujao.
Mackenzie hajafunguliwa mashtaka rasmi kuhusiana na vifo vya mamia ya watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wake, licha ya kuwa kizuizini tangu Aprili
Kupatikana kwa miili hiyo katika makaburi ya halaiki msituni kulishtua Wakenya mapema mwaka huu.
Maelezo zaidi:
Watu wawili wajeruhiwa baada ya Hamas kurusha makombora katika mji wa Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanawake wawili wamejeruhiwa mjini Tel Aviv baada ya wapiganaji wa Hamas ilipkufanya kurusha msururu mpya wa roketi katika mji huo wa Israel, kulingana na ripoti.
"King'ora kililia karibu saa mbili asubuhi mjini Tel Aviv. Kuna sehemu mbili ambazo (zilipigwa) na roketi," shirika la habari la Reuters lilimnukuu mhudumu wa afya akisema.
"Mwanamke alijeruhiwa kwenye paja akiwa alindani ya gari lake."
Hamas inasema mashambulizi ya hivi punde ni jibu la kuongezeka kwa vifo vya raia huko Gaza.
Jeshi la Israel linasema kuwa makombora 9,500, roketi na ndege zisizo na rubani zimerushwa dhidi ya Israel kutoka Gaza na maeneo mengine tangu tarehe 7 Oktoba.
Asilimia 12 ya makombora yaliyorushwa kutoka ndani ya Gaza yameanguka ndani ya ardhi ya Palestina, jeshi linasema.
Unaweza pia kusoma
Mafuriko ya Afrika Mashariki yanatokea mara moja katika karne - UN

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Picha hii ya Alhamisi inaonyesha mafuriko yakiendelea katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu Umoja wa Mataifa umetaja mafuriko ambayo yameathiri maelfu ya watu nchini Somalia na nchi jirani za Afrika Mashariki kuwa ni tukio la mara moja katika karne.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa walisema zaidi ya watu milioni 1.5 nchini Somalia wanaweza kuathiriwa na mvua kubwa ya msimu, ambayo imefanywa kuwa mbaya zaidi kutokana na athari za pamoja za matukio mawili ya hali ya hewa - athari ya El Niño na Dipole ya Bahari ya Hindi.
Mvua kubwa iliyoanza mapema Oktoba ilifuatia miezi kadhaa ya ukame mkali katika eneo hilo.
Zaidi ya watu 300,000 wamelazimika kkuyahama makazi yao nchini Somalia huku miji na vijiji vikukumbwa na mafurika kaskazini mwa Kenya.
Vifaru vya Israel vyaonekana nje ya hospitali ya watoto mjini Gaza
Hapo awali kidogo, tulielezea hali ilivyo katika au karibu na hospitali tatu kaskazini mwa Ukanda wa Gaza: Al-Shifa, Al-Quds na Hospitali ya Indonesia.
Taarifa za hivi punde zinasema vifaro vya Israel zimeonekana nje ya nje ya Hospitali ya Watoto ya Al-Rantisi katika Jiji la Gaza.
Walioshuhudia wameiambia BBC kwamba wanajeshi wa Israel wanatumia vipaza sauti kuamuru mtu yeyote ndani ya hospitali ya watoto, ambaye si mhudumu wa afya au mgonjwa, kuondoka.
Hali katika hospitali ya Al-Shifa ni ngumu kwa mtazamo wa kibinadamu lakini kwa mtazamo wa kijeshi, Israel imesemama kidete kuhusu kile watakachofanya: kuchukua hatua.
Israel imesema mara kwa mara kuwa inalenga mtandao wa mahandaki ya Hamas yaliyojengwa chini ya Ukanda wa Gaza - ambayo baadhi yake, kwa mujibu wa Vikosi vya Ulinzi vya Israel, viko chini ya hospitali.
Waendesha mashtaka wa Burundi wataka Waziri Mkuu wa zamani afungwe maisha jela

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Bw Bunyoni alikanusha mashtaka yote na kuomba aachiliwe kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi dhidi yake. Waendesha mashtaka nchini Burundi wanataka Waziri Mkuu wa zamani Alain-Guillaume Bunyoni, ambaye anakabiliwa na mashtaka saba, ikiwa ni pamoja na kutumia uchawi kutishia maisha ya rais ahukumiwe kifungo cha maisha jela.
Kesi ya Bw Bunyoni ilianza kusikizwa Septemba, mwaka mmoja baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kumfuta kazi kwa tuhuma za kupanga "mapinduzi" dhidi yake.
Bw Bunyoni pia anadaiwa kuhujumu usalama wa taifa, kuharibu taasisi za serikali, kuyumbisha uchumi na kujitajirisha kwa njia zisizo halali
Bw Bunyoni alikanusha mashtaka yote na kuomba aachiliwe kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi dhidi yake.
Mwendesha mashtaka Jean-Bosco Bucumi pia alimtaka Bw Bunyoni alipe "uharibifu sawa na mara mbili ya thamani ya nyumba 153 na viwanja 153 na magari 43 anayomiliki", pamoja na faini ya faranga za Burundi milioni 7.1 ($2,400; 2,000), shirika la habari la AFP liliripoti.
Wayahudi wahofia usalama wao huku uungaji mkono wa Wajerumani kwa Israel ukikabiliwa na changamoto mitaani

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Baadhi ya Wayahudi nchini Ujerumani wanasema wanalazimika kuficha utambulisho wao kwa kuhofia usalama wao. Kansela Olaf Scholz anasema "anafedheheka na kughadhabishwa" na mashambulizi ya chuki ya hivi majuzi dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.
Uungaji mkono wa kidiplomasia wa mji mkuu wa Ujerumani kwa Israeli mara nyingi huelezewa kama suala la jukumu la kihistoria.
Lakini, huku mapigano yakiendelea kati ya Israel na Hamas, mifarakano ya kijamii inaibuka nchini Ujerumani.
Hofu kuhusu kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi, tangu kuzuka kwa uhasama kati ya Hamas na Israel, imeenea kote Ulaya.
Kwa Ujerumani, matukio kama vile ya kurushwa kwa mabomu mawili ya petroli kuelekea kwenye sinagogi la Berlin mnamo Oktoba yanazua wasiwasi mkubwa kuhusu zama za Wanazi.
Unaweza pia kusoma
Watu 700 waliuawa katika mapigano ya Darfur - shirika la Umoja wa Mataifa
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Kalkidan Yibeltal
- Nafasi, BBC News

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji linasema takriban watu 700 waliuawa katika eneo la Darfur Magharibi mwa Sudan kufuatia mapigano kati ya jeshi na vikosi hasimu vya RSF.
Kisa hicho kilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita huko El Geneina ambapo watu wengine 300 wanaripotiwa kutoweka.
Shirika la haki za binadamu la eneo hilo linakadiria kuwa watu 1,300 waliuawa huko Darfur Magharibi tangu Ijumaa iliyopita na inalaumu RSF kwa ukatili huo.
Haya yanajiri huku RSF ikionekana kuongeza kasi ya mashambulizi katika kanda hiyo.
Mashahidi wanashutumu kundi hilo la wanamgambo na washirika wake kwa kuwalenga watu wasio Waarabu katika maeneo ambayo imeteka.
Shirika la Roots Organization for Human Rights and Violions Monitoring, kundi linalotetea haki za binadamu huko Darfur Magharibi, linaituhumu RSF kwa kuvamia kambi za wwakimbizi na kuanzisha mashambulizi.
RSF hapo awali ilikanusha shutuma hizo.
Kulingana na mashirika ya misaada maelfu ya watu wamekimbilia nchi jirani ya Chad katika siku za hivi karibuni.
Zaidi ya watu milioni tano na nusu wanakadiriwa kufurushwa katika makazi yao tangu ghasia kati ya RSF na Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan kuanza mwezi Aprili.
Maelezo zaidi:
Bado hakuna dalili ya kusitishwa kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza
Hakuna ripoti za moja kwa moja zinazoashiria kusitishwa kwa mapigano kaskazini mwa Gaza, licha ya Marekani kusema janondoka.
Jeshi la Israel linasema kutakuwa na "mapumziko ya kimkakati kwa ajili ya kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu"... lakini "hakuna usitishaji wa mapigano".
Wakati huo huo, Cogat, kitengo cha Wizara ya Ulinzi ya Israel, inasema njia ya uokoaji imefunguliwa kwa ajili ya raia kuhama kutoka kaskazini mwa Gaza, ambayo ndiyo kitovu cha mashambulizi ya Israel dhidi ya Hamas.
Katika chapisho kwenye mtandao wa X, zamani ikijulikana kama Twitter ilisema "maelfu ya watu wa Gaza" walikuwa wakihamia kusini mwa Gaza "kwa usalama wao".
Ukanda wa uokoaji utakuwa wazi kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi jioni ya leo, iliongeza.
Wapalestina wameonekana wakitembea katika mitaa ya mji wa Gaza asubuhi ya leo, wengine wakiwa wamebeba bendera nyeupe.
Marekani yaidhinisha chanjo ya kwanza duniani ya chikungunya

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka inayosimamia Chakula na Dawa nchini Marekani umeidhinisha chanjo ya kwanza duniani ya ugonjwa wa chikungunya, ambao inaiona kama "tishio la afya duniani".
Ugonjwa huu unaoenezwa na mbu husababisha homa na maumivu ya viungo na unaweza kuwa mbaya kwa watoto wachanga.
Uidhinishaji wa FDA unatarajiwa kuharakisha utolewaji wa chanjo hiyo kimataifa.
Mwaka huu, takriban watu 440,000 waliambukizwa chikungunya, huku 350, wakiripotiwa kufariki kufikia Septemba.
Kwa sasa hakuna dawa maalum ya kutibu chikungunya.
Amerika Kusini na Asia Kusini zimeshuhudia idadi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa huo mwaka huu
Chanjo hiyo inayojulikana kama Ixchiq imeidhinishwa kwa wale walio na umri wa miaka 18 na zaidi na wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo, FDA ilisema Ijumaa.
Iliundwa na Valneva ya Ulaya na itatolewa kupitia njia ya sindano moja.
"Kuambukiza virusi vya chikungunya kunaweza kusababisha ugonjwa mbaya na shida za kiafya za muda mrefu, haswa kwa wazee na watu walio na matatizo mengine ya kiafya," afisa mkuu wa FDA Peter Marks alisema.
Dire Tladi wa Afrika Kusini achaguliwa kuwa katika mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa

Chanzo cha picha, Chuo Kikuu cha Pretoria
Profesa wa sheria wa Chuo Kikuu cha Pretoria Dire Tladi ameweka historia kwa kuwa Mwafrika Kusini wa kwanza kuchaguliwa kuwa jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ya Umoja wa Mataifa.
Rais Cyril Ramaphosa mnamo Ijumaa alisifu uchaguzi wa Prof Tladi kama "mafanikio bora ya kibinafsi ambayo taifa linashiriki kwa fahari kubwa".
Yeye ni mmoja wa majaji watano waliochaguliwa siku ya Alhamisi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kwa mihula ya miaka tisa, kuanzia Februari mwaka ujao.
ICJ ndiyo chombo kikuu cha mahakama cha Umoja wa Mataifa, kinachotoa ushauri wa kisheria kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na kutatua mizozo ya kisheria kati ya nchi.
Ili kuchaguliwa, wagombea lazima wapate wingi kamili katika Mkutano Mkuu na Baraza la Usalama.
Wagombea wengine watatu wa Kiafrika kutoka Zambia, Misri na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hawakuchaguliwa kuwania nafasi hiyo.
Rais wa Somalia afanyiwa upasuaji Abu Dhabi

Chanzo cha picha, Villa Somalia
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amefanyiwa upasuaji wa bega katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ofisi ya rais inasema.
Bw Mohamud anapata nafuu kutokana na upasuaji huo "mdogo",ofisi yake ilisema Alhamisi.Haikutoa maelezo zaidi juu ya kile kilichotokea kwenye bega lake.
Rais alikaa Abu Dhabi kwa siku chache, ambapo pia alikutana na maafisa wakuu wa Imarati, Shirika la Habari la Kitaifa la Somalia (Sonna) linaripoti.
Baadaye alisafiri hadi Riyadh, Saudi Arabia, kuhudhuria mkutano wa kilele wa Saudi-Afrika.
Tangu kuchaguliwa tena mwaka jana, Bw Mohamud amesafiri katika mataifa kadhaa, yakiwemo mataifa ya Ghuba, kutafuta uungwaji mkono kwa mashambulizi ya serikali yake dhidi ya al-Shabab.
Miili ya watu waliovalia sare za kijeshi yaripotiwa katika mitaa ya Sudan

Chanzo cha picha, Reuters
Mapigano makali yanaripotiwa kuendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, na katika eneo la magharibi la Darfur, ambako mamia wanasemekana kuuawa katika mapigano hayo yanayoendelea.
Walioshuhudia wameliambia shirika la habari la AFP kwamba miili ilitapakaa katika mitaa ya mji wa Omdurman siku ya Alhamisi katika ongezeko la hivi punde la ghasia kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
"Miili ya watu waliovalia sare za kijeshi imetanda katika mitaa ya katikati mwa jiji baada ya mapigano hapo jana," shahidi alinukuliwa akisema.
Magharibi mwa nchi hiyo, takriban watu 700 wameripotiwa kuuawa katika mapigano ya Darfur Magharibi, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Zaidi ya wengine 300 wameripotiwa kutoweka kufuatia mapigano huko El Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi, taarifa hiyo iliongeza.
Mashahidi wameishutumu RSF kwa kuwalenga na kuwaua watu wasio Waarabu katika mapigano hayo.
Ubalozi wa Marekani mjini Khartoum ulisema "umesikitishwa sana na ripoti za mashahidi wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na RSF na wanamgambo washirika".
Lakini RSF inasema haihusiki katika kile inachoelezea kama "mgogoro wa kikabila".
Maelfu ya watu wamevuka hadi Chad katika siku chache zilizopita wakikimbia mapigano hayo.
Takriban watu milioni sita wamelazimika kutoka makwao tangu vita vilipoanza katikati ya mwezi wa Aprili.
Hospitali ya Indonesia yaharibiwa baada ya shambulio Gaza - Wizara ya mambo ya nje ya Indonesia
Hospitali ya Indonesia huko Gaza imeharibiwa baada ya shambulio la roketi karibu nayo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Indonesia alisema Ijumaa.
Alibainisha kuwa lengo la shambulio hilo lilikuwa eneo la Taliza'tar, ambalo liko "karibu sana" na hospitali.
Lalu Muhammad Iqbal alisema watu watatu wa kujitolea kutoka Indonesia walikuwa kwenye chumba cha chini ya ardhi wakati shambulio hilo lilipotokea - lakini akaongeza kuwa hakupata majeraha yoyote.
"Indonesia kwa mara nyingine inalaani mashambulizi ya kinyama dhidi ya raia na vifaa vya kiraia, hasa vituo vya misaada ya kibinadamu huko Gaza," msemaji huyo aliongeza.
Sarbini Abdul Murad wa Kamati ya Uokoaji wa Dharura ya Kimatibabu (MER-C), ambayo inaendesha hospitali hiyo, aliambia kituo cha Republika cha Indonesia: "Shambulio la jana usiku lilikuwa karibu sana na Hospitali ya Indonesia, lakini si shambulio la moja kwa moja kwenye jengo kuu."
Hospitali ya Indonesia huko Gaza ilijengwa kuhudumia mahitaji ya matibabu ya Wapalestina katika eneo hilo, kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Indonesia.
Mzozo wa Israel na Palestina:Yaliyofanyika katika saa chache zilizopita

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Watoto wawili waliokimbia makazi yao wamelala chini karibu na hospitali ya al-Nasser huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza. Iwapo unajiunga nasi sasa hivi , huu ndiyo muhtasari wa ya yaliyofanyika Gaza katika saa chache zilizopita
- Marekani imesema Israel itaanza kusitisha vita kwa muda wa saa nne kila siku katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza ili kuruhusu raia kuondoka
- Kusitishwa huko ni"hatua katika mwelekeo sahihi", Rais wa Marekani Joe Biden amesema, akiongeza kuwa kutakuwa na korido mbili za kibinadamu huko Gaza kuruhusu watu kuepuka kudhuriwa
- Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema nchi yake haitaki kuteka, kukalia au kutawala ukanda wa Gaza baada ya vita na Hamas kumalizika.
- Akizungumza na kituo cha habari cha Marekani cha Fox News, alisema"kikosi cha kuaminika"kitahitajika kuingia katika eneo hilo ikiwa ni lazima ili kuzuia kutokea kwa vitisho vya wanamgambo.
- Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas huko Gaza inasema takriban watu 10,812, wakiwemo watoto 4,412 sasa wameuawa katika eneo hilo tangu Israel ilipoanza mashambulizi yake ya anga.Mashambulizi hayo yalianza kulipiza kisasi shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, ambalo liliua watu 1,400 na wengine 240 walichukuliwa mateka.
Endelea kuwa nasi tunapokuletea taarifa za hivi punde siku nzima.
Unaweza pia kusoma
Babake mchezaji kandanda Luis Díaz aachiliwa na waasi wa Colombia

Chanzo cha picha, PA Media
Babake mzaliwa wa Colombia anayeichezea Liverpool Luis Díaz ameachiliwa na waasi wa mrengo wa kushoto ambao walimteka nyara siku 13 zilizopita, vyanzo vya polisi na vyombo vya habari vya ndani vinasema.
Luis Manuel Díaz alikabidhiwa kwa maafisa wa Umoja wa Mataifa na wa Kanisa Katoliki na wanachama wa Jeshi la Ukombozi wa Kitaifa (ELN).
Alitekwa nyara tarehe 28 Oktoba katika mji wa nyumbani wa familia hiyo, Barrancas.
Mama wa mwanasoka huyo pia alikamatwa, lakini aliachiliwa ndani ya saa chache.
Vyombo vya habari vya eneo hilo vilisema Bw Díaz alikuwa amesafiri kwa helikopta ya kijeshi hadi jiji la Valledupar, ambapo alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kurejeshwa kwa familia yake.
Pia walinukuu mamlaka zikisema kwamba alikuwa katika hali nzuri ya afya, bila dalili za kuumizwa.
Kulingana na gazeti la El Tiempo, kulikuwa na matukio ya vilio katika mtaa walipokuwa wakiishi wanandoa hao, huku wanafamilia wakipakia magari yao barabarani kusherehekea.
Wengi wao walikuwa wamevalia jezi za timu ya Liverpool zenye nambari 23 na jina la Luis Díaz.
Mwanajeshi wa zamani wa Marekani afanyiwa upasuai wa kwanza duniani wa kupandikizwa jicho

Chanzo cha picha, Reuters
Madaktari wa upasuaji mjini New York wanasema kuwa wamefanya upasuaji wa kwanza duniani wa kupandikiza jicho kamili kwa mwanamume, ingawa hakuna uhakika kuwa ataweza kuona tena.
Aaron James, ambaye alinusurika kwenye ajali ya umeme , alifanyiwa upasuaji wa saa 21 ambao ulibadilisha nusu ya uso wake.
Madaktari wa upasuaji wameweza kupandikiza konea kwa mafanikio kwa miaka.
Wataalamu wameita mafanikio hayo kuwa muhimu katika azma ya kuwawezesha mamilioni ya watu kuona .
Bwana James, mfanyakazi wa laini ya umeme kutoka Arkansas, alipoteza sehemu kubwa ya uso wake wakati ilipogusa kwa bahati mbaya waya wa moja kwa moja wa volti 7,200 mnamo 2021.
Mnamo tarehe 27 Mei mwaka huu, alifanyiwa upandikizaji wa nadra wa sehemu ya uso pamoja na upandikizaji wa macho - ambao ulihusisha zaidi ya wataalamu 140 wa afya.
Madaktari wa upasuaji katika NYU Langone Health, ambao walifanya upasuaji huo mgumu, walisema Alhamisi kwamba Bw James, 46, alikuwa akipata nafuu baada ya kupandikizwa mara mbili na jicho lililotolewa lilionekana kuwa na afya tele.Jicho lake la kulia bado linafanya kazi.
Israel haina mpango wa kuteka, kukalia au kuitawala Gaza - Netanyahu

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri mkuu wa Israel anasema nchi hiyo haitaki kuliteka, kukalia au kutawala Ukanda wa Gaza baada ya vita vyake na Hamas kumalizika.
Benjamin Netanyahu alikiambia kituo cha televisheni cha Marekani Fox News kwamba "nguvu ya kuaminika" itahitajika kuingia katika eneo hilo ikiwa ni lazima ili kuzuia kuibuka kwa vitisho vya wanamgambo.
"Hatulengi kuteka Gaza, hatutaki kuikalia Gaza, na hatutaki kuitawala Gaza," alisema, akiongeza kuwa serikali ya kiraia itahitajika, lakini Israeli pia itahitaji hakikisho kwamba shambulio kama lile la Oktoba 7, ambalo Hamas liliua watu wapatao 1,400, halitokei tena.
"Kwa hiyo, tunapaswa kuwa na kikosi cha kuaminika ambacho, ikibidi, kitaingia Gaza na kuwaua wauaji. Kwa sababu hilo ndilo litakalozuia kuibuka tena kwa kundi linalofanana na Hamas," alisema.
Maoni ya Netanyahu mapema wiki hii yalikuwa yamependekeza kuwa Israeli itawajibika kiusalama usalama huko Gaza, na kutoa majibu makali kutoka kwa Marekani
Unaweza pia kusoma
Marekani yasema Israel itaanza kusitisha vita kwa muda kwa saa nne kila siku huko Gaza

Chanzo cha picha, Reuters
Israel itaanza kutekeleza usitishaji wa vita kwa saa nne kila siku katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza, msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani John Kirby alisema.
Hata hivyo waziri wa ulinzi wa Israel alisisitiza kuwa "zitakuwa hatua za ndani na kubainisha kuwa "hazitazuia mapigano ya vita".
Rais Biden alisema kutakuwa na "njia mbili za kibinadamu" zinazoruhusu watu kuondoka katika maeneo ya mapigano.
Siku ya Alhamisi mapigano makali yaliripotiwa karibu na hospitali mbili kubwa katika Jiji la Gaza.
Wakati huo huo, picha kwa mara nyingine tena zilionyesha maelfu ya Wapalestina wakikimbia kuelekea kusini kutoka mji huo na maeneo mengine ya kaskazini.
Bw Biden pia alisema Marekani inajaribu kuongeza vifaa vya kibinadamu na usaidizi kwa Gaza.Alisema analenga lori 150 za msaada kwa siku kuingia katika eneo hilo.
Hata hivyo Umoja wa Mataifa ulisema kiasi cha misaada inayoingia Gaza ilikuwa inakidhi "sehemu" tu ya mahitaji ya watu na hali ya kibinadamu "haivumiliki".Mkutano wa mjini Paris hapo awali ulisikiliza maombi ya mara kwa mara ya kusitisha mapigano huko Gaza.
Israel imekuwa ikishambulia kwa mabomu Gaza kwa zaidi ya mwezi mmoja na ilianza mashambulizi makubwa ya ardhini takriban wiki mbili zilizopita kwa lengo la kuiangamiza Hamas, ambayo Marekani na mataifa mengine yenye nguvu ya Magharibi yanaona kuwa ni kundi la kigaidi.
Vita hivyo vilianza baada ya shambulio la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel na watu wenye silaha wa Hamas tarehe 7 Oktoba, ambapo watu 1,400 waliuawa na wengine 240 kuchukuliwa mateka.
Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imesema watu 10,800 wameuawa katika eneo hilo tangu wakati huo, huku milioni 1.5 wakikimbia makwao.
Bw Biden alisema Israel "inapambana na adui aliyejikita katika raia, jambo ambalo linawaweka Wapalestina wasio na hatia hatarini" lakini Israel ina "wajibu wa kutofautisha kati ya magaidi na raia na kufuata kikamilifu sheria za kimataifa".
Unaweza pia kusoma
Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Ijumaa tarehe 10 Novemba 2023
